Kamishina Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa (UNHCR), Bw. Filippo Grandi yupo nchini tokea tarehe 24 Agosti 2022 kwa
ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na viongozi
wakuu wa Serikali na kutembelea Kambi za Wakimbizi mkoani Kigoma.
Bw. Grandi ambaye leo tarehe 25 Agosti ametembelea
Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu ya mkoani Kigoma na baadaye kuwasili mkoani
Dodoma na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na huduma
bora zinazotolewa kwa Wakimbizi ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita
alipofanya ziara kama hiyo mwaka 2019.
Kwenye Kambi ya Nyarugusu, ambayo inahifadhi
Wakimbizi zaidi ya 130,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi,
Bw. Grandi alijionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi hao na kusikiliza
maelezo ya wawakilishi wao pamoja na taasisi mbalimbali zinazohudumia
wakimbizi.
Baada ya kusikiliza maelezo, Bw Grandi
aliahidi kuwa UNHCR itaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo Serikali Ili
kuboresha maisha ya wakimbizi pamoja na kukabiliana na athari zitokanazo na
shughuli za wakimbizi kama vile uharibifu wa mazingira.
Ziara ya Bw. Grandi nchini imekuja kufuatia
mazungumzo yake aliyofanya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan jijini New York wakati wa Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa mwaka 2021. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana kwa bashasha na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Filippo Grandi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Bw. Grandi yupo nchini kwa ziara ya kikazi. |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Filippo Grand kwenye chumba cha wageni maalum cha Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendeguza na kushoto ni Mkurugenzi wa UNHCR wa Kanda ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Bibi Clementine Awu Nkweta |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.