Monday, May 13, 2024

RAIS SAMIA AWASILI PARIS, UFARANSA KWA ZIARA YA KIKAZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Paris, Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024 na kupokelewa na Viongozi Waandamizi wa Serikali, Watumishi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Watanzania wanaoishi nchini humo.


Rais Samia ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati Safi ya kupikia barani Afrika utakaofanyika Makao Makuu ya UNESCO na kuhudhuriwa na Marais wengine wa Afrika akiwemo Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mhe. Julius Maada Bio na Rais wa Ghana, Mhe. Nana Akufo-Addo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea maua kutoka kwa mtoto Khaira Ali Jabiri mara baada ya kuwasili jijini Paris, Ufaransa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia utakaofanyika tarehe 14 Mei, 2024

Mhe. Rais Samia akisalimiana na Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Suleiman Jaffo (Mb.) mara baada ya kuwasili jijini Paris, Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024.

Mhe, Rais Samia akisalimia na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (Mb.) mara baada ya kuwasili jijini Paris, Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024.

Sehemu ya watumishi wa ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa wakisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuwasili jijini Paris, Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024.






 

Sunday, May 12, 2024

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA KIKAO CHA MAANDALIZI YA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI KUHUSU NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiongoza kikao cha maandalizi cha ujumbe wa Tanzania uliopo jijini Paris, Ufaransa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati Safi ya Kupikia utakaofanyika tarehe 14 Mei, 2024 katika Makao Makuu ya UNESCO.

Lengo la mkutano huo ni kulifanya suala zima la nishati safi ya kupikia kuwa la kipaumbele katika agenda ya kimataifa; kuanisha hatua madhubuti za kisera zitakazoharakisha matumizi ya nisahti safi ya kupikia na kutoa fursa ya washirika kutoa ahadi za kifedha, sera na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kikao hicho cha maandalizi kimefanyika katika ofisi za ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024.

Kutoka kushoto ni Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania- Diplomasia, Balozi Maulida Hassan, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Noel Kaganda na Mkuu wa Utawala na Fedha katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Bw. Amos Tengu wakifatilia kikao kilichofanyika katika ofisi za ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024. 


Wajumbe wa kikao hicho wakifatilia majadiliano.
Kikao kikiendelea. 

Kikao kikiendelea.
 

WAZIRI MAKAMBA AWASILI PARIS KUHUDHURIA MKUTANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amewasili jijini Paris, Ufaransa na kupokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Mwadini tarehe 12 Mei, 2024.

Mhe. Makamba anatarajia kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika utakaofanyika tarehe 14 Mei, 2024 katika Makao Makuu ya UNESCO.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utaongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atakuwa Mwenyekiti Mwenza kufuatia mwaliko wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (International Energy Agency). Aidha, Mhe. Rais anatarajia kuhutubia hafla ya ufunguzi ya Mkutano husika.

Wenyeviti wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati, Dkt. Fatih Birol; Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jonas Gahr Støre na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Mwadini mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Charles de Gaulle jijini Paris, Ufaransa tarehe 12 Mei, 2024.

Mheshimiwa Waziri Makamba akiwasili jijini Paris, Ufaransa kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika utakaofanyika tarehe 14 Mei, 2024.

Mhe. Waziri Makamba akizungumza na Mhe. Balozi Mwadini baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Charles de Gaulle jijini Paris, Ufaransa.

Mapokezi ya Mheshimiwa Waziri January Makamba jijini Paris, Ufaransa.


Thursday, May 9, 2024

WAZIRI MAKAMBA, WAWEKEZAJI WA ICELAND WAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Mkamba (Mb.) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Iceland yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Mkamba amefanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Iceland ambao wapo ziarani nchini kuangalia na kufanya tathimini ya fursa za uwekezaji zinazopatika katika sekta mbalimbali.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 8 Mei 2024 yalilenga kubalishana taarifa mbalimbali na uzoefu katika sekta ya biashara na uwekezaji ambazo zitawasaidia wawekezaji hao katika kufanya maamuzi kwenye utekelezaji wa mikakati ya kuwekeza nchini. 

Waziri Makamba akizungumza na wawekezaji hao ameelezea mageuzi ya kimkakati yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. 

Aliendelea kueleza kuwa licha ya mazingira tulivu ya kisiasa nchini, mageuzi yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali ikiwemo sera na sheria za uwekezaji yameendelea kuifanya Tanzania kuwa kituo bora cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

Kwa upande wake kiongozi wa msafara wa ujumbe wa wawekezaji hao Bw. Miar Gunnarsson ambaye pia ni Mwanzilishi wa Kampuni ya Baridi Group Ltd amesifu uwepo wa fursa lukuki nchini walizozibaini wakati wa zaira yao, kwenye sekta mbalimbali kama vile utalii, ujenzi, uvuvi, madini, kilimo na viwanda. 

Vilevile Bw. Gunnarsson ameeleza kuridhishwa kwakwe na kuvutiwa na jitihada zinazoendelea kufaywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ambayo yanawapelekea kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kipaumbele kwenye mipango yao ya uwekezaji. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga ameeleza kuwa pamoja na masuala mengine kuongezeka kwa kasi ya ukuaji uchumi nchini ni moja ya kigezo kinachowavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza.

Wakiwa nchini Wawekezaji hao watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi na watendaji Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Mkamba (Mb.) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Iceland yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga akifanua jambo wakati wa mazungumzo na Wawekezaji kutoka nchini Iceland yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam
Mazungumzo yakiendelea
Mazungumzo yakiendelea

Wednesday, May 8, 2024

BALOZI YAKUBU, TIC KUSHIRIKIANA KUVUTIA WAWEKEZAJI COMORO

 

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe.Said Yakubu akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw. Gilead Teri  alipowasilia katika ofisi za  TIC jijini Dar es Salaam.


Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe.Said Yakubu akizungumza kitu alipomtembelea Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw. Gilead Teri  (hayupo pichani) katika ofisi za  TIC jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe.Said Yakubu (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw. Gilead Teri  (kulia) katika ofisi za  TIC jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo yakiendelea. 
 Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw. Gilead Teri  (kulia) akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe.Said Yakubu (kushoto) machapicho mbalimbali yanayoelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini alipotembelea Ofisi za TIC jijini Dar es Salaam.

 




Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe.Said Yakubu amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw. Gilead Teri  katika ofisi za  TIC jijini Dar es Salaam.
 
Katika mazungumzo hay,  Mhe. Balozi na Bw. Teri wamejadili  namna ya kukuza uwekezaji kati ya Tanzania na Comoro ambako Balozi huyo anaenda kuiwakilisha Tanzania.
 
Kupitia mazungumzo hayo TIC imeahidi kupeleka ujumbe wa kwanza wa wawekezaji angalau 20 mwishoni mwa mwezi Juni 2024 na itashirikiana na Taasisi za sekta binafsi kuandaa ziara za wawekezaji kila mwezi kati ya Julai na Disemba 2024 kuangalia sekta mbalimbali ikiweka kipaumbele katika sekta ya  uchukuzi, fedha, afya, utalii na ujenzi.

TANZANIA YAZINDUA KAMPENI YA MGOMBEA WA NAFASI YA MKURUGENZI WA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI KANDA YA AFRIKA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akizundua kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemtangaza Mgombea wa Nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Tanzania wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akitambulisha sifa na uwezo binafsi wa mgombea huyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amesema kuwa Mhe. Ngugulile ni mgombea sahihi mwenye uwezo wa kazi na kufanya mageuzi na maboresho katika ya Sekta ya Afya.

Aidha, ameeleza kuwa Mhe. Ndugulile alipokuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Afya aliweka kipaumbele cha kusimamia suala la kutunga, kusimamia sera na kuratibu mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha usimamizi wa sekta ya afya nchini unaimarika kwa ajili ya kujenga nguvu kazi imara ya Taifa.

“Kupatikana kwa nafasi hii kutaiwezesha Tanzania kuimarika zaidi katika utekelezaji wa Diplomasia ya Afya ambayo ni muhimu katika Diplomasia yetu kwa ujumla hususan katika usimamizi wa mipango, maarifa na rasilimali ulimwenguni.’’ Waziri Makamba.

Mbali na hayo Waziri Makamba ameeleza kuwa kufauatia jitihada mbalimbali za kidiplomasia zilizofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki tayari mgombea wa Tanzania ameungwa mkono na Nchi 16 Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi zingine 7 kutoka Afrika, hivyo kuipa Tanzania mtaji wa jumla ya kula 23 katika kinyang’anyiro cha kuwania nafaisi hiyo. 

Naye Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akimwelezea mgombea huyo Mhe. Dkt. Ndugulile ameeleza kuwa akiwa Naibu Waziri katika Wizara ya Afya alifanya jitihada katika kuimarisha afya ya msingi kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka Serikalini na wadau wa maendeleo.

Ameongeza kuwa Mhe. Ndugulile alitoa mchango mkubwa kwenye usimamizi wa maboresho ya afya ya mama na mtoto na lishe na chanjo ambapo usimamizi huo umewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya wajawazito na watoto.

“Akiwa Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Ngugulile alikuwa msaidizi ambaye alitumia taaluma yake katika kushauri masuala ya afya kitaalam na hivyo kuwezesha utekelezaji wenye tija wa masuala mbalimbali katika Wizara yetu.’’ Waziri Ummy

Kwa upande wake Mhe. Ndugulile ameeleza vipaumbele vyake ambayo endapo atafanikiwa kushika nafasi hiyo atavisimamia, ambavyo ni pamoja na; afya ya mama na mtoto, kukabilina na magonjwa yasiyokuambukiza, afya ya msingi, ustahimilivu wa mazingira na mfumo endelevu wa afya, bima ya afya, uvumbuzi na utafiti na ubia na ushirikiano katika masuala ya afya.

Vilevile Dkt. Ndugulile amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumthibitisha kuwa mgombea katika nafasi hiyo hadhimu pamoja Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Afya kwa kiliratibu suala hilo kwa mafaniko makubwa.

Uzinduzi wa nafasi hiyo ya mgombea umefanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Afya, ambapo umehudhuriwa na mabalozi Afrika wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini. 

Wagombea wote Watano wanaowania nafasi hiyo watapigiwa kura na Mawaziri wa Afya wa nchi za Afrika katika Mkutano unaotarajiwa kufanyika nchini Congo Brazaville mwezi Agosti 2024 ambao utahusisha jumla ya nchi 47 za Afrika.

Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuwania nafasi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Sehemu ya mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) iliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja 
Sehemu ya Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) iliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akizundua kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizari wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) iliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) iliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Watendaji  na Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) iliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akizundua kampeni ya mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuesday, May 7, 2024

WAZIRI MAKAMBA AZUNGUMZA NA BALOZI WA SWITZERLAND NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akimsikiliza Balozi wa Switzerland nchini Mhe. Didier Chassot kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Mei 7, 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana na kuzungumza na Balozi wa Switzerland nchini Mhe. Didier Chassot leo tarehe 7 Mei 2024 katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika Mazungumzo yao viongozi hao wamejadili namna kukuza na kuimarisha ushirikiano katika

Sekta ya ulinzi na usalama kwa maslahi ya pande zote mbili na Jumuiya ya Kimataifa.

Pia wamejadili jinsi ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu athari za migogoro inayojitokeza sehemu mbalimbali duniani na kutoa mapendekezo yenye tija kwa jumuiya ya kimataifa juu ya namna bora ya kutatua migogoro hiyo ili kupunguza adhari zake kwa jamii. 

Aidha wamejadili programu mbalimbali zitakazochagiza kuimarika kwa ushirikiano huo ikiwemo ziara za mara kwa mara za viongozi wa sekta ya ulinzi na usalama na kuanda na kushiriki katika mikutano inayolenga kutatua migogoro.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Makamba ameeleza kuwa majadiliano ya utatuzi wa migogoro ni muhimu yakaangazia Bara la Afrika ambapo kwa muda mrefu Nchi nyingi kama vile DRC zimekuwa katika migogo na hazipewi kipaumbele katika mijadala ya kuleta amani inayojitokeza katika majukwaa mbalimbali ya Kimataifa.

Naye Balozi Chassot amesema Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro na kuchangia jitihada za kuleta amani sehemu mbalimbali duniani na Switzerland inaitazama Tanzania kama mdau muhimu wa kushirikiana naye kati eneo hilo. 

Balozi Chassot ametoa pole kwa Watanzania kwa hasara na uharibufu uliojitokeza kutokana na athari za mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini na kusababisha vifo, majeruhi, uharibu wa makazi na mali za watu na miundombinu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Switzerland nchini Mhe. Didier Chassot yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Mei 7, 2024.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Balozi wa Switzerland nchini Mhe. Didier Chassot wakibadilishana mawazo muda mfupi baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.

TANZANIA NA CHINA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI


Serikali ya Tanzania na China zimesisitiza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati ili kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Msisitizo huo umetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 7 Mei, 2024.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kujadili utekelezaji wa maazimio na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyofanyika nchini China mwezi Novemba 2023.  

Aidha, wameainisha maeneo mbalimbali ya kimkakati ambayo nchi hizo mbili zimedhamiria kuziendeleza na kuzisimamia kwa maenedeo ya watu wake. Maeneo hayo ni pamoja na kuanzisha na kuimarisha ushirikiano wa miji dada, kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji, ujenzi wa miji ya kisasa, maendeleo ya viwanda, kilimo cha kisasa na uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo na mifugo na kuboresha mradi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Kwa upande wake Waziri Makamba ameeleza kuwa Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na China ambapo kwa uchache alitaja baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imekuwa ikinufaika na ushirikiano huo kama vile; ushirikiano kati ya Jeshi la Ulinzi la Tanzania na China uliodumu kwa zaidi ya miaka 60.

Kuongezeka kwa muingiliano wa wananchi wa pande hizo mbili kumepelekea kukua kwa shughuli za kiuchumi hususan katika sekta ya biashara, usafirishaji na utalii.

“Tanzania imijiweka mikakati thabiti ya kuyafikia maendeleo ya viwanda, hivyo imeweka kipaumbele cha kufanikisha hilo kupitia ushirikiano wake na China” Waziri Makamba

Naye Balozi wa China nchini ameeleza kuwa China itaendeleza ushirikiano wake wa kihistoria na Tanzania ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini kwa ufanisi.

Sekta nyingine za ushirikiano kati ya Tanzania na China ni pamoja na elimu, afya, kilimo, biashara, uwekezaji, kilimo, utalii, nishati, madini, usafirishaji, mifugo na utamaduni.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) (kulia) akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian alipokutana naye kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 7 Mei, 2024.

Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian akifafanua jambo wakati alipofanya mazungumzo Mhe. Makamba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es salaam tarehe 7 Mei, 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akichangia jambo wakati wa mazungumzo hayo, kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia, Bw. Salvatory Mbilinyi.

Mazungumzo yakiendelea.