Friday, March 1, 2024

TANZANIA NA ETHIOPIA ZASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA ZA KILIMO, NISHATI NA UTAMADUNI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia la Ethiopia zimesaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za kilimo, nishati na utamaduni katika haflabiliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 01 Machi 2023.

Utiaji saini huo ambao umeshuhudiwa na Viongozi Wakuu  wa Nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia la Ethiopia, Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali ni matokeo chanya ya ziara ya Mhe. Dkt. Abiy ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu. 

Kwa upande wa Tanzania, makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na kwa upande wa Serikali ya Ethiopia makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo, Mhe.  Balozi Taye Atseke Selassie.

Hati za Makubaliano zilizosainiwa na  Mhe. Makamba ni Hati ya Ushirikiano katika sekta ya Kilimo ambayo itaanzisha ushirikiano katika utafiti wa mbegu za ngano, kubadilishana uzoefu katika teknolojia ya kilimo, kilimo cha umwagiliaji, kuhudumia mazao baada ya mavuno, kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na Kilimo cha biashara.

Pia, amesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kuhusu Biashara ya Umeme katika utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA). Hati hii imeanzisha ushirikiano katika usambazaji, biashara ya umeme na kuanzisha jukwaa la majadiliano la kuwezesha na kuanzisha biashara ya umeme utokanao na vyanzo vya maji.

Aidha, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Sanaa na Utamaduni ambapo hati hii itaanzisha ushirikiano wa pamoja katika kuendeleza sekta ya Sanaa na utamaduni ikiwemo kushirikiana katika  matamasha ya kitamaduni,  utafiti, filamu, kuongeza ujuzi kwa wadau wa sekta hiyo na   kuandaa maonesho ya Sanaa.

Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta za usafiri wa anga, nishati, Kilimo, mifugo, uhamiaji, biashara na uwekezaji, elimu, ulinzi na usalama.

    Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Ethiopia wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za kilimo na nishati kulia ni Mhe. January Makamba (Mb.) na kushoto Mhe.  Balozi Taye Atseke Selassie akisainiIkulu jijini Dar es Salaam tarehe 1 Machi, 2024..

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiaopia, Mhe.  Balozi Taye Atseke Selassie wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Sanaa na Utamaduni Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 1 Machi, 2024.








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.