Tanzania imeihakikishia Qatar kuwa ipo tayari kutoa vijana watakaoweza kufanya kazi nchini humo, hususan katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya nguvukazi ni makubwa kutokana na nchi hiyo kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Kombe la Dunia yatakayochezwa mwezi Novemba 2022.
Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi yaliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar tarehe 28 Agosti 2022.
Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Mkataba wa Kazi uliosainiwa kati ya Tanzania na Qatar mwaka 2014.
“Tunawapongeza Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA litakaloanza mwezi Novemba mwaka huu. Aidha, napenda kukufahamisha kuwa Tanzania imewaandaa vijana wake wenye ujuzi na hivyo tunaomba kupata nafasi za ajira na za viza (visa allocation) kwa ajili ya Watanzania kuweza kuja kufanya kazi huku hasa wakati huu wa kombe la dunia,” aliongeza Balozi Fatma
Katika Kikao hicho, viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo ya uwekezaji na biashara. Balozi Fatma alieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya mazingira ya uwekezaji na biashara, hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Qatar kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali kama vile utalii, kilimo, madini, maliasili, uvuvi na utamaduni.
“Napenda kukuhakikishia kuwa Tanzania inazo fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji na tunawakaribisha Serikali ya Qatar pamoja na wananchi wenu kuja kuwekeza nchini hususan katika sekta za utalii, madini, biashara na uwekezaji,” ameeleza Balozi Fatma.
Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi Patricia Kiswaga.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.