Rais wa Jamhuri ya Indonesia Mheshimiwa Joko Widodo anatarajia kuanza ziara ya Kitaifa ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia tarehe 21 hadi 22 Agosti 2023
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amesema ziara hiyo ni matokeo ya kazi kubwa anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine.
“Ziara ya Mheshimiwa Widodo itakuwa ni ziara ya pili kwa kiongozi wa taifa hilo kutembelea nchini. Ziara ya kwanza ilifanywa na Mheshimiwa Soeharto, Rais wa Pili wa Indonesia mwaka 1991, ikiwa ni miaka 32 iliyopita,” alisema Dkt. Tax.
“Mheshimiwa Rais Widodo atawasili Leo tarehe 21 Agosti 2023 na atapokelewa rasmi na Mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 22 Agosti, 2023, Ikulu Jijini Dar es Salaam,” aliongeza Waziri Tax.
Waziri Tax ameongeza kuwa, baada ya mapokezi viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na baadaye mazungumzo rasmi na kufuatiwa na hafla ya utiaji saini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano kwenye sekta mbalimbali.
“Tanzania na Indonesia zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria. Uhusiano huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Indonesia Mheshimiwa Soekarno. Uhusiano wa kidiplomasia ulianza mwaka 1964, ambapo mwaka huohuo Indonesia ilifungua Ubalozi wake nchini na kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua Ubalozi wake nchini miaka michache baada ya uhuru. Aidha, Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini Indonesia Agosti, 2022, na kuzinduliwa rasmi mwezi Juni 2023,” aliongeza Dkt. Tax
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax amesema kuwa Tanzania na Indonesia zimekuwa zikishirikiana katika sekta za Uwekezaji ambapo hadi kufikia mwaka 2023, Indonesia imewekeza nchini miradi ipatayo mitano (5) katika sekta za Kilimo, uzalishaji wa viwandani, ujenzi.
Sekta nyingine za ushirikiano ni pamoja na kilimo ambapo mwaka 1996 Indonesia ilianzisha Kituo cha Mafunzo ya Kilimo kwa Wakulima Vijijini (Farmers’ Agriculture and Rural Training Centre-FARTC), kilichopo Mikindo mkoani Morogoro. Kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kwa wakulima.
“Ziara hii inatarajiwa kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kama itakavyoonekana katika Hati za Makubaliano zitakazosainiwa, na matokeo ya mazungumzo kati ya Viongozi wetu yatakayojikita katika diplomasia, biashara, kilimo, uvuvi, elimu, nishati, madini, uchumi wa buluu na uhamiaji,” alisema Dkt. Tax.