Monday, August 15, 2022

WAZIRI MULAMULA: IMARISHENI BIASHARA KATI YA TANZANIA, DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) ameutaka Ubalozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuendelea na jitihada za kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini humo kufanya zaidi biashara na Tanzania. Balozi Mulamula ametoa agizo hilo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Congo, Mhe. Juma Mshana katika Ofisi za Ubalozi nchini humo.

Balozi Mulamula, ametembelea Ubalozi huo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrka (SADC) uliofanyika Kinshasa nchini humo. Mkutano wa Mawaziri pamoja na mambo mengine huandaa agenda mbalimbali ambazo zitawasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa lengo la kuidhinishwa au kutolewa maamuzi.

Mkutano wa Kawaida wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utafanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2022 ambapo ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Balozi Said Juma Mshana wakati akiwasili katika Ubalozi wa Tanzania -Kinshasa, DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi       Liberata Mulamula (Mb) akisaini katika kitabu cha Wageni katika Ubalozi wa Tanzania nchini DRC mara baada ya kuwasili katika ubalozi huo

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo DRC kushiriki Mkutano wa kawaida wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakimshuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Tanzania, DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na baadhi ya ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika Mkutano wa kawaida wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaotarajiwa kufanyika Agosti 17 na 18, 2022 Jijini Kinshasa, DRC


Saturday, August 13, 2022

DKT. KOFLER AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU SABA

Na Mwandishi wetu, Dar

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Bärbel Kofler amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia tarehe 13 – 20 August 2022.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Dkt. Kofler amepokelewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.  

Katika ziara yake nchini, Dkt. Kofler pamoja na mambo mengine, anatarajia kutembelea mradi wa ajira na ujuzi kwa maendeleo ya afrika (E4D) unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani, Kituo cha malezi na mafunzo kwa wasichana wadogo ambao ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu kilichopo Kibamba na Hospitali ya CCBRT Jijini Dar es Salaam. 

Maeneo mengine atakayotembelea Naibu Waziri huyo ni pamoja na Kituo cha Afya cha Ngamiani na Hospitali ya Bombo mkoani Tanga, Zahanati ya Mkanyageni Wilayani Muheza, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Asasi ya Tree of Hope iliyopo mkoani Tanga pamoja na Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika ziara yake nchini, Waziri Kofler anategemea kukutana na mawaziri wa sekta za afya, sheria, utalii, maendeleo ya jamii, fedha, nishati na maji kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler (katikati) akiongozana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga (kulia) baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania. 


Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler akisalimiana na Afisa kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akimueleza jambo Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Bärbel Kofler walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler akizungumza na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam



Friday, August 12, 2022

VACANCY ANNOUNCEMENT AT FAO AND WFP

 




BALOZI MGAZA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA OMAN

Na Mwandishi wetu, Dar

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Kukutana kwa viongozi hao kumelenga kuendelea kuimarisha masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Oman pamoja na kufuatilia masuala waliyokubaliana wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Oman mwezi Mei 2022.  

Viongozi hao pia wamejadili utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) pamoja na mikataba mbalimbali iliyosainiwa na pande hizo mbili. Aidha, mikataba ambayo hadi sasa imesainiwa ni ya ushikiano katika sekta za elimu, uwekezaji, maliasili, pamoja na ushirikiano katika chakula na usalama baina ya Tanzania na Oman. 

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamedajili namna bora ya kutekeleza Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Oman (JPC) ili kufungua zaidi maeneo mengine ya ushirikiano.  



Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza (hayupo pichani) katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza akimsikiliza Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan (hayupo pichani) walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza akimueleza jambo Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan walipokuwa kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


BALOZI FATMA ATETA NA UJUMBE WA SAUDI ARABIA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na ujumbe wa wataalam kutoka Wizara ya Mazingira, Maji na Kilimo ya Saudi Arabia ambao upo nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 10 -13 Aug,2022. 

Ujumbe huo umeambatana na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Ali Mwadini. Aidha, ziara hiyo ni matokeo ya ziara iliyofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula mwezi Machi 2022 nchini Saudi Arabia ambapo katika ziara hiyo ilikubaliwa kuwa wataalamu hao kufanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini katika sekta za kilimo na ufugaji. 

Pamoja na mambo mengine, wataalam hao wamekutana na wadau kutoka Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), Wizara ya Uchumi wa Buluu, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini (TAWA), Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) pamoja na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT).

Maeneo mengine ambayo ujumbe huo unatarajiwa kutembelea ni pamoja na kiwanda cha Tanchoice kilichopo Kibaha mkoani Pwani na Ranchi ya Mbogo ili kiujionea fursa za uwekeji katika maeneo hayo.

Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa ujumbe wa wataalamu kutoka Saudi Arabia, Mhandishi Abdulaziz Bin Abdulrahman Al-Huwaish katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na kiongozi wa ujumbe wa wataalamu kutoka Saudi Arabia, Mhandishi Abdulaziz Bin Abdulrahman Al-Huwaish katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Ali Mwadini,  Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na Ujumbe wa wataalamu kutoka Saudi Arabia katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




Wednesday, August 10, 2022

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA CCBRT KUBORESHA DIPLOMASIA YA AFYA

Na Waandishi wetu, Dar

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeahidi kushirikiana na Hospitali ya CCBRT kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya nchini kupitia utekelezaji wa Diplomasia ya Afya.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo kwa lengo la kujionea shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam 

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula ameupongeza Uongozi wa Hospitali hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia watanzania hasa kuwapa akina mama tumaini la maisha hususan wanaopatwa na changamoto ya ugonjwa wa fistula.

“Wizara ninayoisimamia ni mtambuka na mchango wake umekuwa mkubwa ambapo nyinyi ni wadau wetu, tutashirikiana na Balozi zetu nje kuona ni jinsi gani tutapata wadau/washirika wa maendeleo watakaosaidia katika kuboresha sekta ya afya hususan hapa CCBRT,” amesema Waziri Mulamula.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Brenda Msangi amesema kuwa pamoja na jitihada ambazo Serikali imekuwa ikizichukua kuboresha sekta ya afya nchini, hospitali hiyo pia inajitahidi kuboresha huduma zake na mazingira yake kwa ujumla ili kuweza kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi.

“Tunajitahidi kuwahudumia watanzania kadri tuwezavyo ila tunakabiliwa na baadhi ya changamoto za msaada wa utoaji wa huduma, vifaa tiba pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili kuweza kuboresha huduma zaidi,” amesema Bibi. Msangi.

Julai 05, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la kutolea huduma ya afya ya mama na mtoto katika hospitali ya CCBRT alisema kuwa mikakati ya kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga, Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma vya madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi wameanzisha mfumo wa kupitia takwimu za vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua lengo likiwa ni kuboresha zaidi huduma katika sekta ya afya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akioneshwa baadhi ya viungo bandia vinavyotengenezwa katika hospitali ya CCBRT na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bibi. Brenda Msangi. Balozi Mulamula alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea shughuli na huduma zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam.    

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akieleza jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bibi. Brenda Msangi hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika kikao na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bibi. Brenda Msangi wakati alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea shughuli na huduma zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na baadhi ya wagonjwa wakati alipofanya ziara ya kutembelea hospitali ya CCBRT kwa lengo la kujionea shughuli na huduma zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam

Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bibi. Brenda Msangi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati Mhe. Mulamula alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea shughuli na huduma zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam 

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiagana na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bibi. Brenda Msangi hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam 




JITAHADA ZAIDI ZINAHITAJIKA KUTANGAZA KAZI ZA WIZARA NDANI NA NJE YA NCHI- BALOZI MINDI



Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akiwasilisha mada ya Diplomasia ya Umma (Public Diplomacy) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam


Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam
                                     
Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Songalieli Shila akiwasilisha mada ya Umuhimu wa Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Songalieli Shila akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam


 Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Bw. Bernard Haule akiwasilisha mada ya Umuhimu wa Soko Huru la Biashara Barani Afrika iliyowasilishwa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakifuatilia mafunzo hayo 


 Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Songalieli Shila akiwa na baadhi ya washiriki wa mafunzo  ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga amesema kuwa kuwa jitahada zaidi zinahitajika kutangaza ndani na nje ya nchi kazi ambazo Wizara inazifanya.

Balozi Mindi ametoa kauli hiyo alipowasilisha mada ya Diplomasia ya Umma (Public Diplomacy) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa licha ya Wizara kufanya kazi kubwa bado kazi hizo hazijapata fursa ya kutangazwa ipasavyo na kuna haja ya kuongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha kazi hizo zinajulikana ndani na nje ya nchi.

Amesema waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kufanikisha azma hiyo ya Wizara kwa kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara. Balozi Kasiga aliahidi kuwa Wizara itaendelea kuandaa mafunzo hayo ambayo pamoja na mambo mengine yatawezesha kuwepo na orodha ya waandishi wenye ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia ambao watatambulishwa katika Jumuiya ya wanadiplomasia nchini na hivyo kuendelea kufanya nao kazi kwa ufanisi zaidi kuitangaza diplomasia ya Tanzania ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Mafunzo hayo ya siku mbili (tarehe 27-28/ Julai, 2022) yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Kitengo chake cha Mawasiliano (GCU) yamewashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini ikiwemo mitandao ya kijamii ambapo walieleza jinsi walivyofaidika na mada za mafunzo hayo zilizowasilishwa na mabalozi wabobezi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

 

Waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo walipata nafasi ya kusikiliza mada za Utekelezaji wa diplomasia ya uchumi iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Justin Kisoka; Uandishi wa taarifa za kidiplomasia iliyowasilishwa na Balozi Mstaafu Peter Kallaghe; Uzalendo katika kujenga na kulinda tasiwra ya Tanzania iliyowasilishwa na Balozi Mstaafu Patrick Tsere; Diplomasia ya Umma iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (GCU), Balozi Mindi Kasiga; Umuhimu wa Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Songalieli Shila; na Umuhimu wa Soko Huru la Biashara Barani Afrika iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw. Bernard Haule.

Mada hizo zililenga kuwapatia waandishi wa habari ufahamu kuhusu majukumu, malengo na mikakati ya Wizara katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.

Wawasilishaji mada walitumia fursa hiyo kuwaelimisha waandishi wa habari hao kuhusu agenda za nchi katika Jumuiya ya Kimataifa zikiwemo kutumia Soko Huru la Biashara barani Afrika kwa manufaa ya kiuchumi.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula tarehe 27 Julai, 2022 ambapo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ni wadau muhimu na kuwaahidi kuwa Wizara itaendelea kuimarisha uhusiano na kundi hilo muhimu kwa kuwawekea mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA CANADA BAADA YA KUMALIZA MUDA WA UWAKILISHI

Na Waandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), ameagana na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Balozi O'Donnell Waziri Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji kazi wake ambao umewezesha Serikali ya Tanzania na Canada kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu pamoja na biashara na uwekezaji.

Waziri Mulamula ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Canada ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi O'Donnell wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.

“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Canada na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa na Tanzania na Canada. Kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za afya na elimu pamoja na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Canada na kokote uendako Duniani,” amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell amesema anajivunia uwepo wake Tanzania, amejifunza mengi ikiwemo ukarimu wa Watanzania na amewashukuru Watanzania kwa upendo mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini.

“Naishukuru Tanzania na watu wake kwa ukarimu na ushirikiano walionionesha wakati natekeleza majukumu yangu ya kibalozi hapa nchini, kwa kweli ni ngumu sana kuaga na kusema kwaheri lakini hakuna budi, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania,” amesema Mhe. Balozi O'Donnell.

Pamoja na mambo mengine, Balozi O'Donnell ameihakikishia Tanzania kuwa Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya gesi pamoja na biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Canada wamekuwa wakiridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji na baadhi yao wameonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika sekta ya gesi Tanzania,” ameongeza Balozi O'Donnell

Kadhalika, Balozi O’Donell amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania ya kuimarisha ukuaji wa Uchumi, utoaji wa huduma bora za afya, elimu ya msingi bure kwa watanzania pamoja na kuboresha miundimbinu kwa maendeleo ya watanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula  akizungumza na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakifuatilia kikao cha Waziri Mulamula na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula  katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula  akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


TAARIFA KWA UMMA

 






Tuesday, August 9, 2022

DKT. KIKWETE ASHUHUDIA UPIGAJI KURA, KENYA

Rais Mstaafu wa Tanzania na Kiongozi wa Timu ya waangalizi ya Uchaguzi  Mkuu wa Kenya, ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya wajumbe 52 kutoka taasisi na mashirika ya kiraia ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inashuhudia zoezi la upigaji kura la uchaguzi mkuu nchini Kenya lililoanza Leo mapema asubuhi.

Kabla ya uchaguzi huo  Dkt. Kikwete alikutana na wadau mbalimbali wakiwemo wagombea wa Urais kupitia chama cha Muungano wa Azimio la Umoja, Mhe. Raila Odinga na mgombea Urais wa chama cha UDA,vMhe. William Ruto.

Rais Mstaafu wa Tanzania na Kiongozi wa Timu ya waangalizi ya Uchaguzi  Mkuu wa Kenya, ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na mgombea Urais wa chama cha UDA, William Ruto. Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni Jijini Nairobi

Rais Mstaafu wa Tanzania na Kiongozi wa Timu ya waangalizi ya Uchaguzi  Mkuu wa Kenya, ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na mgombea Urais wa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga hivi karibuni Jijini Nairobi

Rais Mstaafu wa Tanzania na Kiongozi wa Timu ya waangalizi ya Uchaguzi  Mkuu wa Kenya, ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na mgombea Urais wa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga Jijini Nairobi

Rais Mstaafu wa Tanzania na Kiongozi wa Timu ya waangalizi ya Uchaguzi  Mkuu wa Kenya, ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na mgombea Urais wa chama cha UDA, William Ruto Jijini Nairobi


Sunday, August 7, 2022

SERIKALI YAWAHAHIKISHIA WAWEKEZAJI MAZINGIRA SALAMA YA UWEKEZAJI NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Pwani

Serikali imeendelea kuwahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ina mazingira rafiki na salama kwa uwekezaji na inaendelea kuweka mikakati mahususi ya kuimarisha na kuendeleza sekta ya viwanda ili kuongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umaskini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo jana wakati aliposhiriki katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula amewahakiki wawekezaji kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati mahsusi ya kuimarisha na kuendeleza sekta ya viwanda ili kuongeza ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umaskini.

“Serikali inaendelea kuwalinda wawekezaji wote wanaoamua kuanzisha viwanda hapa nchini kwa kuwapatia vivutio maalumu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara,” amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Kilimo ya Cuba, na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Cuba, Bw. Orlando Diaz Rodriguez amesema kuwa Cuba imekuwa ikijivunia ushirikiano wake na Tanzania na kwamba wanaamini kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo ulidumu kwa miaka 60.

“Kuanzishwa kwa kiwanda hiki cha Labiofam ni Faraja kwetu sisi Cuba, kiwanda hiki ni nguzo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba…….pia ufanyaji kazi wa kiwanda hiki utasaidia sana kupunguza kasi ya Malaria nchini Tanzania,” amesema Bw. Rodriguez

Bw. Rodriguez ameongeza kuwa, Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za afya, elimu na kilimo  pamoja na kuhakikisha kuwa mataifa hayo mawili yanaimarisha misingi ya kidiplomasia baina yao.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Aboubakari Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unaongoza kwa Viwanda ambapo kuna viwanda 1,453 na kati ya hivyo 87 ni viwanda vikubwa.

“Upatikanaji wa nishati, maji na miundombinu imara ni mambo muhimu katika uwekezaji wa viwanda. Tatizo la maji na nishati halipo tena katika mkoa wa pwani hivyo nawasihi wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuja kuwekeza Tanzania hususan Kibaha kwani maeneo ya kuwekeza yapo ya kutosha na mazingira ni mazuri,” amesema Mhe. Kunenge

Juni 29, 2022 Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla akiwa chini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Mhe. Balozi Liberata Mulamula, aliahidi kuboresha utendaji wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha, Pwani ili malengo ya uwekezaji pamoja na yale ya kudhibiti malaria yaweze kufikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Kilimo ya Cuba, na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Cuba, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamona na Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe wakishuhudia utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamona na Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania, Kibaha Mkoa wa Pwani


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na viongozi mbalimbali wakipata maelezo kuhusu kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania walipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho Kibaha Mkoa wa Pwani


Thursday, August 4, 2022

WAZIRI MULAMULA AWAAGA MABALOZI WA SWEDEN, FINALAND

Na Waandishi wetu, Dar 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameagana na mabalozi wa Sweden na Finland nchini, Mhe. Anders Sjöberg na Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa utumishi nchini Tanzania.

Waziri Mulamula amewaaga mabalozi hao kwa nyakati tofauti leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo amempongeza Balozi wa Sweden Mhe. Sjöberg kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania wakati wote wa uwakilishi hapa nchini.  

 Waziri Mulamula amempongeza Balozi wa Sweden kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kuendeleza uhusiano baina ya Sweden na Tanzania ambapo Sweden imekuwa na mchango mkubwa katika miradi ya maendeleo vijijini, biashara na uwekezaji pamoja na elimu.

“Biashara kati ya nchi zetu mbili bado ipo chini, hivyo nimemhimiza Mhe. Sjöberg pamoja na kuwa amemaliza muda wake wa uwakilishi aendelee kuwasihi wafanyabiashara kutoka Sweden kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Balozi Mulamula 

Waziri Mulamula amesema mbali na sekta za biashara na uwekezaji pamoja na elimu,Tanzania itaendelea kushirikiana na Sweden katika sekta za afya, nishati na utalii hasa katika kuitangaza filamu ya ‘The Royal Tour’. 

Kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Finland, Balozi Mulamula ameongeza kuwa Finland na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu na wa karibu ambapo kupitia ushirikiano huo Finland imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa misaada katika mradi wa ukusanyaji wa kodi pamoja na mradi wa kuendeleza misitu.

Kwa upande wake Balozi wa Sweden Mhe. Sjöberg ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliompatia wakati wote alipokuwa nchini akitekeleza majukumu yake ya kibalozi.

“Naondoka baada ya kumaliza muda wangu wa uwakilishi hapa Tanzania lakini kwa jinsi nilivyofanya kazi na watanzania, Tanzania ni sawa na nyumbani…….nafarijika pia kuona masuala ya utawala bora, amani na usalama pamoja na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi vikiwa vimeboreshwa kwa kiasi kikubwa,” amesema Balozi Sjöberg

Naye Balozi wa Finland, Mhe. Swan ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Mhe. Swan ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya Finland na Tanzania na amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

“Nimekuwa hapa nchi kwa zaidi ya miaka mitatu, mambo mengi yamebadilika kwa sasa nimefurahishwa na maboresho katika ukuaji na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji……naiona Tanzania ya mafanikio siku za karibuni,” amesema Balozi Swan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akimuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiagana na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini



TANZANIA NA CHINA ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya watu wa China zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo kwa kuzingatia misingi ya ushirikiano wa kirafiki kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mulamula amesema katika mazungumzo yao wamejadili masuala mbalimbali, ikiwemo suala la namna ya kuimarisha misingi ya ushirikiano baina ya mataifa hayo.

"Tanzania tutaendelea kuzingatia kwa dhati kanuni ya kuwa na China moja, kuunga mkono kwa dhati msimamo halali wa China, kuunga mkono China katika kulinda maslahi yake ya msingi," amesema Waziri Mulamula

Kwa Upande wake Balozi wa China nchini, Mhe. Mingjian amesema kuwa Serikali yake wakati wote imekuwa rafiki mzuri kwa Serikali ya Tanzania na kwamba urafiki wa nchi hizo mbili umekuwa mfano mzuri wa kuigwa na China itaendelea kuheshimu na kuenzi urafiki huo.

"Tunathamini ushirikiano kati ya Tanzania na China, uhusiano huu umejengwa katika misingi imara na isiyotikisika…..China itaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha uhusiano bora kati yake na Tanzania," amesema Balozi Mingjian.

Uhusiano kati ya Tanzania na China ulianza mapema miaka ya 1960 wakati nchi hizo mbili zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 9 Desemba 1961.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Balozi Mindi Kasiga pamoja na Afisa kutoka ubalozi wa China katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam