Tuesday, August 30, 2022

MIRADI NANE YA KIPAUMBELE YAWASILISHWA TICAD8


Serikali ya Tanzania imewasilisha miradi nane ya kipaumbele yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.334 katika Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD8) uliohitimishwa tarehe 28 Agosti 2022 jijini Tunis nchini Tunisia. 

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) aliyaeleza hayo jana tarehe 29 Agosti, 2022 akiwa nchini Tunisia ambako alimwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo. 

Miradi hiyo nane ambayo itatekelezwa Tanzania Bara na Tanzania - Zanzibar imetajwa kuwa ni; ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete, ujenzi wa bwawa la kusambaza maji la Lugoda, Mufindi Mkoani Iringa, ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, ujenzi wa njia ya umeme ya Songa-Fungu-Mkuranga, uanzishwaji wa maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi, kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam na ujenzi wa bandari nne za kisasa za uvuvi

Sambamba na miradi hiyo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa, licha ya Tanzania kunufaika na ujenzi wa daraja la Mfugale, mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II kupitia TICAD, vilevile amewasilisha maombi ya kukamilishiwa miradi mitatu ya ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili, Bandari ya Kigoma na mradi wa maji wa Zanzibar yenye thamani ya dola za Marekani milioni 343.8.

Mbali na kushiriki TICAD 8, Waziri Mkuu kwa nyakati tofauti alifanya mikutano ya pembezoni na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Bw. Yasuteru Hirai na Mwenyekiti wa Bodi ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) Bw. Mutsuo Iwai 

Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu amewashukuru na kuwapongeza wadau hao kwa kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana wilayani Urambo iliyojengwa na JTI, ambapo pia ametoa rai kwa kampuni hiyo kuendelea kununua zao la tumbaku nchini sambamba na kuongeza kiwango cha ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima.

Waziri Mkuu vilevile amewapongeza watendaji wa Kampuni ya Mitsubishi kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme mkoani Kilimanjaro na akatoa rai waangalie uwekezekano wa kujenga kiwanda cha uzalishaji mbolea nchini.

Kwa upande wake Rais wa JICA Dkt. Tanaka, amemuahidi Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa maisha ya kila siku ya Watanzania, pia ameahidi kuwarudisha wafanyakazi waliokuwa wakijitolea katika sekta mbalimbali nchini ambao walilazimika kurudi Japan kwa sababu ya janga la UVIKO-19. 

Rais wa JICA Dkt. Tanaka alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuelezea furaha yake na kufikisha shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia makala ya chapisho kuhusu TICAD 8. 

Miradi hiyo nane iliyowasilishwa TICAD8 ni yakipaumbele kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III).
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) akisalimiana na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka walipokutana kwa mazungumzo jijini Tunis nchini Tunisia.
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Dkt. Akihiko Tanaka yaliyofanyika jijini Tunis nchini Tunisia
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Mbarouk (Mb.) akichangia jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA.
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango - Zanzibar Bw. Aboud Mwinyi, akichangia jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri Mkuu na Rais wa JICA
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na ujumbe wake akiwa na katika picha ya pamoja na ujumbe wa JICA. 

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na ujumbe wake akiwa na katika picha ya pamoja na ujumbe wa JICA

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Bw. Yasuteru Hirai, yaliyofanyika jijini Tunis nchini Tunisia

8. 




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.