Sunday, August 7, 2022

SERIKALI YAWAHAHIKISHIA WAWEKEZAJI MAZINGIRA SALAMA YA UWEKEZAJI NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Pwani

Serikali imeendelea kuwahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ina mazingira rafiki na salama kwa uwekezaji na inaendelea kuweka mikakati mahususi ya kuimarisha na kuendeleza sekta ya viwanda ili kuongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umaskini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo jana wakati aliposhiriki katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula amewahakiki wawekezaji kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati mahsusi ya kuimarisha na kuendeleza sekta ya viwanda ili kuongeza ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umaskini.

“Serikali inaendelea kuwalinda wawekezaji wote wanaoamua kuanzisha viwanda hapa nchini kwa kuwapatia vivutio maalumu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara,” amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Kilimo ya Cuba, na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Cuba, Bw. Orlando Diaz Rodriguez amesema kuwa Cuba imekuwa ikijivunia ushirikiano wake na Tanzania na kwamba wanaamini kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo ulidumu kwa miaka 60.

“Kuanzishwa kwa kiwanda hiki cha Labiofam ni Faraja kwetu sisi Cuba, kiwanda hiki ni nguzo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba…….pia ufanyaji kazi wa kiwanda hiki utasaidia sana kupunguza kasi ya Malaria nchini Tanzania,” amesema Bw. Rodriguez

Bw. Rodriguez ameongeza kuwa, Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za afya, elimu na kilimo  pamoja na kuhakikisha kuwa mataifa hayo mawili yanaimarisha misingi ya kidiplomasia baina yao.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Aboubakari Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unaongoza kwa Viwanda ambapo kuna viwanda 1,453 na kati ya hivyo 87 ni viwanda vikubwa.

“Upatikanaji wa nishati, maji na miundombinu imara ni mambo muhimu katika uwekezaji wa viwanda. Tatizo la maji na nishati halipo tena katika mkoa wa pwani hivyo nawasihi wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuja kuwekeza Tanzania hususan Kibaha kwani maeneo ya kuwekeza yapo ya kutosha na mazingira ni mazuri,” amesema Mhe. Kunenge

Juni 29, 2022 Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla akiwa chini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Mhe. Balozi Liberata Mulamula, aliahidi kuboresha utendaji wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha, Pwani ili malengo ya uwekezaji pamoja na yale ya kudhibiti malaria yaweze kufikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Kilimo ya Cuba, na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Cuba, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamona na Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe wakishuhudia utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania (Tanzania Biotech Products Ltd) Kibaha Mkoa wa Pwani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamona na Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya utiaji saini mkataba wa uzalishaji mbolea na viuatilifu hai katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania, Kibaha Mkoa wa Pwani


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na viongozi mbalimbali wakipata maelezo kuhusu kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibiolojia Tanzania walipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho Kibaha Mkoa wa Pwani


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.