Friday, November 1, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUKUZA MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI KIKANDA NA KIMATAIFA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) ameliambia Bunge kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza na kutangaza Lugha ya Kiswahili duniani ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha matumizi ya Lugha hiyo katika Taasisi za Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha inafundishwa kama taaluma ili kuzalisha wakalimani bora.

 

Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo Bungeni, jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2024 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hawa Subira Mwaifunga aliyetaka kujua kwa nini Lugha ya Kiswahili haitumiki kwenye Jukwaa la Wabunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) kama inavyotumika kwenye Bunge la Afrika (PAP).

 

Mhe. Chumi ambaye alizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, mwezi Julai 2024,  amesema kuwa Tanzania imeendelea  na jitihada mbalimbali za kukuza Lugha ya Kiswahili na kufanikisha Lugha hiyo kuridhiwa  na SADC kama lugha ya kazi katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo tangu mwaka 2019, huku ikiendelea na jitihada za kukiwezesha Kiswahili kutumika katika Mikutano ya ngazi ya Makatibu Wakuu na Taasisi nyingine za SADC ikiwemo Jukwaa la Wabunge la SADC.

 

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mwaifunga, kuhusu changamoto kwa Serikali katika kugharamia wakalimani ili kukitangaza Kiswahili, Mhe. Chumi amesema kwamba Serikali kupitia ushawishi wake, imefanikiwa kujenga hoja ya kushirikiana na SADC katika kugharamia wakalimali na hoja hiyo kukubalika ambapo sasa SADC inagharamia wakalimani  katika mikutano yote inayoendelea chini ya Jumuiaya hiyo.

 

“Kuhusu wakalimani, ni kweli kuna gharama kubwa za kugharamia suala zima la ukalimani. Hata hivyo, kwa ushawishi Serikali imefanikiwa kujenga hoja ili kusudi mzigo huo uweze kubebwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na SADC na kwa sasa SADC katika mikutano inayoendelea wamekubali kugharamia wakalimani,” alisema Mhe. Chumi.

 

Kadhalika ameongeza kusema, ili lugha iwe rasmi yapo mabadiliko ya kanuni na miongozo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ndani ya SADC na kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kipengele hicho kinafanyiwa marekebisho ili kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya SADC.

 

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mhe. Anatropia Lwehikila kuhusu mikakati ya Serikali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa wakalimani kutoka Tanzania, Mhe. Chumi amesema kuwa, ukalimani ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine na kutoa wito kwa wadau mbalimbali vikiwemo Vyuo chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwekeza katika kuhakikisha mafunzo ya ukalimani yanatolewa kama taaluma ili kuwawezesha wakalimani kutoka Tanzania kukidhi vigezo vinavyotakiwa na kutumiwa katika mikutano mbalimbali duniani.

 

‘Ukalimani ni taaluma, kujua Kiswahili na Kiingereza kama lugha haitoshi kukufanya kuwa mkalimani.  Hivyo, natoa wito kwa Vyuo vyetu nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha wanatoa mafunzo ya ukalimani kama taaluma ili na sisi tunapokwenda katika mikutano mbalimbali duniani tukutane na wakalimani ambao ni watanzania’ alisisitiza Mhe. Chumi.

 

Kadhalika amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya  Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania  (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na Balozi za Tanzania imeendelea na jitihada za kutangaza Kiswahili kama bidhaa kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa ikiwemo makongamano, mikutano pamoja na kuwa na madawati ya kiswahili kwenye Balozi za Tanzania na kuzishawishi Balozi zinazowakilisha nchi zao hapa Tanzania kuwa na madawati ya namna hiyo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akizungumza wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 1 Novemba 2024.
Mhe, Chumi akijibu swali Bungeni



 

Wagonjwa wa Moyo kutoka Malawi Kutibiwa JKCI

Serikali ya Jamhuri ya Malawi imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wa moyo waliopo nchini humo hasa watoto kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Mhe. waziri Chiponda ambaye pia kitaaluma ni mfamasia alisema ameridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwani ameona vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo, amekutana na wataalamu wabobezi ambao wanatibu moyo na kuipongeza JKCI kwa kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo.

 “Nimefurahi sana kufika hapa nimeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yenu pamoja na huduma inayotolewa ni jambo la kufurahi na kushangaa kuona huduma hii inapatikana Afrika tena katika nchi jirani ya Tanzania, tukirudi nyumbani tutaona namna ya kuwa na makubaliano na taasisi hii ili wagonjwa wetu waje kutibiwa hapa hasa watoto”.

“Ninawashukuru wataalamu wa taasisi hii kwani mmekuwa mkiwahudumia wagonjwa kutoka nchini Malawi ninawaomba mzidi kuwahudumia kwani tunahitaji msaada wenu tunafurahi kuona baada ya kupata matibabu wagonjwa wanarudi nyumbani wakiwa na furaha. Pia ninawaomba mje nchini kwetu japo kwa wiki mbili kufanya kambi za matibabu ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”, alisema waziri Chiponda.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo Dkt. Angela Muhozya alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea JKCI na kusema kuwa watahakikisha wanatoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi wenye matatizo hayo.

Dkt. Angela alisema mwaka jana wataalamu wa taasisi hiyo walikwenda nchini Malawi katika hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo katika nchi hiyo kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ambapo waliona watu 724 kati ya hao waliokuwa na matatizo ya moyo walikuwa 537.  

“Taasisi yetu imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika hasa zile tunazopakana nazo mipaka ikiwemo ya Malawi hadi sasa tumeona wagonjwa 33 kutoka nchini hiyo ambapo watu wazima walikuwa 22 na watoto 11”.

“Licha ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo taasisi yetu pia inatoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa afya, ninawaomba muwatume madaktari na wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba vya moyo waje kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kutumia vifaa hivyo”, alisema Dkt.Angela.

Kwa upande wake balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola alisema wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutangaza diplomasia ya uchumi inayojumuisha mipango ya kuinufaisha nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

“Wenzetu kutoka nchini Malawi wamekuja Tanzania kuhudhuria mkutano wa MERCK Foundation nasi tukaona tutumie nafasi hii kuwaleta JKCI ili waone huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, wamefika hapa wameziona na kuzitambua hii itasaidia kuwashawishi wamalawi kuja kutibiwa moyo nchini kwetu”, alisema Mhe. Balozi Agnes.

Mhe. Balozi Agnes alisema Tanzania imepiga hatua katika sekta ya afya kwani wananchi wanapata kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu wao kama ubalozi wataendelea kuwashawishi wamalawi kuja kutumia huduma za matibabu ya zilizopo nchini. 



AICC NI MUHIMILI WA SEKTA YA UTALII NCHINI


Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kimeelezwa kuwa ni moja ya muhimili muhimu katika kufanikisha agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 31, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo alipokutana na uongozi wa kituo hicho chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe.

Mhe. Londo alisema kuwa Rais Samia amelipa umuhimu mkubwa suala la utalii ndiyo maana amecheza filamu ya Tanzania: The Royal Tour, na manufaa yake yameaanza kupatikana kwa kuongezeka kwa watalii na fedha za kigeni nchini.

 "Utalii una maeneo mengi na moja kati ya hayo maeneo ni utalii wa mikutano. Hivyo, kwa  Tanzania hakuna taasisi nyingine inayotegemewa na Serikali kulitekeleza kwa ufanisi eneo hili na kulitolea  miongozo isipokuwa AICC pekee", Waziri Londo alisema.

Mhe. Londo aliongeza kuwa AICC ndiyo sura na kioo cha nchi na ni moja ya kituvu cha diplomasia ya Tanzania, hivyo,  endapo watumishi wa kituo hicho watajituma kwa kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa, basi watakuwa wamelitangaza vyema jina la Tanzania. 

"Mnapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi, wanaokuja kushiriki mikutano. Wageni hawa, wengi wao huwa hawapati fursa ya kwenda sehemu yoyote zaidi ya AICC kutokana na ratiba za mikutano, maana yake wakiridhika na huduma zenu, mtakuwa mmelitangaza jina la Tanzania na kinyume chake mtakuwa mnalibomoa jina la Tanzania" Mhe. Londo alitahadharisha.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Mwakatobe ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, amesema kuwa malengo yake ni kukifanya kituo hicho kuwa taasisi namba moja nchini, Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau ili aweze kufanikisha lengo hilo.

Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho kama vile uchakavu wa miundombinu, kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi, ameanza kuchukua hatua ya kufanya maboresho ya majengo na ununuzi wa vifaa vya kisasa kama vile vifaa vya ukalimani, vyoo na vipoza joto.

Aidha, amesema  kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao, Kituo kimeanza kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili shughuli zote ziweze kufanyika kidigitali kwa lengo la kuongeza mapato na kuleta ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja. 

Amemalizia kwa kusema kuwa mapato ya kituo hicho yameongezeka kwa kupata faida ghafi ya bilioni 6.5 mwaka 2023/2024 ukilinganisha na faida ya bilioni 1.7 mwaka 2022/2023.

Mhe. Naibu Waziri Londo kabla ya kufanya kikao na menejimenti ya AICC alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na kituo hicho. Maeneo hayo ni pamoja na Kijenge site D 1 lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 21, Kijenge site E lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48 na Soweto ambapo pia kuna makazi na ukubwa wa ekari zaidi ya 50. 

Mhe. Naibu Waziri baada ya kuona maeneo hayo ambayo yote yapo katikati ya jiji la Arusha, amesema kuwa AICC ina uwezo wa kulibadilisha jiji hilo endapo rasilimali hizo zitatumiwa ipasavyo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Menejimenti ya Kituo  cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Aliyesimama ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe akiwasilisha taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya AICC.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisisitiza jambo alipozuru eneo Kijenge lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48. Eneo hilo inamilikiwa na linapatikana katikati ya jiji la Arusha.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe kabla ya Mhe. Naibu Waziri hajaanza ziara ya kukagua miradi ya kituo hicho jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika eneo lingine la makazi linalomilikiwa na AICC ambalo pia lipo Kijnege. eneo hili lina ukubwa wa ekari 21 pia linapatikana katikati ya jiji la Arusha.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo (kulia) akiwa katika moja ya maeneo ya AICC. Anayetoa maelezo kwa Mhe. Naibu Waziri ni Afisa Mwandamizi wa Kituo hicho, Bw. Assah Mwambene. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili AICC kwa ajili ya kufahamu shgughuli za kituo hicho. Anayemwangalia ni Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe

 

Thursday, October 31, 2024

SERIKALI IPO TAYARI KUPOKEA MAPENDEKEZO YA KUFANIKISHA MPANGO WA BIMA YA AFRYA KWA WOTE, WAZIRI MKUU


Serikali imewahakikishia wananchi kuwa ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote, na kutoa wito kwa washiriki wa kongamano la mpango wa bima ya afya kwa wote na mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya kuja na mapendekezo yatakayosaidia kutimiza dhamira hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) wakati anafungua matukio hayo mawili yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Matukio hayo yanayofanyika kwa siku nne hadi Novemba 1, 2024 yamekusanya wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi ili kwa pamoja kujadili mikakati na mbinu bora zitakazoiwezesha Serikali kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi, anakuwa na bima ya afya itakayomwezesha kupata matibabu bila kuangalia kipato chake.

Waziri Mkuu ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali katika hafla hiyo ya ufunguzi, wakiwemo Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) na viongozi wa mkoa wa Arusha, amesema kuwa Serikali imejiandaa vyema kutekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Imeelezwa kuwa tokea aingie madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya trillion 6.2 zimeelekezwa katika sekta ya afya. Fedha hizo zimetumika kujenga miundombinu kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ununuzi wa vifaa tiba na kuwapatia ujuzi na elimu watumishi wa sekta ya afya.

Umetolewa mfano kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, nchi ilikuwa na upungufu wa madaktari bingwa 2989, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tu, kupitia Ufadhili wa Mama Samia (Samia Scholarships), madaktari bingwa 1485 wamesomeshwa na kupunguza upungufu huo kwa takribani nusu.

Mhe. Waziri Mkuu amesema uwepo wa madaktari hao, ujenzi wa hospitali za ngazi mbalimvali pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa umeiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kufanya tiba za kibingwa kama vile upandikizaji wa figo, uboho, mimba na vifaa vya kusikia ambapo awali tiba hizo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi.

Eneo lingine ambalo Serikali imeliimaalisha ni upatikanaji wa dawa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Imeelezwa kuwa upatikanaji huo unatofautiana ambapo unaanzia asilimia 75 katika zahanati hadi 98 kwa hospitali za rufaa. Bohari Kuu ya Dawa imejenga vituo kila kanda na baadhi ya halimashauri ili kurahisisha usambazaji wa dawa katika maeneo husika.

Waziri Mkuu amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya afya umepunguza vifo kwa asilimia 20 hadi 30 na matarajio ni kwamba mpango wa bima ya afya kwa wote utakapokamilika utapunguza zaidi vifo nchini.

Waziri Mkuu alihitimisha hotuba yake kwa kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afrya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote, ili itakapoanza kusiwe na mtu atakayeachwa nyuma.   

Awali, Mhe. Naibu Waziri Londo alisema kuwa kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu ufadhili wa sekta ya afya ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliyoyatoa wakati wa mkutano wao uliofanyika jijini Dar Es Salaam mwezi Mei 2024. Aidha, ameongeza kuwa mdahalo huo ni mwendelezo wa vita vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga,

Matukio hayo yamehudhuriwa na wadau wa maendeleo na nchi marafiki kama vile Shirika la Afya Duniani, Mfuko wa Afya, Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), Jamhuri ya Korea, Indonesia, Rwanda ambao wameahidi kuwa watashirikiana na Serikali ya Tanzania katika safari yake ya kufikia bima ya afya kwa kila mwananchi.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akiwasilisha hotuba kwa washiriki wa kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akitoa neno kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kutoa hotuba ya ufunguzi katika kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) akitoa neno katika kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo wakiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, Bi. Christine Mwakatobe

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, Bi. Christine Mwakatobe (wa pili kushoto) wakiwa na watumisha wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaoshiriki  kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia hotuba mbalimbali wakati wa ufunguzi wa kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.

Hadhira ikifuatilia

Washiriki mbalimbali wakifuatilia kongamano la Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili katika sekta ya afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha Oktoba 30, 2024.


 

TANZANIA NA CUBA ZASISITIZA KUKUZA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI

 

Serikali ya Tanzania na Cuba zimesisitiza kukuza ushirikiano wa kimkakati ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania  na Hayati, Fidel Castor Ruz wa Cuba.

 

Msisitizo huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 30 Oktoba 2024 katika Kikao cha Ngazi ya Wataalamu ambapo ujumbe wa Tanzania ulishiriki kikao hicho katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Naomi Mpemba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameeleza kuwa na imani na wajumbe wa mkutano huo na kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana kwa dhati na Cuba kwa ajili ya maendeleo endelevu na ustawi wa nchi hizo mbili.

 

Aidha, ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya ziara ya Makamu wa Rias wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa nchini mwezi Januari, 2024 ambapo alikubaliana masuala mbalimbali ya ushirikiano na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na kuelekeza kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.

 

‘’Mkutano huu ni ushahidi tosha wa nia thabiti waliyonayo viongozi wetu na sisi wataalamu katika kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa kuweka mfumo rasmi wa ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya utekelezaji na kujitathmini mara kwa mara’’ alieleza Bi. Mpemba.

 

Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba licha ya kuwa imara kisiasa na kidiplomasia, pia umekuwa ngao muhimu ya kufungua fursa mbalimbali katika sekta muhimu kama vile: afya, elimu, utalii, biashara, uwekezaji na utafiti. Kadhalika ushirikiano huu umerasimishwa kwa Mikataba na Hati za Makubaliano ya Ushirikiano zenye taratibu za kisheria zilizopelekea kupatikana kwa fursa za ufadhili wa masomo, teknolojia mpya, mafunzo ya udaktari na kushirikishana pamoja utaalamu katika maeneo tofauti.

 

Hata hivyo, ameleeza kuwa bado kuna fursa mbalimbali katika ushirikiano wa Tanzania na cuba zinazohitaji kuwekewa mikakati ya kuzikuza na kuziimarisha kwa kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano.

 

Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Kikao cha Wataalam na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Cuba, Balozi Carlos Hernandez ameeleza kuwa na matumaini na kikao hicho kuwa cha mafanikio kwa ustawi wa pande zote mbili na kusisitiza umuhimu wa kufanyika majadiliano ya kina na ya mafanikio katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati.

 

‘’ Kwa kile kidogo tulicho nacho tupo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kujenga uwezo na kutoa ujuzi hususan katika masuala ya teknolojia kwa maendeleo na ustawi wa pande zote mbili’’ alisema Balozi Hernandez.

 

Kikao hiki pamoja na masuala mengine kimejadili kukuza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kati ya Tanzania na Cuba ikiwemo ushirikiano katika sekta ya afya, kilimo na uzalishaji wa chakula, elimu na masuala ya utamaduni na michezo. Aidha, kikao hicho cha watalaamu ni maandalizi ya Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Tanzania na Cuba utakaofanyika tarehe 4 Novemba, 2024 jijini Havana, Cuba.

 

Kikao cha Ngazi ya Wataalamu pia kimehudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humprey Polepole na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.

 

Tanzania na Cuba zilianzisha ushirikiano wa kidiploamsia mwaka 1962 mara baada ya uhuru wa Tanzania na mwaka 1986 zilisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika uchumi, sayansi na ushirikiano katika masuala ya kitaalamu.

Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Naomi Mpemba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, akifungua kikao cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kilichafanyika kwa njia ya mtandao tarehe 30 Oktoba, 2024 katika ngazi ya wataalamu. Pembeni yake ni Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kikao




Wednesday, October 30, 2024

WANANCHI WA BOTSWANA WAPIGA KURA KWA AMANI NA UTULIVU

 

 

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi Mkuu ya SADC (SEOM) Mhe. Mizengo  akiwa na wajumbe wa SEOM wakiangalia moja ya sanduku la kuwekea karatasi za kupigia kura  katika kituo cha Taasisi ya sayansi ya Afya alipotembelea kituo hicho kabla ya zoezi la kupiga kura kuanza jijini Gaborone tarehe 30 Oktoba, 2024


Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi Mkuu ya SADC (SEOM) Mhe. Mizengo  akiwa katika chumba cha kupigia kura akiangalia zoezi hilo lilivyoendelea  katika kituo cha kupigia kura alipotembelea kituo hicho jijini Gaborone tarehe 30 Oktoba, 2024

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi Uchaguzi Mkuu wa Botswana wa SADC( SEOM) Mhe. Mizengo Pinda akiangalia mmoja wa wapiga kura wenye uhitaji maalum akipokea karatasi ya kupigia kura huku asaidiwa na mmoja wa watu waliokuwa katika kituo hicho kutekeleza haki yake katika moja ya kituo cha kupiga kura alipotembelea  kuangalia zoezi linaendaje katika Uchaguzi Mkuu wa Botswana  tarehe 30 Oktoba, 2024

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi Uchaguzi Mkuu wa Botswana wa SADC (SEOM) Mhe. Mizengo Mhe. Pinda akisalimiana na Rais wa zamani wa Botswana Mhe. Festus Mogae alipokutana naye katika kituo cha kupigia kura alipotembelea kituo hicho kuangalia upigaji kura unavyoendeshwa  tarehe 30 Oktoba, 2024

Wananchi wa Botswana wakiwa nje ya kituo cha kupigia kura wakisubiri kuingia ndani ya  kituo hicho kupiga kura zao kuchagua wabunge na wenyeviti wa mabaraza ya serikali za mitaa katika uchaguzi mkuu wa Botswana uliofanyika tarehe 30 Oktoba, 2024

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi uchaguzi Mkuu ya SADC (SEOM) Mhe. Mizengo  akiwa na wajumbe wa SEOM wakiwa nje ya kituo cha kupiga kura baada ya kuangalia zoezi la kupiga kura lilivyokuwa likiendelea

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi Uchaguzi Mkuu wa Botswana wa SADC (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda akiwa na   Rais wa zamani wa Nigeria na  Mkuu wa Misheni ya uangalizi ya Umoja wa Afrika (AU EOM) Mhe. Goodluck Jonathan walipokutana katika moja ya kituo cha kupigia kura jijini Gaborone Botswana tarehe 30 Oktoba, 2024

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi Uchaguzi Mkuu wa Botswana wa SADC (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda katika picha ya pamoja na  

 Rais wa zamani wa Nigeria na  Mkuu wa Misheni ya uangalizi ya Umoja wa Afrika (AU EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa walipokutana katika moja ya kituo cha kupigia kura jijini Gaborone Botswana tarehe 30 Oktoba, 2024

Rais wa zamani wa Nigeria na  Mkuu wa Misheni ya uangalizi ya Umoja wa Afrika (AU EOM) Mhe. Goodluck Jonathan (katikati) akizungumza na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi Uchaguzi Mkuu wa Botswana wa SADC (SEOM) Mhe. Mizengo Pinda (kulia) walipokutana katika moja ya kituo cha kupigia kura jijini Gaborone Botswana tarehe 30 Oktoba, 2024





















Wananchi wa Botswana leo tarehe 30 Oktoba 2024 wamepiga kura kuchagua wabunge watakaounda Bunge la 13 la nchi hiyo na wenyeviti wa Serikali za mitaa ambao wataongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na timu yake wametembelea vituo vitatu vya kupigia kura katika jiji la Gaborone na vituo viwili katika kijiji cha   Mochudi kujionea hali ya upigaji kura inavyoendelea.

Jumla ya Viti 61 vya ubunge na vinagombewa na wagombea kutoka vyama vinne vya siasa vya Botswana Democratic Party (BDP); Umbrella for Democratic Change (UDC); Botswana Congress Party (BCP) na Botswana Patriotic Front (BPF) ambapo Viti 609 vya mabaraza ya Serikali za mitaa vinagombewa na vyama mbalimbali vya siasa na wagombea binafsi ambao wamekidhi vigezo vilivyowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (IEC).

Uchaguzi mkuu wa Botswana umeshuhudiwa na waangalizi wa kimataifa kutoka wa Misheni za Umoja wa Afrika (AUEOM) iliyoongozwa na Rais wa Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Goodluck Jonathan, Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Madola iliyoongozwa na Mhe. Gideon Moi, na Jukwaa la Tume za Uchaguzi kutoka nchi za SADC lililoongozwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania (INEC), Mhe. Jaji Jacob Mwambegele.  

Sambamba na hilo, uchaguzi huo umeshuhudiwa na Ubalozi wa Marekani, Japan, Indonesia, Namibia na waangilizi kutoka katika taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya siasa kutoka nchini humo.

Misheni hizo zimewapongeza wananchi wa Botswana kwa kuendesha shughuli za uchaguzi kwa amani na usalama katika siku ya uchaguzi mkuu ambapo waangalizi hao wameshuhudia idadi kubwa ya wapiga kura ikiwa imejitokeza kupiga kura katika hali ya amani na usalama katika jiji la Gaborone.

Kwa mujibu wa utaratibu wa uchaguzi nchini humo chama kitakachopata zaidi ya viti 31 vya Bunge ndicho kitakachotoa Rais ambaye ataunda Serikali itakayoongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.