Friday, July 12, 2024

MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC WAMALIZIKA JIJINI LUSAKA

Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) umemalizika leo tarehe 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia.

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 08 na 09 Julai 2024 jijini hapa umejadili na kupitisha agenda mbalimbali zenye lengo la kukuza na kuimarisha hali ya siasa, ulinzi na usalama katika Kanda ya SADC.

 

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe ameshukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kushiriki kikamilifu kuchangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo na hatimaye kufikia makubaliano ya pamoja.

 

Amesema licha ya kuwepo changamoto kadhaa za amani na usalama katika kanda bado ana imani kubwa na nchi wanachama kutokana na kuwa na nia ya dhati ya kuzimaliza ili kuwa na kanda yenye amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi.

 

Pia amewashukuru wajumbe hao kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha uenyekiti wa kamati hiyo na kuwaomba kumpatia ushirikiano huo na zaidi wenyekiti ajaye ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Januari Makamba.  

 

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kusimamia na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

 

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa ameongozana na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda,  Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa amesimama na viongozi wengine wa Tanzania kutoa heshima kwa wimbo wa Taifa wa Zambia na ule wa SADC wakati wa hafla ya kufunga rasmi Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) uliofanyika Lusaka tarehe 11 na 12 Julai 2024
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe akifunga rasmi Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo
Mhe. Makamba akimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbekwa kuendesha Mkutano huo kwa mafanikio
Mhe.Makamba akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Tanzania na wajumbe kutoka DRC walioshiriki Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
Mhe. Makamba akijadili jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe, Daniel Sillo pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Uslama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024


















 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.