Monday, July 22, 2024

BALOZI SHELUKINDO AFUNGUA JPC YA KWANZA KATI YA TANZANIA NA COMORO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akifungua mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 22 – 24 Julai, 2024

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amefungua Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro katika Ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22-24 Julai 2024.

Akizungumza katika mkutano huo wa kihistoria, Balozi Shelukindo ameelezea kuridhishwa kwake na ukuaji wa mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ambao umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

“Mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka mitatu iliyopita kutoka Dola za Marekani milioni 6.75 mwaka 2021 hadi Dola milioni 54.67 mwaka 2023”. Alisema Balozi Shelukindo.

Balozi Shelukindo amesema ukuaji huo wa biashara ni mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa bado kuna haja kwa nchi hizo mbili kuongeza uwigo wa ushirikiano wa kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kwa tija ya pande zote mbili.

Amesema mikutano hiyo ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano inatoa fursa kwa nchi hizo mbili kupanua na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kupitia nyanja mbalimbali.

Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina nia ya dhati ya kupanua ushirikiano na Visiwa vya Comoro kupitia sekta mbalimbali, zikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, masuala ya kisheria, fedha, biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, miundombinu, TEHAMA, afya, elimu, michezo, sanaa na utamaduni.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Visiwa vya Comoro Mhe. Balozi Fatima Alfeine akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo ameeleza kuwa mkutano huo hautalenga kujadili namna ya kutatua changamo pekee bali kwa pamoja kuibua maneo mapya ya ushirikiano yatakayo chochea zaidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.

“Kutokana na uhimu wa mkutano huu wa kihistoria, ujumbe wetu umejumuisha wataalam kutoka sekta zote muhimu, kwa sababu tuna dhamira ya dhati sio tu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na undugu wa kihistoria uliopo kati yetu bali kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunaweka mazingira wezeshi na rafiki zaidi kwa wananchi wa pande zote mbili kunufaika zaidi kiuchumi kupitia fursa lukuki zilizopo”. Ameeleza Balozi Fatima Alfeine 

Mkutano huo wa siku tatu unashirikisha wadau kutoka Sekta za Diplomasia, Sheria, Ulinzi, Biashara, Kilimo, Biashara, Uwekezaji, Uchumi wa Buluu, ICT na Nishati


Kiongozi wa Ujumbe wa Visiwa vya Comoro Mhe. Balozi Fatima Alfeine akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam

Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam
Meza Kuu wakifuatilia Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ali Bujiku na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Sheria Dkt. Gift Kweka wakifuatilia mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi wa Tanzania Visiwa vya Comoro Mhe. Saidi Yakubu akichangia jambo kwenye mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu Mussa akichangia jambo kwenye mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Viziwa vya Comoro Nchini Tanzania Mhe. Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed akifuatilia mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 
Picha ya pamoja
Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam. 

Friday, July 19, 2024

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO UINGEREZA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi ya Wizara  amekagua miradi ya maendeleo iliyopo jijini London, Uingereza kuanzia tarehe 14 hadi 18 Julai, 2024.


Katika ziara hiyo Kamati imekagua jengo la ofisi, makazi na kiwanja cha serikali. Vilevile, imefanya kikao cha mashauriano na ubalozi na wataalam wa ujenzi na uwekezaji nchini humo juu ya namna bora ya kuendeleza milki hizo za Serikali.


Katika ziara hiyo Kamati pia imekabidhi nyumba moja kwa mtumishi wa Ubalozi ambayo ukarabati wake umekamilika kwa asilimia 100 na hivyo kupunguza gharama za kulipia kodi ya pango kwa Serikali ambayo imekuwa ikilipwa kabla ya kukamilika kwake. 


Ziara hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango mahsusi wa Wizara wa kuendeleza viwanja na milki zake zilizopo nje ya nchi, ambao ulielezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) wakati alipowasilisha Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma mwezi Mei, 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (wa pili kulia) akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki (wa kwanza kulia) katika ofisi za ubalozi huo jijini London, Uingereza wakati alipofanya ziara nchini humo kuanzia tarehe 14 hadi 18 Julai, 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi nyumba ya makazi iliyokamilika ukarabati kwa mtumishi wa Ubalozi jijini London, Uingereza.

Balozi Said Shaib Mussa akiongoza kikao cha mashauriano kati ya Kamati ya miradi, watumishi wa ubalozi na wataalam wa ujenzi na uwekezaji kilichofanyika jijini London, Uingereza wakati wa ziara hiyo.

Ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiendelea.

Picha ya pamoja.

Kamati ikikagua miradi.

Wednesday, July 17, 2024

TANZANIA NA OMAN ZAJIPANGA KUKUZA BIASHARA


Ubalozi wa Tanzania nchini Oman umeandaa Kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika nchini Oman kuanzia tarehe 26 – 28 Septemba 2024.  

Hayo yameelezwa wakati wa kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf kilichofanyika Julai 15, 2024.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Ghuba (GCC) na Jumuiya za kikanda ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Balozi Fatma alisisitiza pia umuhimu wa Oman kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, maarufu Sabasaba yanayofanyika kila mwaka mwezi Julai.

Kwa upande wake, Waziri Qais aliafiki mapendekezo ya Oman kushiriki maonesho ya sabasaba ambapo aliahidi kuwa atatembelea Tanzania na wafanyabiashara wakubwa ili kujionea fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini. 

Alitoa mwaliko kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuzuru Oman kwa lengo la kujionea maendeleo ya viwanda, hasa eneo la viwanda la Sohar na kujadili namna ya kuanzisha makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (MoU) baina ya pande mbili. Alipendekeza ziara hiyo kufanyika katikati ya mwezi wa Septemba au Oktoba 2024.

Viongozi hao walihimiza umuhimu wa usafiri wa moja kwa moja wa ndege ya mizigo kati ya Tanzania na Oman ili kurahisisha biashara. Kufuatia umuhimu huo, Balozi Fatma alieleza kuhusu kusainiwa kwa Mkataba mpya wa Ushirikiano wa Anga (BASA) baina ta Tanzania na Oman Julai 16, 2024 utakaoiwezesha Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kufanya safari zake nchini Oman.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi hao kuhimiza umuhimu wa kusaini Mkataba wa Kuepuka utozaji wa Kodi mara mbili ili kutimiza azma ya kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili. 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf wakikabidhiana zawadi baada ya mazungumzo yao.

 

Friday, July 12, 2024

MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC WAMALIZIKA JIJINI LUSAKA

Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) umemalizika leo tarehe 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia.

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 08 na 09 Julai 2024 jijini hapa umejadili na kupitisha agenda mbalimbali zenye lengo la kukuza na kuimarisha hali ya siasa, ulinzi na usalama katika Kanda ya SADC.

 

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe ameshukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kushiriki kikamilifu kuchangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo na hatimaye kufikia makubaliano ya pamoja.

 

Amesema licha ya kuwepo changamoto kadhaa za amani na usalama katika kanda bado ana imani kubwa na nchi wanachama kutokana na kuwa na nia ya dhati ya kuzimaliza ili kuwa na kanda yenye amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi.

 

Pia amewashukuru wajumbe hao kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha uenyekiti wa kamati hiyo na kuwaomba kumpatia ushirikiano huo na zaidi wenyekiti ajaye ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Januari Makamba.  

 

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kusimamia na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

 

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa ameongozana na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda,  Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa amesimama na viongozi wengine wa Tanzania kutoa heshima kwa wimbo wa Taifa wa Zambia na ule wa SADC wakati wa hafla ya kufunga rasmi Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) uliofanyika Lusaka tarehe 11 na 12 Julai 2024
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe akifunga rasmi Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo
Mhe. Makamba akimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbekwa kuendesha Mkutano huo kwa mafanikio
Mhe.Makamba akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Tanzania na wajumbe kutoka DRC walioshiriki Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
Mhe. Makamba akijadili jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe, Daniel Sillo pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Uslama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024