Wednesday, March 6, 2024

WIZARA YA MAMBO YA NJE KUSHIRIKI MAONESHO MAALUM KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inashiriki maonesho maalum ya wanawake yanayofanyika kimkoa katika viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma kuanzia tarehe 07 hadi 11 Machi 2024 ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika duniani kote tarehe 08 Machi 2024.


Maonesho hayo ambayo yanaratibiwa na  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma yatafunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Rosemary Senyamule tarehe 07 Machi 2024.


Huduma zitakazotolewa katika Banda la Wizara wakati wa maonesho hayo ni pamoja na uthibitishaji wa nyaraka mbalimbali ikiwemo vyeti vya taaluma, ndoa na nyaraka nyingine, zoezi ambalo litaanza rasmi tarehe 07 hadi 11 Machi, 2024.


Taarifa nyingine  ni kuhusu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na  mchango wa wanawake kwenye medani za kimataifa na diplomasia.

Kadhalika maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim zamani Chuo cha Diplomasia; Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) na Mpango wa Hiari wa Kujipima kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM) yatatolewa.


Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2024 yamebeba kaulimbiu isemayo "Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii". 

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Kawina Kawina akimsikiliza Afisa Mambo ya Nje, Bi. Elizabeth Bukwimba akimweleza kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya ushiriki wa Wizara kwenye maonesho maalum yatakayofanyika katika Viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma kuanzia tarehe 07  hadi 11 Machi 2024 ikiwa ni maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa duniani kote tarehe 08 Machi 2024. Bw. Kawina ametembelea banda hilo tarehe 06 Machi 2024 kukagua hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya ushiriki wa Wizara
Bw. Kawina akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wizara kukagua maandalizi  ya ushiriki wa Wizara katika maonesho maalum kuelekea siku ya wanawake duniani yanayofanyika  katika viwanja vya mashujaa jijini Dodoma kuanzia tarehe 07 hadi 11 Machi 2024. Wanaoshuhudia ni Watumishi kutoka Taasisi za Wizara akiwemo Badriya Masoud (kulia), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa APRM, Bi. Praxeda Gaspar kutoka APRM na Bi. Susan Masawe kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim


Bw. Kawina akikagua vipeperushi vitakavyogawiwa kwa wananchi watakaotembelea banda la Wizara wakati wa maonesho maalum kuelekea siku ya wanawake duniani yanayofanyika jijini Dodoma katika viwanja vya mashujaa kuanzia tarehe 07 hadi 11 machi 2024

Afisa kutoka Taasisi ya Wizara ya Mpango wa Hiari wa Kujipima kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM), Bi. Praxeda Gaspar akimpatia Bw. Kawina kipeperushi kuhusu Taasisi hiyo

Bw. Kawina akipata maelezo kutoka kwa Bi. Janeth Benedict kutoka  Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC)  kuhusu vipeperushi watakavyosambaza kwa wananchi kuhusu taasisi hiyo

Mwonekano wa Banda la Wizara



 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.