Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam |
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga amesema kuwa kuwa jitahada zaidi zinahitajika kutangaza ndani na nje ya nchi kazi ambazo Wizara inazifanya.
Balozi Mindi ametoa kauli hiyo alipowasilisha mada ya
Diplomasia ya Umma (Public Diplomacy) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo
waandishi wa habari na utaalamu na ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia
yaliyofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa licha ya Wizara kufanya kazi kubwa bado kazi
hizo hazijapata fursa ya kutangazwa ipasavyo na kuna haja ya kuongeza jitihada
zaidi ili kuhakikisha kazi hizo zinajulikana ndani na nje ya nchi.
Amesema waandishi wa habari ni wadau muhimu katika
kufanikisha azma hiyo ya Wizara kwa kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano cha
Wizara. Balozi Kasiga aliahidi kuwa Wizara itaendelea kuandaa mafunzo hayo
ambayo pamoja na mambo mengine yatawezesha kuwepo na orodha ya waandishi wenye
ujuzi wa kuandika taarifa za kidiplomasia ambao watatambulishwa katika Jumuiya
ya wanadiplomasia nchini na hivyo kuendelea kufanya nao kazi kwa ufanisi zaidi
kuitangaza diplomasia ya Tanzania ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Mafunzo hayo ya siku mbili (tarehe 27-28/ Julai, 2022)
yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kupitia Kitengo chake cha Mawasiliano (GCU) yamewashirikisha waandishi wa
habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini ikiwemo mitandao ya
kijamii ambapo walieleza jinsi walivyofaidika na mada za mafunzo hayo
zilizowasilishwa na mabalozi wabobezi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo walipata
nafasi ya kusikiliza mada za Utekelezaji wa diplomasia ya uchumi
iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Justin
Kisoka; Uandishi wa taarifa za kidiplomasia iliyowasilishwa na Balozi Mstaafu
Peter Kallaghe; Uzalendo katika kujenga na kulinda tasiwra ya Tanzania iliyowasilishwa
na Balozi Mstaafu Patrick Tsere; Diplomasia ya Umma iliyowasilishwa na
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (GCU), Balozi Mindi Kasiga;
Umuhimu wa Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa
iliyowasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Ushirikiano wa
Kimataifa, Bw. Songalieli Shila; na Umuhimu wa Soko Huru la Biashara Barani
Afrika iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za
Uzalishaji, Bw. Bernard Haule.
Mada hizo zililenga kuwapatia waandishi wa habari ufahamu
kuhusu majukumu, malengo na mikakati ya Wizara katika utekelezaji wa Sera ya
Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.
Wawasilishaji mada walitumia fursa hiyo kuwaelimisha
waandishi wa habari hao kuhusu agenda za nchi katika Jumuiya ya Kimataifa
zikiwemo kutumia Soko Huru la Biashara barani Afrika kwa manufaa ya kiuchumi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula tarehe 27 Julai, 2022
ambapo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ni wadau muhimu na kuwaahidi kuwa
Wizara itaendelea kuimarisha uhusiano na kundi hilo muhimu kwa kuwawekea
mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mafunzo ya mara kwa mara ili
waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.