Saturday, September 7, 2024

RAIS SAMIA AWAHIMIZA DIASPORA KUWEKEZA NCHINI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

· Atumia saa 7 kuongea na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora) kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini. 

Rais Samia ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na Diaspora waishio nchini China katika mkutano uliojumuisha watanzania wanaofanya kazi nchini humo, wafanyabiashara na wanafunzi uliofanyika jijini Beijing tarehe 6 Septemba 2024.

Akizungumza na Diaspora hao waliojitokeza kwa wingi, wakionesha furaha na shauku kubwa ya kuzungumza na Rais Samia, aliwaeleza kuwa licha ya fursa lukuki za kiuchumi zilizopo nchini Serikali imefanya maboresho ya sera na sheria mbalimbali ili kutoa fursa na kutanua wigo kwa Diaspora kuwekeza nchini.

Rais Samia amezitaja fursa hizo zinazopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, viwanda, kilimo na madini. Aliongeza kufafanua kuwa, katika sekta ya ujenzi hivi sasa Serikali imeandaa utaratibu mahususi kwa Diaspora, unaowapa fursa ya kujengewa na kumiliki nyumba nchini. 

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaeleza Diaspora kuhusu hatua liyopigwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma za kijamii kwa Wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, na usafirishaji akitolea mfano wa treni iendayo kwa haraka (SGR) ambayo katika kipindi kifupi imeleta mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo na ujenzi wake ukiwa unaendelea. Sekta zingine ni nishati, kilimo, maji, mawasiliano na ukuaji wa demokrasia.

“Nyumbani tuko vizuri, mfano sasa hivi safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma inachukua saa 3 hadi 4 pekee kwa kutumia treni yetu mpya tuliyoizindua hivi karibuni. Tumefanya maboresho makubwa ya sera na sheria ili kuwapa fursa ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa urahisi. Njoeni muwekeze nymbani”. Alisema Rais Samia.

Mbali na hayo amepongeza juhudi na uzalendo unaoendelea kuonyeshwa na Diaspora katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini ikiwemo kuleta watalii, wawekezaji na kusaidia kuratibu shughuli za matibabu. Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la fedha zinazotumwa nyumbani (remittance) kutoka ughaibuni,

Vilevile, Rais Samia ametoa wito kwa Diaspora wa nchini humo na kwa nchi zingine, hususan kwa jamii ya wanafunzi kujiandisha katika vyama vyao vya Jumuiya kwenye maeneo waliyopo. Akasisitiza kuwa hatua hiyo hiyo, licha kusadia kutambuana na kukuza umoja wao inarahisisha namna ya kuwafikia wanapohitaji huma mbalimbali hasa wakati zinapotokea changamoto ikiwemo majanga kama vile mlipuko wa magonjwa. 

Katika hatua nyingine Rais Samia akiwa jijini Beijing amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni Sita (6) makubwa ya nchini humo ikiwemo China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC), Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND jijini Beijing, tarehe 06 Septemba, 2024.

Katika zoezi hilo alilolifanya kwa takribani saa 7 mfulilulizo bila mapunziko, aliambatana na Watendandaji na Mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali wakiwemo; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mb.), Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb.), Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega (Mb.).

Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb.) Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed Khamis Abdullah na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Bw. Gilead Teri.

Rais Samia alikuwa nchini China kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika tarehe 4-6 Septemba 2024. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza Diaspora kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo,akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.
 Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Felista Rugambwa (katika) akifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na watazania wanaoishi nchini China (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika jijini Beijing.

Matukio mbalimbali katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania waishio nchini China (Diaspora) uliofanyika Jijini Beijing tarehe 06 Septemba, 2024.






Matukio mbalimbali wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungu na Wawekezaji na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC) pamoja na Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND ya nchini China jijini Beijing, China tarehe 06 Septemba. 



Thursday, September 5, 2024

CHINA KUTOA USD 50 BILIONI KUSAIDIA MAENDELEO AFRIKA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China.


· Asisitiza kutoingilia masuala ya ndani ya nchi
· Ahaidi hakuna Taifa likakalosalia nyuma katika safari ya maendeleo
· Ataja vipaumbele 10 vya ushirikiano wa kimkakati na Afrika

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping ametangaza kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 zitakazo elekezwa kusaidia masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mataifa ya barani Afrika. 

Ahadi hiyo imetolewa leo tarehe 5 Septemba 2024 alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) jijini Beijing. 

Akifungua mkutano huo Rais Xi Jinping ameeleza kuwa kiasi hicho kitaelekezwa katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya pande zote mbili bila kuathiri misingi na taratibu za Taifa husika. Aidha, aliongeza kusema kwamba kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika maeneo kumi (10) ya kipaumbele ya ushirikiano wa kimkakati na Afrika. Aliendelea kwa kuhimiza umuhimu wake katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na usasa huku akisisitiza kuwa hakuna Taifa litakalo baki nyumba katika maendeleo hayo. 

Rais Xi Jinping ameyataja maeneo hayo ya ushirikiano wa kimkakati kuwa ni ubia katika ushirikiano wa maendeleo (partnership action for development cooperation), Afya (partnership action for health), kilimo na ustawi (partnership action for agriculture and livelihood), mwingiliano wa watu na watu (partnership action for people to people exchanges), maendeleo ya kijani (partnership action for green development) na masuala ya ulinzi na usalama (partnership action for common security). 

Maeneo mengine yaliyoainishwa ni ushirikiano katika viwanda (partnership action for industrial chain cooperation), mawasiliano (partnership action for connectivity), ubia katika kukuza biashara (partnership action for trade prosperity) na ubia katika mafunzo (Partnership Action for Mutual Learning among Civilizations).

Aidha Rais Xi Jinping amefafanua kuhusu mgawanyo wa dola za Marekani bilioni 50 zitakazotolewa kama ifuatavyo, bilioni 29 zitaelekezwa katika mikopo, bilioni 11 zitaelekezwa kwenye misaada ya aina mbalimbali na bilioni 10 zitaelekezwa katika uwekezaji kupitia makampuni ya China yatakayoenda kuwekeza katika Nchi mbalimbali barani Afrika.

Ni zama mpya za ushirikiano na usasa kati ya China na Afrika, ushirikiano na urafiki wetu uliodumu katika miongo mingi na kuleta aina mpya ya ubia na ushirikiano katika jumuiya ya mataifa sasa tumefanikiwa kufika katika hatua ya juu ya ushikiano wa kimkakati. Nawahakikishia ninyi wote ndugu na marafiki zangu tuliokusanyika hapa kuwa hakuna Taifa lolote litakalo salia nyuma katika safari hii ya usasa (modernization).Ameeleza Rais Xi Jinping. 



Mbali na hayo Rais Xi Jinping ametaja hatua kadhaa zinazotarajiwa kuchukuliwa na Serikali yake katika kipindi cha miaka 3 ijayo (2025-2027) katika kufikia adhima yake ya kusaidia kuleta mageuzi ya maendeleo na usasa barani Afrika ikiwemo utekelezaji wa miradi 30 ya nishati safi, miradi 30 ya mawasiliano, programu 500 za kilimo cha kisasa na kutoa fursa 60,000 za mafunzo hasa kwa vijana na wanawake. 

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amehutubia mkutano huo ambao ulipata mwitikio mkubwa kutoka kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika, viongozi na watendaji kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa, huku ukifuatiliwa na mamilioni ya watu kote duniani. Rais Samia amehutubia mkutano huo akiwakilisha kanda ya Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake Rais Samia ameeleza kuhusu umuhimu wa ushikirikiano wa kimkakati katika kuchagiza maendeleo na kutoa wito kwa pande zote mbili kuendelea kuunganisha nguvu ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Marais wengine kutoka Afrika waliohutubia mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Matamela Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Mheshimwa Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania, Mheshimiwa Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo na Mheshimiwa Bola Ahmed Adekunle Tinubu wa Nigeria. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika jijini Beijing, China tarehe 05 Septemba, 2024
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping akifungua Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 05 Septemba, 2024

Wednesday, September 4, 2024

HATI YA MAKUBALIANO YA KUBORESHA RELI YA TAZARA YASAINIWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema kwa pamoja wameshuhudia uwekaji saini wa hati ya makubaliano (MoU) ya kuboresha reli ya TAZARA uliofanyika katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, tarehe 4 Septemba, 2024.

Kwa upande wa Tanzania zoezi la uwekaje saini limefanywa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping pamoja na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema wakishuhudia uwekaji saini wa hati ya makubaliano ya kuboresha reli ya TAZARA katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, tarehe 4 Septemba, 2024.

RAIS SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA CHINA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ameambatana na ujumbe wake amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Xi Jinping katika ukumbi wa The Great Hall of the People jijini Beijing, Septemba 4, 2024.

Katika mazungumzo hayo Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping ameutaja uhusiano wa Tanzania na China kuwa ni wa mfano barani Afrika.

Mheshimiwa Rais Samia yupo nchini China kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)













Tuesday, September 3, 2024

WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA MAWAZIRI WA FOCAC.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakipitia nyaraka za mkutano wa Mawaziri wa FOCAC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (9th Ministerial Conference of the Forum on China-Africa Cooperation) uliofanyika tarehe 3 Septemba 2024 jijini Beijing, China.

Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili na kupitisha agenda za Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) unaotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Septemba 4-6, 2024. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China ambaye pia ni mwenyeki mwenza wa mkutano huo Mhe. Wang Yi ameeleza kuwa ushirikiano wa China na Afrika hautazamwi kuwa ni wakindugu na urafiki pekee bali unalenga kuchagiza kasi ya maendeleo ya pande zote mbili kwa kutatua changamoto zinazokabili jamii.

Ameongeza kuwa FOCAC limekuwa jukwaa muhimu linalotoa fursa hadhimu kwa Viongozi wa China na Afrika kukutana na kujadili kwa pamoja masuala muhimu ya kimkakati kwa mustakabali mwema wa mataifa hayo na watu wake. 

Vilevile Waziri Wang ameeleza kuridhishwa kwake na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala yaliyokubaliwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal ikiwemo kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu,viwanda na kilimo, biashara na uwekezaji, ubunifu na teknolojia. 

Kwa upande wake Waziri Mambo ya Nje wa Senegal ambaye pia ni mwenyeketi mwenza wa mkutano huo Mhe. Yacine Fall ameeleza kuwa China ni mshirika wa kimkakati wa maendeleo kwa Mataifa ya Afrika hivyo uhusiano wa kindungu uliopo kati ya pande hizo mbili unapaswa kudumishwa na kulindwa daima kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Aidha, mkutano huo kwa kauli moja umepitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC, rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji na tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bi. Felista Lugabwa ukiongozwa na Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akifuatilia Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika jijini Beijing, China, tarehe 3 Septemba 2024.
 Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika ukiendelea jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Musalia Mudavadi muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano 9 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika

Monday, September 2, 2024

WAZIRI KOMBO AWASILI NCHINI CHINA KUSHIRIKI FOCAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili Jamhuri ya Watu wa China leo tarehe 2 Septemba 2024 kushiriki katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba 2024.

Mkutano huo unaolenga kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika utatanguliwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika leo tarehe 2 Septemba 2024, ambapo Tanzania imekilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samuel Shelukindo na ngazi ya Mawaziri tarehe 3 Septemba 2024.

Katika mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri miongoni mwa masuala mengine, kipaumbele ni kujadili na kupitisha rasimu ya agenda ya Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC.

Agenda zingine ni pamoja na kufanya tathimini ya utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika mkutano wa 8 wa FOCAC uliofanyika jijini Dakar, Senegal, na kujadili na kupitisha rasimu ya tamko na mpango wa utekelezaji. 

Mbali na kushiriki mkutano wa FOCAC, Waziri Kombo anatarajiwa kufanya mikutano ya pembezoni na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchini Algeria, Egypt na Libya ambapo watajadili masuala mbalimbali yanayolenga kudumisha na kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia. 

Mkutano huu unaofanyika kwa mara ya 9 tokea kuanzishwa kwake mwaka 2000, unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja”. Kauli mbiu hii inalenga kuwahamasisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na China kujadili kuhusu masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China ili kuchagiza kasi ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing Waziri Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar muda mfupi baada ya kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian muda mfupi baada ya kuwasili jijini Beijing, China.

Sunday, September 1, 2024

RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA INDONESIA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia na sehemu nyingine duniani kuja kuwekeza nchini katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hususan kwenye maeneo ya Utalii, Bandari, Uvuvi na Kilimo cha Baharini, Uchukuzi na uchimbaji wa Mafuta na Gesi.

 

Mhe. Rais Mwinyi ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali, Indonesia leo tarehe 1 Septemba, 2024.

 

Mhe. Rais Mwinyi ambaye yupo nchini hapa kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa la Pili la Ushirikiano wa Indonesia na Afrika amesema, Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kwenye sekta ya uchumi wa buluu duniani na kwamba Tanzania imejipanga kunufaika kupitia sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wawekezaji kutoka Indonesia na kwingine duniani.

 

 “Tunaamini kwamba uzoefu uliowawezesha Indonesia kupiga hatua kubwa kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu utatuwezesha na sisi kujifunza na kufanikiwa. Hivyo tumekuja kuwaonesha na kujifunza  kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua kwenye maeneo niliyozungumzia ikiwemo Uvuvi, kilimo cha mwani, uchukuzi, utalii na uchimbaji wa mafuta na gesi” amesema Mhe. Rais Mwinyi.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury amesema Sera ya Mambo ya Nje ya Indonesia na ile ya Tanzania zinafanana kwa kiasi kikubwa ambapo zote zinasisitiza katika kuchochea maendeleo kupitia diplomasia ya uchumi. Hivyo, Kongamano hilo ni njia mojawapo ya kutekeleza sera hizo katika kuhamasisha uwekezaji na biashara ili kuinua uchumi wa nchi hizi mbili.

 

Pia alimshukuru Mhe. Rais Mwinyi na ujumbe wake kwa kushiriki Kongamano hilo ambalo linalenga kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika sekta ya uchumi wa buluu kwa manufaa ya pande mbili.

 

Wakati wa Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), mada mbalimbali kuhusu uwekezaji ziliwasilishwa na Taasisi za Tanzania ikiwemo ZIPA na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 

Ujumbe wa Mhe. Rais Mwinyi ulioshiriki Jukwaa hilo unamjumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Amina Khamis Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Indonesia.

 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika utafanyika jijini Bali, kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali tarehe 1 Septemba 2024 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika litakalofanyika nchini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024. Mhe. Rais Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa hilo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (kulia) akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi naye akishiriki Kongamano hilo. 
Mhe. Rais Dkt. Mwinyi akiwa ameongozana na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele mara baada ya kuwasili kwa ajilio ya kushiriki Kongamano la  Biashara kati ya Zanzibara na Indonesia lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. John Kambona akiwa na Afisa Dawati kutoka Idara hiyo, Bw. Suleiman Magoma wakishiriki Kongamano la Biashara
Sehemu ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia wakishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia, Bw. Suleiman Saleh akishiriki Kongamano hilo
Picha ya pamoja
 

Saturday, August 31, 2024

RAIS DKT. MWINYI AWASILI INDONESIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasili jijini Bali,Indonesia leo tarehe 31 Agosti 2024 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Pili la Indonesia na Afrika unaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Mariam Mwinyi pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali alipokelewa na Naibu Waziri  wa Biashara wa Indonesia Mhe, Jerry Sambuaga. 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika ambao utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Bandung Spirit for Africa's Agenda 2063,” unalenga kuangazia kanuni za pamoja ambazo zimeweka msingi imara wa kuwa na uhusiano jumuishi, usawa na endelevu kati ya Indonesia na Afrika. 

Maeneo muhimu ya ushirikiano yanayotarajiwa kujadiliwa katika Jukwaa hilo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, nishati, uchumi wa buluu, madini, afya na ushirikiano wa maendeleo.

Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Rais Mwinyi atafanya ziara ya kikazi nchini Indonesia kuanzia tarehe 04 hadi 06 Septemba 2024.