Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, viwanda, kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi pamoja na uchumi wa buluu.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa hafla ya utiaji Saini wa Hati mbalimbali za makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Indonesia iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Indonesia Mheshimiwa Joko Widodo.
Hati za makubaliano (MoUs) zilizosainiwa ni saba ambazo ni uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC), msamaha wa visa kwa wamiliki wa hati za kusafiria za Kidiplomasia, Huduma za Afya, nishati, mafuta na gesi mapoja na madini.
Mara baada ya kusainiwa kwa Hati hizo za makubaliano, Marais wote wawili waliongea na vyombo vya Habari ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia alisema kuwa chimbuko la uhusiano kati ya Tanzania na Indonesia ni Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955 ambapo nchi nyingi za Afrika na Asia zilikuwa katika utawala wa kikoloni kwa kipindi hicho.
“Tanzania na Indonesia zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria. Uhusiano huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Indonesia Mheshimiwa Soekarno. Uhusiano wa kidiplomasia ulianza mwaka 1964, ambapo Indonesia ilifungua Ubalozi wake nchini mwaka 1964 na kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua Ubalozi wake nchini miaka michache baada ya uhuru,” alisema Rais Samia.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa Tanzania na Indonesia zimekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi ili kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, viwanda, kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi, uvuvi na utalii pamoja na uchumi wa buluu.
Kadhalika, Mhe. Rais Samia amesema majadiliano baina yake na mgeni wake pamoja na mambo mengine, wamebainisha nia ya Tanzania kupata uzoefu wa uzalishaji mafuta ya mawese kutoka kwa Indonesia ambapo imekuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya mawese duniani.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo amesema kuwa Indonesia itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo unazidi kuimarika zaidi.
“Indonesia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali hususan sekta ya afya ambapo tumekusudia kuanzisha kiwanda cha dawa na vifaa tiba nchini Tanzania kwa maslahi ya pande zote,” alisema Mhe. Widodo
Rais Widodo ameongeza kuwa Indonesia imekubaliana na Tanzania katika kuboresha kilimo na kukifanya kuwa cha kisasa na chenye tija. “Indonesia itaendelea kuboresha Kituo cha Mafunzo ya Kilimo kwa Wakulima Vijijini (FARTC) kilichopo Mkindo – Morogoro na kuwawezesha wakulima wengi nchini Tanzania kulima kisasa zaidi,” aliongeza Rais Widodo.
Rais Widodo aliwasili nchini tarehe 21 Agosti 2023 kwa ziara ya Kitaifa ya siku mbili na amehitimisha ziara yake leo tarehe 22 Agosti 2023 na kureje Indonesia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam |
Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Joko Widodo akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.