Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuboresha maisha ya watanzania kupitia mageuzi mbalimbali pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbaimbali duniani ikiwemo Uturuki.
“Nilipopokea taarifa kuhusu kutunukiwa shahada hii nilijiuliza, wametumia vigezo gani hadi kufikia uamuzi huu, Waziri wangu wa Mambo ya Nje alinipatia orodha yenye vigezo hivyo nikakubali, nawashukuru sana” alisema Rais Dkt. Samia
Mhe. Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki katika kufikia malengo yake ya kukuza uchumi kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, uwekezaji na ushirikiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.
Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara kwa kauli moja liliamua kumtunukia Mhe. Rais Dkt. Samia Shahada hiyo ya heshima, kwa kutambua Uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania. Mageuzi hayo yameboresha ustawi wa Watanzania; na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni; na yamekuza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.
|
Shahada hii ni ya pili kwa Mhe. Rais Samia kutunukiwa kutoka ugenini ambapo Shahada ya kwanza ya aina hiyo alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India mwezi Oktoba 2023.
Taratibu mbalimbali zikiendelea kabla ya Mhe. Rais Samia kutunukiwa Shahada yake ya Udaktari. Pichani ni viongozi wakiwa wamesimama kwa heshima ya nyimbo za mataifa yao |
Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Chuo cha Ankara, Wakufunzi na Viongozi mbalimbali |