Friday, January 21, 2022
WAZIRI MULAMULA AZISISITIZA BALOZI KUTUMIA FURSA ZINAZOPATIKA KWA MASLAHI YA TAIFA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Liberata Mulamula ameyasema hayo alipozungumza na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania
nchini Uganda tarehe 20 Januari 2022.
Waziri Mulamula alikutana na watumishi wa Ubalozi huo
alipokuwa nchini Uganda kwa ziara ya siku mbili ambapo, pamoja na mambo mengine
alishiriki Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) uliomalizika tarehe
19 Januari 2022.
“Balozi zilizopo mipakani zina fursa nyingi
kiuchumi hivyo, ni muhimu kufanya Vikao vya Ujiraini Mwema na
kuendelea kuhuisha mipango kazi kila inapohitajika kufanya hivyo kwa lengo la
kutatuta changamoto na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano”, alisema Waziri Mulamula.
Pia, akaeleza Wizara inaendelea kuboresha mazingira ya kazi
na kuhakikisha Balozi zote zinakuwa na Rasilimali zinazojitosheleza kuwezesha
majukumu ya kisekta kutekelezwa kwa tija.
Vilevile akahimiza umuhimu wa kuongeza kasi ya kuzitangaza
shughuli zinazofanyika sambamba na fursa mbalimbali zinazopatikana katika nchi hiyo hususani shughuli za kiuchumi ili ziweze kunufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima alieleza kuwa Ubalozi ulifanikisha kikao cha ujirani mwema kilichofanyika kati ya Tanzania na Uganda, mwaka 2017 mjini Bukoba, Kagera.
Pia, kufuatia kupungua kwa masharti ya ugonjwa wa UVIKO- 19,
Ubalozi unaendelea kuratibu shughuli nyingine zenye lengo la kuhakikisha Diplomasia
ya uchumi na Diplomasia ya Umma inatekelezeka kikamilifu.
Kadhalika, Waziri Mulamula alitumia ziara hiyo kutembelea
mali za Ubalozi huo ikiwemo majengo na viwanja, ambapo alipata ufafanuzi juu ya
maboresho yanayotarajiwa kufanyika pamoja na uanzishaji wa miradi mipya katika
maeneo hayo.
Wednesday, January 19, 2022
WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA UGANDA
Mhe. Waziri Mulamula akikabidhi zawadi kwa Mhe. Waziri Odongo |
Picha ya Pamoja Waheshimiwa Mawaziri na Mabalozi wa Tanzania na Uganda. |
MKUTANO WA NNE WA TUME YA KUDUMU YA PAMOJA (JPC) KATI YA TANZANIA NA UGANDA UMEMALIZIKA JIJINI KAMPALA, UGANDA
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Uganda walifungua Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya nchi hizo mbili unaofanyika leo tarehe 19 Januari 2022 jijini Kampala, Uganda.
Mkutano huu wa siku moja
ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 17 Januari 2022
na kufuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 18 Januari 2022.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano
huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) ambaye ameambatana na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi Geodfrey
Kasekenya(Mb.), Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud
Kigahe (Mb.), Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde (Mb.) na Naibu Waziri
Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.).
Mkutano wa Nne umejadili na
kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano
yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi. Maeneo hayo ni pamoja na; Siasa na
Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha
na Uchumi, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Maendeleo na ujenzi wa
Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo
na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu.
Akifungua Mkutano huo Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata
Mulamula ameishukuru Jamhuri ya Uganda kwa mapokezi mazuri ya kidugu na uratibu mzuri wa mkutano huo.
Pia, akaeleza imani aliyonayo
kwa wajumbe wa mkutano huu ambao walijadili na kutoa maamuzi katika maeneo
mbalimbali ya utekelezaji yaliyowasilishwa kwa ustawi wa mataifa haya, sambamba
na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano kupitia majadiliano hayo.
“Serikali zetu zimejikita katika kuhakikisha vikwazo vya biashara
vinatatuliwa na hili linafanyika mara kwa mara katika ngazi zote za utekelezaji
na maamuzi”, alisema Balozi Mulamula
Pia akafafanua kuwa kupitia
ziara za viongozi wetu wakuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mhe. Yoweri Kaguta Museven, Rais wa Jamhuri ya Uganda
changamoto na tozo mbalimbali za kibiashara zilitatuliwa ili kukuza na kuinua
urali wa biashara baina ya Tanzania na Uganda.
Kwa upande wa Waziri wa Mambo
ya Nje wa Uganda, Mhe. Jen. Jeje Odongo alieleza kuwa Mkutano huu utajadili na kufanya makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano zitakazosainiwa katika nyakati tofauti kwa lengo la kufungua maeneo
mapya ya ushirikiano ili kuendelea kuimarisha ushirikiano na kutumia fursa
zilizopo kwa manufaa ya wananchi wa Nchi hizi mbili.
Aidha, akafananua mkutano huu
utajadili hali ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika nchi
hizi mbili pamoja na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaojengwa na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Reli hii ya kisasa (SGR)
itapunguza adha za usafiri kwa Nchi za Afrika Mashariki sambamba na
kuziunganisha nchi za ukanda huo na kupunguza gharama za kibiashara”, alisema
Jen. Odongo.
Kwa pamoja viongozi hao
walizitaka sekta zilizopo katika maeneo hayo ya ushirikiano kuhakikisha
wanatekeleza na kutatua kwa wakati masuala yote ya kitendaji ili kuruhusu sekta
hizo kustawi kiuchumi na kuinua maisha ya Wananchi.
====================================================================
Mhe. Waziri Mulamula pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakifatilia majadiliano ya mkutano huo. |
Mhe. Jen. Odongo, Mawaziri kutoka katika sekta za ushirikiano na ujumbe wa Wataalamu wakifuatilia majadiliano. |
Kutoka kushoto Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Steven Byabato wakifuatilia Mkutano. |
Kutoka kulia Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi Geodfrey Kasekenya na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe wakifuatilia majadiliano. |
Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Mulamula na Jen. Odongo wakionesha Hati za Muhtasari wa Makubaliano walizosaini mara baada ya kukamilisha majadiliano ya mkutano huo. |
Picha ya Pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Mulamula na Jen. Odongo |
Picha ya Pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wengine wa kisekta walioshiriki kwenye majadiliano ya Mkutano huo. |
Tuesday, January 18, 2022
MKUTANO WA NNE WA JPC NGAZI YA MAKATIBU WAKUU UMEFANYIKA JIJINI KAMPALA, UGANDA
Balozi Fatma (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia majadiliano wakati wa Mkutano huo. |
Bw. Kagiire Waiswa pamoja na Mhandisi Irene Okello Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda wakifuatilia Mkutano. |
Makatibu Wakuu na ujumbe wa Uganda wakifuatilia Mkutano. |
Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Uganda ikifuatilia Mkutano. |
WAZIRI MULAMULA ASISITIZA UTEKELEZAJI DIPLOMASIA YA UCHUMI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah na kusisitiza juu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa maslahi ya Taifa
Mazungumzo ya viongozi hao yamelenga kusisitiza utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi baina ya Wizara na Balozi za Tanzania ili kuweza kutumia fursa zilipo katika mataifa mbalimbali kunufaisha Taifa.
Vilevile, Waziri Mulamula amesisitiza uwajibikaji kwa balozi zote za Tanzania ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukuzaji na utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah
Monday, January 17, 2022
MKUTANO WA NNE WA TUME YA KUDUMU YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA UGANDA WAFUNGULIWA JIJINI KAMPALA, UGANDA
Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati
ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya
Wataalamu Jijini Kampala, Uganda.
Mkutano huu wa awali pamoja na mambo mengine utajadili masuala
ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Mkutano huu utafuatiwa na mkutano katika ngazi
ya Makatibu Wakuu utaofanyika tarehe 18 Januari 2022 na utamalizika kwa Mkutano
ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 19 Januari 2022.
Lengo la Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ni kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa tatu uliofanyika mwezi Septemba 2019 jijini Dar es salaam, Tanzania.
Pia, kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika ziara zilizofanywa na Marais wa pande zote mbili katika nyakati tofauti, tangu kumalizika kwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda.
Vilevile, mkutano huu utashuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita itakayohusisha sekta mbalimbali za ushirikiano pamoja na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Kadhalika utajadili ushirikiano katika ujenzi wa miradi ya kimkakati unaofanywa na mataifa hayo hususan ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) unaofanywa na Serikali ya Tanzania ambao unatarajiwa kunufaisha nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tanzania na Uganda zinashirikiana katika sekta za Siasa
na Diplomasia, Mawasiliano, Fedha na Uchumi, Nishati, Maendeleo na ujenzi wa
Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo
na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu.
=====================================================
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima akifafanua utaratibu wa majadiliano ndani ya mkutano huo. |
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania wakifuatilia mkutano. |
Ujumbe kutoka Tanzania. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia mkutano. |
Viongozi wakitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi wa Mkutano huo. |
BALOZI WA TANZANIA NCHINI OMAN AKUTANA NA WAWAKILISHI WA TAASISI ZINAZOTOA MISAADA NCHINI ZILIZOPO OMAN
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah
Abasi Kilima, hivi karibuni amekutana kwa mara ya kwanza na Wawakilishi wa
Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo zinatoa
huduma za kijamii nchini Tanzania.
Katika hotuba ya kuwakaribisha Wawakilishi hao, Mhe. Balozi alisema
Taasisi hizo zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania na
kuwataka waendelee na huduma zao hizo. Vilevile, alizitaka Taasisi hizo kutoa
taarifa za miradi ya kijamii wanayoitekeleza nchini Tanzania ili mchango wao
uweze kutambulika rasmi Serikalini kwani alisema ingawa mchango wao ni mkubwa
kwa taifa lakini Taasisi hizo haziwasilishi rasmi taarifa zao.
Akitaja baadhi ya huduma zinazotolewa na Taasisi
hizo alisema zipo Taasisi zinazochimba visima na hivyo zimekuwa zikisaidia
kampeni ya Serikali ya "Kumtua ndoo mama". Vilevile, zipo Taasisi
zinazotoa huduma za elimu, kusaidia yatima, kujenga nyumba za makazi na nyumba
za ibada. Aliendelea kusema kuwa,
kwa kuwa viongozi wa Taasisi hizo wana asili ya Tanzania na bado wana
mafungamano makubwa na nchi yao ya asili, Serikali inawatambua kama Diaspora na
hivyo uwasilishaji wa taarifa za huduma wanazozitoa utasaidia lengo la Serikali
la kuwapa hadhi maalum.
Mhe. Balozi Kilima alizitaka Jumuiya hizo kuwa
kitu kimoja na kukutana mara moja au mbili kila mwaka kujadili masuala yao.
Miongoni mwa Taasisi alizokutana nazo ni pamoja
na Alwadood International, Istiqama
International, Attaqwa,
Tuelekezane Peponi, Sundus, Coco
Charity na Alfirdaus.
Pia alitumia fursa hiyo kuzipa tuzo maalum
Taasisi mbili zilizofanya vizuri nchini Tanzania. Taasisi hizo ni Tuelekezane
Peponi na Attaqwa. Taasisi nyengine zilizofanya vizuri zilipewa Tuzo wakati wa
Sherehe za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Katika mkutano huo, Wawakilishi wa Taasisi hizo
walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo
ushuru kwa bidhaa na vifaa wanavyoleta nchini kwa ajili ya Misaada na kuiomba
Serikali iwaondolee ushuru kwa bidhaa hizo. Kadhalika, walieleza
changamoto nyengine ya kuchelewa kupata usajili
kwa baadhi ya Taasisi, upatikanaji wa vibali na tozo za viza. Pia, wameomba
Serikali iwapatie utambulisho maalum ili waweze kuingia nchini mara kwa mara
kutekeleza miradi ya Kijamii.
Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo, Mhe. Balozi
Kilima alisema ni vyema Taasisi hizo ziwasiliane na Ubalozini pale zinapohitaji
kupeleka misaada ya kijamii ili Ubalozi uweze kuwatambulisha rasmi katika
Mamlaka za Serikalini. Aidha, kuhusu viza aliwashauri kuomba viza ya kuingia mara kwa mara (Multiple entry visa)
au viza ya kutembelea jamaa (family visit visa).
Pamoja na majibu hayo, alisema Serikali inaendelea na mchakato wa
kuandaa mpango maalum wa kuwatambua Diaspora na kuwapatia hadhi maalum
itakayowarahisishia utekelezaji wa shughuli zao za kijamii nchini.
Taasisi hizo kwa pamoja zimechimba visima virefu 200, visima vifupi
5000, zimejenga nyumba za yatima 17, Madrasa 62, na Misikiti 47. Aidha, Taasisi
ya Alwadood inakusudia kuleta nchini mtambo wa kuchimbia visima virefu wenye
thamani ya USD 170,000.
|
Saturday, January 15, 2022
BALOZI HEMEDI MGAZA AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI KUWAIT
Balozi Mgaza akimkaribisha Mhe. Said Shaibu Mussa katika ofisi za Wizara jijini Dodoma. |
Friday, January 14, 2022
WAZIRI MULAMULA AWAHIMIZA MABALOZI KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata
Mulamula (Mb.) amewasisitiza mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nje ya nchi
kuweka mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu ya kidiplomasia wenye maslahi
mapana kwa uchumi wa Taifa.
Mhe.
Mulamula ameyasema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini
Kuwait, Mhe. Said Shaibu Mussa aliyekuja kumuaga ofisisni kwake leo tarehe 14
Januari 2022 katika ofisi za Wizara, jijini Dodoma.
Mazungumzo
baina ya wawili hao yalijikita katika kuangalia namna bora ya kuboresha utendaji
wa ofisi za balozi za Tanzania sambamba na Wizara ili kuweza kutumia fursa
zilipo kunufaisha Taifa.
“Nasisistiza
balozi zetu kutekeleza majukumu kwa kuhakikisha fursa za kiuchumi zinawekewa
msisistizo sambamba na mafanikio yanayopatikana yanatangazwa kikamilifu ili
kuweza kuuhabarisha uuma namna ya kuzitumia fursa zinazopatikana”. Alisema Mhe.
Waziri
Pia
ameeleza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kufikia malengo tarajiwa
katika sekta ambazo serikali ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na
mataifa wanayowakilisha.
Naye
Balozi Said Shaibu Mussa amemshukuru Mhe. Waziri kwa maelekezo ya kiteundaji
aliyoyapata sambamba na kuahidi kufanya kazi kwa ubunifu katika majukumu hayo
mapya ili kuongeza maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Kutwait.
Tanzania
na Kuwaita zimekuwa zikishirikiana katika sekta za kilimo, afya, ujenzi wa miundombinu
ya barabara na maji.
====================================
Mazungumzo yakiendelea. Kulia ni Msaidizi wa Waziri, Bw. Seif Kamtunda akifatilia mazungumzo. |
Mhe. Waziri Mulamula akimkabidhi vitendea kazi Mhe. Said Mussa. |
WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA MALAWI NCHINI
TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA MISRI KATIKA KUBORESHA SEKTA YA AFYA
Serikali ya Tanzania imepokea tani 16 za Dawa, Vifaa Tiba na Vifaa Kinga
ikiwa ni msaada wenye thamani ya shillingi milioni 864 kutoka Serikali ya Misri.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali wakati wa hafla fupi ya kupokea shehena
ya dawa hizo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi
amesema Tanzania inaishukuru Serikali ya Misri kwa msaada huo muhimu kwa
wananchi wa Tanzania na kwamba itandelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya
Misri hususan katika kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuusimamia kikamilifu msaada huo ili uwafikie walengwa kwa wakati.
Pia aliongeza kusema kuwa, msaada
huo umewasili wakati mwafaka ambao Tanzania inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa
kusogeza huduma za afya kwa wananchi pamoja na kuongeza upatikanaji wa Dawa na
Vifaa Tiba katika maeneo ya mijini na vijijini.
Aidha, alipongeza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo
kati ya Tanzania na Misri ambao umekuwa wa manufaa makubwa tangu kuanzishwa
kwake na kupongeza jitihada zinazofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya nchini ambapo
alisema msaada huo ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Mhe. Rais aliyoifanya
nchini Misri mwezi Novemba, 2021.
"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na pia kwa
niaba ya Waziri wa Afya. Mhe. Ummy Mwalimu napokea msaada huu wa Dawa na Vifaa
Tiba wenye thamani zaidi ya shilingi milioni 800 kutoka Serikali ya Misri. Kama
Serikali, tunaendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi hivyo
msaada huu utachangia jitihada hizo. Ninakuomba Mhe. Balozi ufikishe salamu
zetu za shukrani kwa Mhe. Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Misri kwa msaada huu
ambao tumeupokea kwa dhati na utatimiza lengo lilokusudiwa la kuwasaidia wananchi
wa Tanzania" alisema Dkt. Makubi.
Kwa upande wake, Balozi wa Misri hapa nchini. Mhe.
Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na
Tanzania na inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi makini wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania za kuwaletea watanzania maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Kadhalika, Mhe. Balozi Abulwafa alieleza kuwa,
mbali na ushirikiano wa Tanzania na Misri kwenye sekta ya afya, Nchi yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kutoa fursa za mafunzo ya kuwajengea uwezo watu
wa sekta ya afya na fani mbalimbali kwa watanzania.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichwale, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi, Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Celestine Kakele na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Balozi wa Misri hapa nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa (katikati) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi (wa pili kulia) msaada wa Dawa na Vifaa Tiba kutoka Serikali ya Misri. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe ( wa pili kushoto), Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichalwe (wa kwanza kushoto) na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Misri, Brigedia Sherif Farag Mohamed (wa kwanza kulia). Hafla ya makabidhiano ya msaada huo imefanyika jijini dar es Salaam hivi karibuni.
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi kwa pamoja na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa wakisaini Hati ya Makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba vilivyopokelewa nchini kutoka Misri
Afisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Faith Masaka akibadilishana mawazo na Afisa kutoka Ubalozi wa Misri hapa nchini, Bw. Mahmoud Hamdy Khalifa wakati wa hafla ya makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba kutoka Misri |