Balozi Yahya akiendelea kuzungumza. |
Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mazungumzo kutoka kwa Balozi Yahya |
Mkutano ukiendelea.
Picha na Reginald Philip
|
TAARIFA FUPI KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU AJIRA KWA WATANZANIA KATIKA SHIRIKA LA NDEGE LA EMIRATES KWA MWAKA 2015
- UTANGULIZI
Tarehe 22 Januari, 2015 kuanzia saa tano hadi sita mchana, Wizara ilizungumza na waandishi wa habari ili kuufahamisha umma wa Watanzania kuhusu fursa za ajira katika Shirika la Ndege la Emirates kuanzia mwaka 2015. Katika tukio ambalo lilifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo.
- TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI
Katika kutekeleza moja ya malengo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, hususan kuwatafutia ajira Watanzania nje ya nchi, Wizara kupitia Ubalozi Mdogo wa Tanzania ulioko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umefanikiwa kulishawishi Shirika la Ndege la Emirates kuajiri watanzania wengi zaidi kuanzia mwaka huu 2015.
Shirika hilo la Ndege limekubali kuajiri Watanzania katika kada mbalimbali ambapo maafisa wake wanaosimamia ajira watakuja Tanzania mwezi Machi 2015 kwa ajili ya kuwafanyia usaili Watanzania watakaoomba kazi hizo na kupata uteuzi wa awali.
Shirika la Emirates litaajiri kada mbalimbali kuanzia Maintenance Technicians/Mechanics, Planners-Ground Handling, Metal Workers, Customer Service Professionals na Cabin Crews.
Lengo kuu la kuongea na Waandishi wa Habari ni kuutangazia Umma wa Watanzania kuchangamkia ajira hizo ambazo awali zilitangazwa mwezi Julai 2014, lakini ni Watanzania wachache tu waliomba wakati huo na hivyo kutofikia lengo lililokusudiwa. Baada ya mazunguzo ya kina, Uongozi wa Shirika la Ndege hilo umekubali kuongeza muda wa kuzitangaza ajira hizo kwa mara nyingine, na kupanga kufanya usaili kama ilivyoelezwa hapo awali.
Serikali kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ikishirikiana na Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Ajira inawatangazia Watanzania wote wenye sifa na vigezo vinavyotakiwa wachangamkie fursa hizi za ajira bila kukosa.
Waombaji wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia anuani ya emirates.com/careers. Aidha, waombaji wanashauriwa kuuarifu Ubalozi Mdogo kwa barua pepe (tzconsdb@emirates.net.ae) mara baada ya kuwasilisha maombi yao ili kurahisisha ufuatiliaji. Mwisho wa kuwasilisha maomba ni tarehe 15 Machi, 2015, wakati usaili umepangwa kufanyika tarehe 29 Machi, 2015.
- HITIMISHO
Watanzania wote mnahimizwa kutumia fursa hii adhimu kuomba nafasi hizi kwa wale wenye sifa na vigezo stahiki, na pia kujiandaa vema katika usaili ili Tanzania iweze kufanya vizuri kama wenzetu wengine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, ambao kwa sasa wameajiriwa kwa wingi sana katika soko la Ajira la UAE.
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
JANUARI, 2015