Thursday, August 17, 2023

BALOZI WA TANZANIA NCHINI UMOJA WA FALME ZA KIARABU(UAE) AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Lt. Jen. (Mst) Yacoub Hassan Mohamed akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan katika Ikulu ya nchi hiyo (Qasr Al Watan) iliyopo mjini Abu Dhabi.


==============================================

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Lt. Jen. (Mst) Yacoub Hassan Mohamed mapema wiki hii amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan katika Ikulu ya nchi hiyo (Qasr Al Watan) iliyopo mjini Abu Dhabi.

Viongozi hao pia walipata wasaa wa mazungumzo ambapo Mheshimiwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu alimhakikishia Mhe. Mohamed ushirikiano wa Serikali yake katika kutekeleza majukumu yake nchini UAE kwa manufaa ya pande zote mbili hususan kiuchumi.

Kwa upande wa Balozi Mohamed alimuahidi Mheshimiwa Rais kuwa atahakikisha Watanzania na Waemirati wananufaika na fursa za uchumi zilizopo pande zote mbili.

Tanzania na UAE zina fursa nyingi za kushirikiana kiuchumi hususan katika sekta za nishati ambayo UAE ni miongoni mwa nchi tajiri katika uzalishaji wa mafuta. Kadhalika Tanzania ina eneo kubwa la kilimo hivyo ina soko kubwa la bidhaa za Kilimo na Mifugo ambapo ushirikiano huo utawezesha uzalishaji wa kisasa na kuongeza thamani ya bidhaa.

Bidhaa zenye soko kubwa kwa Tanzania nchini UAE ni pamoja na mbogamboga, matunda, nyama, korosho, karafuu, chai, karanga, asali, samaki na kahawa. Hivyo Ubalozi unaendelea na jitihada za kuwashawishi wawekezaji wa UAE kuja kushirikiana na Watanzania kuwekeza kwenye sekta ambazo zitatoa ajira kwa Watanzania wengi na zenye soko kubwa UAE kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu ubalozi huo pia unawakilisha nchi za Bahrain, Pakistan na Iran. 

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Lt. Jen. (Mst) Yacoub Hassan Mohamed akiteta na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan katika Ikulu ya nchi hiyo (Qasr Al Watan) iliyopo mjini Abu Dhabi.

Picha ya pamoja.

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.