Tuesday, August 30, 2022

TANZANIA NA SINGAPORE KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Serikali ya Tanzania na Singapore zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kihistoria uliopo baina yao ili kutekeleza kwa ufanisi malengo ya kiuchumi ya mataifa hayo.

Ahadi hiyo imetolewa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake Singapore, Mhe. Douglas Foo yaliyofanyika tarehe 30 Agosti 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi Mulamula alieleza kuwa ni muhimu kwa Tanzania na Singapore kuuenzi ushirikiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa yao kwa manufaa ya wananchi wake.

Pia alieleza Tanzania ina nia ya kushirikiana na Singapore katika maeneo mbalimbali ikiwemo: Kukuza shughuli za bandari, kilimo cha mbogamboga na matunda, usafirishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa na chai, biashara, utalii, ufadhili wa masomo na ushirikiano katika masuala ya utamaduni hususan kuanzisha makubaliano ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Singapore.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na: Kujenga uwezo katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, uwekezaji katika maeneo maalum ya viwanda, usafiri wa anga na ushirikiano katika masuala ya kikanda.

“Tanzania inawekeza katika kujenga uwezo wa rasilimali watu kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, pia kupitia uwepo wa mkongo wa mawasiliano wa taifa ina dhamira ya kutoa huduma ya mawasiliano nje ya mipaka yake” alisema Balozi Mulamula.

Kwa upande wa Mhe. Douglas Foo alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Singapore unatimiza miaka 40 tangu ulipoanzishwa hivyo, ni muhimu kuangalia maeneo yenye fursa za kiuchumi ili kuendelea kuimarisha ushirikiano kwa manufaa kwa pande zote mbili.

Tanzania na Singapore zinaunganishwa na uanachama wao katika Umoja wa nchi za jumuiya ya madola na hivyo ni fursa kwa mataifa hayo kuongeza maeneo ya ushirikiano kupitia makubaliano yatakayowezesha usimamizi wa karibu wa utekelezaji wa malengo katika maeneo husika ya maendeleo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Douglas Foo alipomtembelea katika ofisi za Wizara tarehe 30 Agosti 2022 jijini Dodoma.

Mhe. Douglas Foo akifafanua juu ya uzoefu wa Singapore katika kusimamia makubaliano mbalimbali yanayoanzishwa na serikali yake kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mazungumzo yakiendelea.
 Mhe. Balozi Mulamula akiagana na Mhe. Foo baada ya mazungumzo. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.