Thursday, March 24, 2016

Tanzania na Saudia zasaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya uchumi na uwekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mhe. Adel Al Jubair alipowasili nchini kwa ziara ya siku moja. Wakati wa ziara hiyo Mhe. Al Jubair alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kusaini Mkataba wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Vijana na Michezo. Waziri Al Jubair pia alimfikishia Rais Magufuli salamu kutoka kwa Mfalme Salman wa Saudi Arabia.  
Rais Magufuli akizungumza na Waziri Adel Al Jubair (kushoto)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wajumbe wa Serikali zote mbili wakishuhudia uwekwaji saini wa mkataba kuhusu Ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Ufundi, Vijana na Michezo. Kwa upande wa Tanzania mkataba ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (kulia) na Serikali ya Saudi Arabia iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Adel Al Jubair.
Waziri Mahiga na Waziri Al Jubair wakibadilishana mkataba mara baada ya kusainiwa
Mhe. Rais Magufuli akiagana na Waziri Al Jubair
Waziri Al Jubair akiagana na Waziri Mahiga mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli na zoezi la uwekaji saini kukamilika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mhe. Al Jubair, Waziri Mahiga, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Abdallah Kilima (wa kwanza kulia) na ujumbe uliombatana na Waziri Al Jubair. 

Picha na Reginald Philip 


Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje yaitaka Wizara kusimamia Sera ya Diplomasia ya Uchumi

 Sehemu ya Waheshimiwa Wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia mazungumzo.
Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Wabunge.

 Sehemu ya Wakurugenzi na  Maafisa wa Wizara wakifuatilia kikao.
 Sehemu nyingine ya Wakurugenzi na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia kikao


Wednesday, March 23, 2016

Waziri Mahiga azungumza na Kundi la Mabalozi wa Afrika waliopo nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Kundi la Mabalozi wa Afrika waliopo nchini walipomwalika kwa ajili ya kuzungumza nae juu ya namna ya kuimarisha mahusiano kati ya nchi zao na Tanzania. Mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Yasser Elshawaf wakati wa mkutano kati ya Waziri Mahga na Kundi la Mabalozi wa Afrika waliopo nchini
Mhe. Dkt. Mahiga alizungumza na Kiongozi wa Mabalozi hao ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe nchini, Mhe. Edzai Chimonyo
Waziri Mahiga akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini Mhe. Chirau Ali Mwakwere wakati wa mkutano wake na Kundi la Mabalozi wa Afrika. Kulia ni Balozi wa DRC, Mhe.Jean Pierre Tshampanga Mutamba.
Waziri Mahiga akisalimiana na Balozi wa Rwanda nchini Mhe. Eugene Kayihura wakati wa mkutano wake na Kundi la Mabalozi wa Afrika.
Waziri Mahiga akisalimiana na Kaimu Balozi wa Burundi nchini, Bw. Prefere Ndayishimiye
Dkt. Mahiga akisalimiana na Mwakilishi wa Ubalozi wa Angola nchini, Bw. Joel Cumbo

Tuesday, March 22, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje afanya ziara Chuo cha Diplomasia

Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe.  Dkt. Susan Kolimba (Mb.) , akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha Diplomasia wakati wa ziara yake Chuoni hapo. Chuo hicho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Balozi  Dkt. Mohammed Maundi (katikati) na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Taaluma Chuoni  hapo, Dkt. Wetengere Kitojo

Naibu Waziri akiangalia vitabu vilivyopo kwenye Maktaba ya Chuo hicho

Naibu Waziri akiwaeleza jambo uongozi wa chuo hicho.
Naibu Waziri akikagua Darasa la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Chuo cha Diplomasia
Dkt. Suzana Kolimba akizungumza na uongozi wa Chuo cha Diplomasia mara baada ya kumaliza kuzungukia eneo la Chuo cha Diplomasia
Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia naye akizungumza wakati Naibu Waziri alipotembelea Chuo hicho
Naye Mkurugenzi wa Taaluma, Dkt. Watengere Kitojo akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri
Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu Chuoni hapo Dkt. Charles Bekon akionesha  Mpango Mkakati wa Chuo cha Diplomasia ikiwemo mfano wa  michoro ya majengo ya Chuo.
 Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba akitazama sampuli ya michoro ya majengo yanayotarajiwa kujengwa Chuoni hapo
Dkt. Susan akisalimiana na Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia mara baada ya kuwasili Chuoni hapo.
Naibu Wizara Dkt. Suzan Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Chuo cha Diplomasia, wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia Dkt. Mohammed Maundi, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Dkt. Achiula (wa pili kutoka kulia), Mkurugenzi wa Taaluma wa Chuo cha Diplomasia Dkt. Watengere Kitojo (wa kwanza kulia) na Mhasibu Mkuu Dkt. Charles Bekon. 


Picha na Reginald Philip

=========================================================================================================


Naibu Waziri Dkt. Kolimba aeleza nia ya Wizara katika kuendeleza Chuo cha Diplomasia 

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa imejipanga kuhakikisha Chuo cha Diplomasia kinaboresha huduma zake za utoaji elimu na mafunzo ya masuala ya Diplomasia ili kukidhi mahitaji ya Watanzania katika taaluma hiyo.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Mhe. Kolimba alisema kwamba Chuo cha Diplomasia ambacho kilianzishwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji ni miongoni mwa vyuo vilivyojipatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi kwa kutoa  mafunzo katika masuala ya Diplomasia na hivyo Wizara haina budi kuhakikisha inaendelea kukiboresha ili kuhakikisha kinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Mhe. Dkt. Susan alisema kuwa, miongoni mwa masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika maboresho hayo ni pamoja na miundombinu ya Chuo kwa maana ya kuongeza majengo, vifaa vya kisasa vya kufundishia, maabara za kisasa za lugha, maktaba na kuongeza Wakufunzi.

Aidha, Mhe. Kolimba aliueleza Uongozi wa Chuo hicho kuwa ni vema vipaumbele katika kukiletea chuo maendeleo vikaainishwa ikiwa ni pamoja na kuonyesha mikakati ya kila changamoto ili kupata suluhisho la haraka la changamoto hizo.

“Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya na tunaahidi kuwa pamoja nanyi wakati wote ili kuhakikisha Chuo chetu kinafikia viwango vinavyostahili” alisema Mhe. Kolimba.

Vilevile alieleza kuwa ni vema Chuo kikaimarisha ushirikiano na Vyuo vingine vya ndani na nje kwa kuainisha maeneo muhimu ya ushirikiano yenye faida kwa pande zote. Pia alikitaka Chuo kuwa na mikakati itakayokiwezesha Chuo hicho kuweza kujiendesha kibiashara  kama vyuo vingine nchini na kuacha utegemezi mkubwa katika bajeti ya Serikali.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Chuoni hapo, Mkurugenzi wa Chuo hicho, Balozi Mohammed Maundi alisema kuwa Chuo hicho kinaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ya Chuo hicho ikiwemo kuanzishwa kwa Kozi ya Shahada mwaka 2015 na tayari chuo kimepata michoro ya majengo kwa Chuo kipya wanachotarajia kukijenga na sasa kinachohitajika ni fedha ili kukamilisha mpango huo ambao kwa kiasi kikubwa utamaliza changamoto zinazokikabili Chuo.

Chuo cha Diplomasia (CFR) ni chuo kilichoanzishwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji mwaka 1978. Chuo kimekuwa kikitoa elimu katika ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada na Shahada ya Juu. 

-Mwisho-

JK aendelea kusuluhisha Mgogoro wa Libya.

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya amewasili jijini Tunis nchini Tunisia  kushiriki Mkutano wa nane wa nchi Jirani ya Libya. Mkutano huo ulioitishwa na Serikali ya Tunisia ni muendelezo wa jitihada za nchi jirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya. Rais Mstaafu amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman aliposhiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa jijini Tunis, Rais Mstaafu Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, Arab na Afrika wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh aliyemtembelea hotelini kwake. Katika mazungumzo yao, Waziri Messaleh alimpongeza  Rais Mstaafu Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa Libya ambapo alimuelezea hali ya usalama na kisisa ya  Libya na mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo.Mheshimiwa Abdelkader Messaleh Alimhakikishia Rais Mstaafu ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete alimshukuru Waziri Abdelkader Messaleh kwa maelezo aliyompatia na ushirikiano aliomuahidi na kumuelezea matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo madhali nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau wote kuhakikisha mgogoro huo unatatulika ambapo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa hatimaye suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya uko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.


 Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje ya Oman Mheshimiwa Yusuf bin Alawi bin Abdallah mjini Salalah, Oman kuzungumzia mgogoro wa Libya. Katika mkutano wao wamebadilishana mawazo juu ya suluhisho la kudumu la hali ya siasa, usalama na amani nchini Libya.


 Katika Mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona kuwa mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu. Amewakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya ya hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao. Amewakumbusha dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kupawapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto za Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote. 


 Picha ya pamoja.

===================== 
Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa nchi Jirani na Libya, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya (Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj,  wadau wengine wa Libya  pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya iliyoko jijini Tunis. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016. 

Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika utatuzi wa mgogoro wa Libya ameshiriki Mkutano wa Kamati ya Uandishi ya Baraza Maalum la Uandishi wa Katiba ya Libya (Constitution Drafting Assembly) unaoendelea mjini Salalah, Oman. Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yusuf bin Alawi bin Abdallah na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler.

Katika Mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona kuwa mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu na Amewakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya ya hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao ikiwa ni pamoja na dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kuwapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto za Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote. 

Rais Mstaafu Kikwete pia amepongeza jitihada za Umoja wa Mataifa chini ya Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler za kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya kupitia Mkataba wa Amani wa Libya (Libya Political Agreement) uliotiwa saini tarehe 17 Desemba, 2015 huko Shkirat, Morocco na kuwahimiza wadau wa pande zote za siasa nchini Libya kutekeleza makubaliano hayo ikiwemo kuundwa kwa serikali na kusimikwa kwa serikali hiyo yalipo makao makuu ya nchi hiyo mjini Tripoli mapema iwezekanavyo.

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Afrika amewahakikishia wajumbe hao utayari wa Umoja wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Falme za Kiarabu (Arab League)  na wadau wengine wote kusaidia jitihada za wananchi wa Libya kurejesha hali ya usalama, amani na utulivu nchini Libya.
                                     MWISHO.

Friday, March 18, 2016

Mkurugenzi wa Idara ya Asia azungumza na Balozi wa India nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki akizungumza na Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya alipofika Wizarani kwa ajili ya kueleza dhamira ya India ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Elimu na ile ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar.
Balozi Arya akichangia jambo wakati wa mazubngumzo yake na Balozi Kairuki
Balozi Kairuki akiagana na Balozi Arya mara baada ya mazungumzo yao.

Thursday, March 17, 2016

Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wafanya Ziara Kilosa

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. John Henjewele akitoa taarifa ya Wilaya na historia ya migogoro kwa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini ambao walitembelea jamii ya wafugaji na wakulima Wilayani humo kwa lengo la kuwashawishi kuwa wavumilivu kwa kila mmoja katika kutatua migogoro ya Ardhi na kuimaliza kabisa, sambamba na kutoa vifaa kwa watoto wa shule katika shule ya Sekondari Parakuyo na shule za msingi Mabwerebwere, Tindiga na Ulaya. Kauli mbiu ya Ziara hiyo ilikuwa "Tusipigane Tuzungumze Wakulima na Wafugaji Tushirikiane kudumisha Amani

Sehemu ya Maafisa walioshiriki Ziara wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Mhe. Henjewele. 

Maafisa Habari kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wakikabidhi fulana kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Parakuyo Wilayani Kilosa, kutoka kushoto Bi. Rose Mbilinyi, kutoka kulia Bw. Ally Kondo na Bw. Teodos Komba. Vilevile maafisa hao walikabidhi msaada wa Vitabu, Zana za Kufundishia na Madawati.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Tindiga Wilayani Kilosa wakiwa wamekaa katika Madawati waliyokabidhiwa na Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini, ambapo shule hiyo ilipokea msaada wa Madawati 50.


========================================================================


Ziara hiyo ni miongoni mwa shughuli zilizofanyika wakati Kikao Kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kikiendelea, Kikao hicho kilifunguliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye tarehe 14 Machi na kinatarajiwa kumalizika tarehe 18 Machi,2016.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akifungua Kikao kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini nchini hawapo pichani kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel ambapo alieleza lengo la kikao hicho ni kupeana na kushirikishana uzoefu ili kuboresha utendaji na kuleta ufanisi kwa maafisa hao, Pia aliwasisitiza ni vema kila Afisa akaonesha uwezo binafsi ili kuweza kukubalika na kuthaminiwa kwa nafasi yake katika Tasisi anayoiwakilisha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bi. Mindi Kasiga kati akiwa na baadhi ya Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wakifuatilia kikao.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es salaam Bw. Luke Chilambo ambaye alikuwa miongoni mwa wawezeshaji katika kikao kazi hicho akitoa mada kuhusiana na Diplomasia na Itifaki.
Bi Joy Nyabongo ambaye ni muwezeshaji na mtoa mada ya Huduma kwa Mteja akitoa Zawadi kwa mshindi wa pili Bi. Mindi Kasiga baada ya kushinda jaribio la uelewa wa mada hiyo.
Mhe. Waziri Nape na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa Habari na Mawasiliano kutoka Serikali kuu.