Wednesday, October 12, 2016

Waheshimiwa Mabalozi watembelea Chuo Kikuu cha Afya kilichopo Mloganzila.



Balozi wa Tanzani Moscow Mhe. Luteni Generali Wynjones Mathew Kisamba (wa kwanza kushoto) akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea walipotembelea Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili kilichopo Mloganzila, Jijini Dar es Salaam. Waheshimiwa Mabalozi walipata fursa ya  kuona miradi inayoendelea Chuoni hapo, sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya vifaa vya kisasa vya matibabu. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Balozi Mbelwa Kairuki 
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe.Radhia Msuya akizungumza wakati wa ziara yao katika Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili kilichopo Mloganzila, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Ephata Kaaya
Makamu Mkuu wa Chuo  Kikuu cha Afya Muhimbili cha Mloganzila Jijini Dar es Salaam Profesa Ephata Kaaya (katika) akiwakaribisha Waheshimiwa Mabalozi walipotembelea chuo hicho
Picha ya pamoja mbele ya Jengo la Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili kilichopo Mloganzila Jijini Dar es Salaam



Mabalozi waahidi neema MUHAS

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzanikatika nchi mbalimbali duniani wameahidi kuzishirikisha Serikali na Sekta binafsi kwenye nchi walizopo kuja kuwekeza na kuchangia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ikiwemile ya Chuo Kikuu  cha Afya na Sayansi Kishiriki cha Muhimbili (MUHAS) hususan kwenye maendeleo ya teknolojia, miundombinu na kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya.

Mabalozi hao walitoa ahadi hiyo walipotembelea na kuonana na Uongozi wa juu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Mhumbili kilichojengwa katika  eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji Dar es Salaam.
          Taswira ya Jengo la Chuo Kikuu Shirikishi cha Afya na Sayansi Muhimbili
kilichojengwa eneo la Mloganzila Jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na Uongozi wa Chuo hicho na wadau waliojitokeza kwenye ziara hiyo, kwa niaba ya  Mabalozi wengine Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Radhia Msuya alitoa pongezi kwa Serikali na Uongozi wa Chuo hicho kwa hatua madhubuti zinaoendelea kufanyika ili kuboresha mazingira ya tiba nchini sambamba na mazingira ya kufundishia wataalam wa kutoa huduma za afya.

Kwa upande wake, Makamu   Mkuu wa Chuo hicho Profesa Ephata Kaaya alisema kuwa Hospitali hiyo iliyojengwa kwa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Kimarekani 49,500,000 kutoka Serikali ya Korea Kusini ni ya kisasa na itatoa huduma za kiafya za hali ya juu. 

Pia aliongeza kusema kuwa  Mafunzo bora kwa wanafunzi wa fani za afya, uchunguzi wa magonjwa na tafiti zenye ubora katika fani za afya hapa nchini yatatolewa chuoni hapo na kwamba kukamilika kwa chuo hicho kutapunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.

"Waheshimiwa Mabalozi, njambo la faraja kuwa Hospitali hii itakapoanza kufanyakazi itapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa na gharama zinazotumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu" alisema Prof. Kaaya.

Katika hatua nyingine, Prof. Kaaya aliwaomba Mabalozi waliotembelea Chuo hicho kusaidia katika upatikanaji wa wataalam waliobobea kwenye masuala ya afya kutoka nchi za nje kutokana na upungufu wa wataalam hao nchini, ili waweze kushirikiana nao katika kutoa huduma bora za afya pamoja na kufundisha wataalam wetu.



Aidha alieleza kuwepo kwa mpango wa kuanza kwa mradi wa ujenzi wa Kituo Kilichobobea katika masuala ya Utafiti, mafunzo na Tiba ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu katika Ukanda wa Afrika Mashariki kitakachojengwa katika eneo hilo la Chuo la MloganzilaUjenzi wa kituo hicho utaanza mwezi Mei 2017. Ilielezwa kuwa kupitia Mradi huu jumla ya wataalamu 24 wa kada  mbalimbali za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu watapewa mafunzo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi. 

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wapo nchini kufuatia kikao kati yao na Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika tarehe 07 Oktoba, 2016.

Tuesday, October 11, 2016

Waziri Mahiga aongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi ya SADC nchini DRC

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (wa sita kushoto) akiongoza kikao cha pamoja cha Mawaziri kilichofanyika katika Hoteli ya Pullman, Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Wengine katika picha upande wa kulia ni Mabalozi wa Nchi wanachama wa SADC wanaowakilisha nchi zao DRC.
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa tatu kulia) akiongoza ujumbe wa SADC katika kikao alichokifanya na Mhe. Raymond Tshibanda (wa nne kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC ambaye  aliongozana na viongozi wa juu wanaoratibu uchaguzi nchini DRC.

==========================================



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MAHIGA AONGOZA UJUMBE WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC NCHINI DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe Augustine Mahiga yupo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi 13 Oktoba, 2016.

Mhe. Mahiga ambaye anaongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi hiyo yupo nchini humo kwa maagizo ya Mwenyekiti wa Asasi, Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutathmini hali ya siasa ilivyo nchini humo ili kushauri ipasavyo.

Aidha, tathmini hiyo inafanyika kufuatia hali tete ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama nchini DRC iliyochangiwa na maandamano yaliyofanyika tarehe 19 Septemba, 2016 ambayo yaliandaliwa na vyama vya upinzani kwa lengo la kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kutangaza tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Awali misheni hii ilikuwa ifanye ziara kati ya tarehe 4 na 5 Oktoba, 2016, lakini kutokana na ziara ya Kitaifa ya Mhe Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo hapa nchini ililazimu kuahirishwa. Aidha, kufuatia mazungumzo kati ya Mhe Rais John Pombe Joseph Magufuli, na Mhe Rais Jospeh Kabila wakati wa ziara hiyo walikubaliana Misheni hiyo ifanye ziara kwa tarehe hizo.

Hadi sasa Misheni hiyo imeweza kukutana na wadau mbalimbali ambapo imewasisitiza umuhimu wa kushiriki kwenye mjadala ikiwa ni njia pekee ya kuweza kuwakwamua hapo walipo pamoja na umuhimu wa uvumilivu wa kisiasa na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi kwa kipindi watakachokuwa wamekubaliana pamoja.

Wadau hao ni pamoja na Mabalozi wa Nchi SADC walioko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Mhe. Eden Kodjo, Msuluhishi Mkuu wa Umoja wa Afrika; Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wadau wengine ni Muungano wa vyama vilivyosusia kushiriki katika mjadala shirikishi wa kitaifa ( Rassamblement); Muungano wa vyama vinavyounda Serikali  (Presidential Majority); Asasi zisizo za kiserikali zinazoshiriki katika mjadala shirikishi wa kiitaifa; Asasi zisizoshiriki katika mjadala shirikishi wa kitaifa na Taaisi za kidini.

Itakumbukwa kuwa, Mkutano wa 36 wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika uliofanyika Mbabane, Swaziland mwezi Agosti 2016 ulimteua Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama. Nchi zingine zinazounda Asasi hii ni Angola (Makamu Mwenyekiti) na Msumbiji (Mwenyekiti anayeondoka).

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 11 Oktoba, 2016.

Monday, October 10, 2016

Rais Mhe. Dkt. Magufuli apokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi

Balozi wa Jamhuri ya Ghana mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe.Kwame Asamoah Tenkorang akisaini kitabu cha Wageni alipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Joseph Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Joseph Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. Kwame Asamoah Tenkorang Ikulu Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kaimu Mkuu wa Itifaki, Bw. James Bwana
Balozi wa Jamhuri ya Sudan mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi akisaini kitabu cha Wageni alipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Joseph Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Joseph Pombe Magufuli akipokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Sudan, Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi Ikulu Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Jamhuri ya Slovak mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe. Frantisek Dlhopolcek akisaini kitabu cha wageni kabla ya kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Slovak mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mhe. Frantisek Dlhopolcek Ikulu Jijini Dar es Salaam
Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Slovak. Wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (mwenye sketi nyeusi), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine (wa pili kulia) na Mshauri wa Rais masuala ya Diplomasia, Balozi Zuhura Bundala.
Balozi wa Ukraine mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Yevhenii Tsumbaliuk akisaini kitabu cha wageni Ikulu Jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Mhe. Rais, Dkt. Joseph Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Ukraine mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Yevhenii Tsymbaliuk Ikulu Jijini Dar es Salaam

Sunday, October 9, 2016

Naibu Waziri apokea hati za utambulisho kutoka kwa Waheshimiwa Mabalozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokea hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa  Jamhuri ya Slovak mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Frantisek Dlhopolcek, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokea hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Ukraine mwenye Makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Yevnii Tsymbaliuk Wizarani Jijini Dar es Salaam 
Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Ukraine mara baada ya kukabidhi hati ya utambulisho
Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba akiwa katika picha ya pomaja na  Balozi wa Ukraine Mhe. Yevnii Tsymbaliuk na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani  Balozi Joseph Sokoine
Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokea hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Ghana mwenye Makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Kwame Asamoah Wizarani Jijini Dar es Salaam 
Naibu Waziri Mhe. Susan Kolimba akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Ghana mara baada ya kukabidhi hati ya utambulisho. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Balozi Samuel Shelukindo.
Wakiwa katika picha ya pamoja

Friday, October 7, 2016

Rais Dkt. Magufuli akutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Nje ya nchi Ikulu Dar es Saalam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Eng. John Kijazi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hamisi Kigwangwalla katika picha ya kumbukumbu   na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi alipokutana nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 7, 2016.