Tuesday, August 29, 2023

TANZANIA INATHAMINI MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inathamini mchango wa Asasi za Kiraia katika kutekeleza mipango na sera mbalimbali za maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Dkt. Shelukindo amesema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Asasi za Kiraia ambazo hushiriki kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza  shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali. Hivyo, ni vyema kuwa na asasi za kiraia zenye ubora ambazo zitaleta mchango chanya katika maendeleo.

“Serikali imekuwa ikipanga Mipango na Sera za maendeleo ambayo utekelezaji wake hufanywa na wadau mbalimbali ikiwemo Asasi za Kiraia. 

Hivyo, utekelezaji wa sera na mipango hiyo inahitaji asasi za kiraia zenye ubora,” alisema Balozi Shelukindo

“Nimeona mada mbalimbali katika Warsha ya leo ambazo zinazungumzia masuala mengi, ikiwemo misingi ya kidemokrasia, haki za binadamu, utawala bora na vitu vya msingi katika kukuza uchumi wa nchi yetu ambapo vitu vyote vinakwenda sambamba,” aliongeza Dkt. Shelukindo.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo amesema Warsha hiyo ni muhimu ambapo mwaka 2002, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliibadilishwa na kugeuzwa kuwa Umoja wa Afrika. Lengo la hayo ilikuwa ni kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kufikia azma hiyo, mwaka 2004, Umoja wa Afrika ulipitisha Mkataba wa kuanzisha Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni (ECOSOCC).

“Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni linatoa fursa kwa asasi za kiraia zilizopo Barani Afrika kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika kwa kutoa ushauri kwenye Vyombo vya Kisera vya Umoja wa Afrika na kuwaelimisha pia wananchi kuhusu mipango na mikakati mbalimbali ya Umoja wa Afrika ili kurahisha utekelezaji wake,” alisema Balozi Shiyo.

Balozi Shiyo aliongeza kuwa utendaji kazi wa Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni la Umoja wa Afrika hufanyika katika ngazi ya Kanda, ambapo kila nchi inawakilishwa kwenye Kamati Tendaji (Permanent General Assembly). Sambamba na hilo, kila nchi ina jukumu la kuanzisha Jukwaa la Kitaifa (ECOSOCC National Chapters) ili kuhamasisha asasi nyingi zaidi za kiraia kushiriki kwenye masuala ya Umoja wa Afrika.

“Lengo la warsha ni kuhamasisha na kuongeza uelewa na kuzijengea uwezo wa Asasi za Kiraia za Tanzania kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Pamoja na Mambo mengine, Warsha hii itasaidia kuongeza ushiriki na uelewa wa Asasi za Kiraia na Watanzania kwa ujumla kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Umoja wa Afrika,” aliongeza Balozi Shiyo. 

Naye Mkuu wa Mkuu wa Sekretarieti ya ECOSOCC, Bw. William Carew amesema kuwa ECOSOCC itasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia nchini Tanzania. Hivyo kutoa fursa ya jukwaa la ushirikishwaji katika kutafuta Afrika bora.

“lengo letu kama ECOSOCC ni kusaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla,” alisema Br. Carew.  

Tanzania ni miongoni mwa nchi ya tano za awali kuanzisha majukwaa ya kitaifa ya Ecosocc ili kuwa karibu na asasi za kiraia kwa lengo la kuhamasisha maendeleo nchini pamoja na kufikia malengo ya Ajenda ya 2063 inayohusu masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya na demokrasia. Mbali na Tanzania, nchi nyingine ni Mauritius, Sierra Leone, Zambia na Misri.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Mkuu wa Mkuu wa Sekretarieti ya ECOSOCC, Bw. William Carew akieleza jambo wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Washiriki wakifuatilia Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo katika picha ya pamoja Washiriki wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.