Monday, July 8, 2024

MAANDALIZI YA MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC YAANZA JIJINI LUSAKA

Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unatarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia. 

 

Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 08 na 09 Julai 2024 jijini hapa ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.

 

Mkutano wa 26 unalenga pamoja na mambo mengine kujadili agenda mbalimbali zenye lengo la kukuza na kuimarisha hali ya siasa, ulinzi na usalama katika Kanda ya SADC.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mulungushi jijini Lusaka, Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Gundersen amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo na kuwataka kujadili kikamilifu agenda mbalimbali zilizopo mbele yao kabla ya kuziwasilisha kwa Mawaziri.

 

Aidha, kuhusu hali ya usalama na amani katika Kanda ya SADC, Bi. Etambuyu amesema kuwa, hali ni shwari huku akisisitiza kuendelea na jitihada za pamoja ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika maeneo machache yenye changamoto za kiusalama katika kanda ikiwemo eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Kadhalika ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa kuendesha kwa amani na utulivu zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge lililofanyika katika nchi hizo hivi karibuni.

 

Mbali na Balozi Shelukindo, viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda,  Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye pia ni Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Gundersen akifungua rasmi mkutano huo uliofanyika tarehe 8 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia. Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 8 na 9 Julai 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe (kushoto) akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni (kulia) wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lusaka, Zambia
Balozi Shelukindo akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri wakati akifafanua jambo kwake kuhusu agenda za mkutano
Ujumbe wa Zambia ambao ni wenyeji wa Mkutano huo wakishiriki hafla ya ufunguzi

Ujumbe wa  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu

Ujumbe wa  Madagascar wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu

Ujumbe wa Malawi wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu
Ujumbe wa Angola wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu
Ujumbe wa  Lesotho wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu
Ujumbe wa  Botswana wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu
Ujumbe wa  Msumbiji wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu
Ujumbe wa Shelisheli wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi. Talha Waziri akifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC

Mkutano ukiendelea






 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.