Tuesday, August 2, 2022

RAIS SAMIA, HICHILEMA WAKUBALIANA KUBORESHA UHUSIANO

Na Mwandishi wetu, Dar 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu kufufua ushirikiano baina ya nchi hizo ambao ulikuwa umelegalega.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo Mhe. Hichilema alikuja kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku moja.

Rais Samia amesema kuwa Tanzania na Zambia ni nchi ambazo zilikuwa karibu zikiwa na urafiki na undugu ambao ulianzishwa na waasisi wa mataifa hayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa upande wa Tanzania na Hayati Keneth Kaunda wa Zambia.

“Wazee hawa ndio walioshirikiana kuleta ukombozi kusini mwa bara la Afrika lakini kwa upande wao katika nchi zetu mbili wakatuanzishia mambo ambayo walitaka yadumu milele na yatuunganishe,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa katika kurudisha undugu wameangalia maeneo yote ambayo yatachochea kurudi huko kwa kuangalia uhusiano wa kisiasa na kuongoza wananchi wao katika kuelewana vyema.

Mbali na hayo Rais Samia amesema wamejadili masuala ya usalama wa nchi hizo na kuangalia changamoto za kiusalama zinazokabili ukanda wao ikiwemo ugaidi na kukubaliana kushirikiana.

Wawili hao walizungumzia pia masuala ya uchumi ambapo walikubaliana kufufua upya miundombinu ya kiuchumi baina ya nchi hizo ikiwemo reli ya TAZARA na Bomba la mafuta la TAZAMA.

Rais Samia alisema wamekubaliana kuboresha reli ya TAZARA kwa kuijenga kwa kiwango cha kisasa (SGR) ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kidunia.

“Tumekubaliana tuboreshe TAZARA kama tunaifanyia marekebisho reli iliyopo lakini tukakubaliana kwamba kwa dunia ya leo reli ni SGR, kwahiyo tutakuwa na mradi wa pamoja tutafute pesa kwa pamoja kupitia PPP pengine na marafiki waliotujengea reli hiyo tuone jinsi tutakavyoboresha kwa kiwango cha SGR,” amesema Rais Samia.

Kuhusu Bomba la mafuta la TAZAMA marais hao wamekubaliana kuwa lililopo ni dogo ikilinganishwa na mahitaji na hivyo kuona haja ya kujenga lingine kubwa kwani kwa sasa bomba la TAZAMA halifanyi kazi kama ilivyokusudiwa kutokana na mabadilko ya sera za Nishati za Zambia.

“Tumekubaliana bomba lile (TAZAMA) ni dogo sana kwahiyo kuna haja ya kujenga kubwa litakalopeleka mafuta kwa wingi na bandari ya Dar es Salaam na miundombinu iliyopo Tanzania iwasaidie kupunguza ughali wa mafuta katika nchi yao,” ameongeza Rais Samia

Kadhalika viongozi hao walijadili kuhusu biashara na uwekezaji ambapo pamoja na mambo mengine,  wameangalia vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi na kukubaliana mamlaka zinazoshulika na kodi na forodha kukutana na kuangalia mambo ya kuondoa ili kuruhusu biashara baina ya nchi hizo kufanyika vizuri.

Rais Samia alisema wamewazungumzi pia wafanyabishara wadogowadogo wanaovuka mipaka na kubaini kuwa masharti wanayopewa ni makubwa kuanzia vibali vya kuingia hadi tozo.

“Tumeagiza Mawaziri wakae na kuangalia jinsi ya kusaidia biashara ziendelee bila matatizo,” amesema Rais Samia.

Vilevile wamejadili changamoto za madereva na kukubaliana taasisi za madereva za Zambia na Tanzania ziwekwe pamoja zizungumze na Serikali zote mbili na kuona ni jinsi gani changamoto zinazowakabili zinaondolewa.

Rais Samia ameongeza kuwa katika mazungumzo yao waligusia mambo ya kilimo ambapo wameona kuwa wote ni wazalishaji wa soya ambayo ina soko nje ya nchi zetu, na kwamba Zambia wapo vizuri katika uzalishaji wa mbegu.

“Tumekubaliana tusishindane lakini tuongezeane uwezo, wenzetu ni mabingwa wa uzalishaji wameendelea kidogo wana mbegu nzuri na tumezungumza kwamba linapokuja suala la mbegu mnatutoza sana akaniambia basi tuzungumze tuuziane kirafiki na kindugu.”

“Tumekubaliana kufanya kazi kwa pamoja na kama mmoja ana soko amwambie mwingine kuna soko hapa na sisi leo tumeofa soko la nyama, ng’ombe na kondoo tuna soko kubwa tumelipata Saudia Arabia tumewaalika wenzetu waje twende tukalitumie hilo soko,” amesema Rais Samia

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema amesema viongozi wa nchi hizo mbili  ni kizazi ambacho kinatakiwa kuendeleza  urithi ulioachwa na waasisi  Keneth Kaunda na Julius Nyerere.

“Tumekubaliana na dada yangu Rais Samia kuendeleza urafiki wetu katika mambo mbalimbali kama vile masuala ya utamaduni kwa sababu ukienda maeneo kama Nakonde au Tunduma kuna familia ambazo shangazi anaishi upande wa Zambia na mjomba anaishi upande wa Tanzania kwa hiyo sisi ni ndugu.

“Tunaangalia pia namna ya kutumia umoja wetu kupitia majukwaa kama SADC, Nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa ikizingatiwa Tanzania ni nchi wanachama kote, sisi hatupo baadhi lakini tunaweza kufaidika na uwepo wa Tanzania kwenye umoja huo,” amesema Rais Hichilema 

Rais Hichilema ameongeza kuwa Zambia imepanga kuimarisha uhusiano na Tanzania na kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili.

Aidha, Mhe. Hichilema amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kwenye sekta ya madini ambapo imewawezesha wachimbaji wadogo na kuwainua hadi kuwa wachimbaji wakubwa.

Katika hafla hiyo pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo  wamesaini mikataba mitatu ya ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama pamoja na sanaa na utamaduni.

Akifafanua kuhusu ziara hiyo, Waziri Mulamula alisema mikataba miwili inahusu ulinzi na usalama ambapo nchi hizo zitashirikiana kwenye masuala ya kijeshi pamoja na mafunzo kwa maofisa wa ngazi za juu kwenye masuala ya ulinzi na usalama wakati mkataba wa tatu utahusu masuala ya sanaa na utamaduni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema wakisalimiana na viongozi mbalimbali waliofika kwenye mapokezi baada ya Mhe. Hichilema kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema wakisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula baada ya Mhe. Hichilema kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema wakati nyimbo za Taifa (Tanzania na Zambia) zikiimbwa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wanahabari (hawapo pichani) katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema Ikulu Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo  wakionesha mikataba waliyosaini. Mikataba hiyo ni ya ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama pamoja na sanaa na utamaduni

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku moja Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku moja Jijini Dar es SalaamNo comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.