Friday, January 27, 2023

TANZANIA, INDIA KUFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA

Tanzania na India zimeonesha dhamira ya kufanya kazi kwa karibu katika kutafuta njia bora za kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.)  amesema kufunguliwa kwa soko la parachichi nchini India mwaka 2022 ni miongoni mwa mifano ya hatua zilizochukuliwa za kuimarisha biashara kati ya Tanzania na India. 

Balozi Mbarouk amesema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 74 ya Jamhuri ya India zilizofanyika tarehe 26 Januari 2023 katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam.

“India ni mshirika wa tatu kwa ukubwa wa kibiashara na Tanzania na imekuwa miongoni mwa wawekezaji watano bora kwa kuwekeza Dola za Kimarekani bilioni 4.58 kwa mwaka 2021/22. Usawa wa kibiashara katika mwaka huo ulikuwa sawa na miradi 630 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 3.68 iliyozalisha ajira mpya 60,000,” alisema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa wawekezaji wa India wameonesha nia ya kuwekezaka nchini Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile madini, utalii, viwanda, kilimo, usindikaji wa mazao ya kilimo, nishati, usafirishaji, ujenzi, huduma za fedha na maendeleo ya rasilimali watu umekuwa ukiongezeka kwa kasi. 

“Sekta nyingine wawekezaji wa India walizowekeza nchini Tanzania ni pamoja na afya, elimu, maji, teknolojia ya Habari na mawasiliano. Mfano, Mwezi Juni 2022 tulishuhudia kampuni sita kutoka India zikisaini kandarasi ya uchimbaji wa visima vya maji katika miji 28 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 500, kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha watanzania milioni sita (6) kupata maji safi na salama,” aliongeza Balozi Mbarouk

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na India katika kuendeleza na kuimarisha misingi ya ushirikiano iliyowekwa na waasisi wa Mataifa yetu mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mahatma Gandhi. “tutaendelea kutafuta maeneo mapya yenye fursa za kushirikiana ili kuimarisha zaidi ushirikiano wetu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa,” aliongeza Balozi Mbarouk.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania ambapo uhusiano huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa mataifa yote mawili. 

Balozi Pradhan alisema kuwa katika kipindi cha baada ya uhuru, uhusiano kati ya India na Tanzania umestawi na kuchochea misingi ya kuongezeka kwa uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kwa pande zote mbili.

“Tunaendelea kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha nchi hizi mbili zinakua kiuchumi, hivyo ushirikiano wa India na Tanzania ni muhimu katika kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo yanaimarika,” alisema Balozi Pradhan

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akihutubia sherehe za maadhimisho ya 74 ya Jamhuri ya India jana jioni katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akihutubia sherehe za maadhimisho ya 74 ya Jamhuri ya India jana jioni katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam


Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan akihutubia sherehe za maadhimisho ya 74 ya Jamhuri ya India jana jioni katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam

Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan akihutubia sherehe za maadhimisho ya 74 ya Jamhuri ya India jana jioni katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed pamoja na Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan  



Wednesday, January 25, 2023

CFR WAASWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA MSINGI

Chuo cha Diplomasia (CFR) kimeaswa kutekeleza majukumu yake ya msingi ili kukifanya chuo hicho kuwa kituo mahiri cha diplomasia.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipotembelea chuo hicho kilichopo Jijini Dar es Salaam na kuzungumza na watumishi wake.

Dkt. Tax amekitaka chuo hicho kifanye tafiti mahsusi za kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali kwenye jamii hususani za kistratejia na kiintelijensia na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa chuo hicho.

Amekitaka chuo kupanua wigo wa programu kutokana na ongezeko la wanafunzi ambao wanahitaji kujiunga na chuo hicho na kuandaa mpango wa kitaifa wa kutekeleza diplomasia ya uchumi. 

“Chuo kinapaswa kiongeze wigo wa mafunzo yake kama vile kutoa mafunzo ya strategia, kifanye tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia,……….tafiti hizo zitachangia kuimarisha diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabili changamoto zinazoikabili Serikali katika eneo hilo,” alisisitiza Dkt. Tax

Aidha, Dkt. Tax ameongeza kuwa, kila mhadhiri na mtumishi chuoni hapo anapaswa kuzingatia maadili na sheria kwani maadili ni sehemu muhimu katika eneo la kazi na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kutoa wahitimu wenye maadili na tabia njema ambayo ni sifa kwa chuo.

Dkt. Tax pia amewahahakishia watumishi wa Chuo hicho kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na chuo hicho katika kuhakikisha kinaboresha mazingira yake ili kiendelee kuzalisha wanadiplomasia wabobezi watakao endeleza sifa nzuri ya chuo hicho nchini, kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi amesema chuo  hicho ni muhimu katika kutoa mafunzo ya uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza kuwa kwa sasa chuo kinaendelea kuboresha muundo wake na mitaala ili kukifanya kuwa bora zaidi.

“Mhe. Waziri kwa sasa tuna jukumu la kukibadilisha chuo chetu kuwa taasisi ya kitaaluma na kimkakati, hii ni moja kati ya hatua za utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu,” alisema Balozi Mwinyi.

Awali Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Felix Wandwe alisema chuo kinaendelea kuandaa miundo mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kuboresha mbinu za kuwanoa wanadiplomasia chuoni hapo.

Aidha, Dkt. Wandwe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kukilea chuo hicho na kukiwezesha kuzalisha wanadiplomasia wazalendo wanaopeperusha vyema bendera ya Tanzania kitaifa na kimataifa. 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Wangwe aiomba Serikali kukiwezesha chuo hicho kutatua changamoto ya wakufunzi wa masomo ya lugha za kigeni hususan Kireno na Kifaransa.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na watumishi wa Chuo cha Diplomasia (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muhongwa Mwinyi akizungumza  na watumishi wa Chuo cha Diplomasia (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam 

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na watumishi wa Chuo cha Diplomasia kikiendelea Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikabidhi vitabu kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muhongwa Mwinyi na Kaimu Mkuu wa CFR, Dkt. Felix Wandwe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikagua mradi wa ujezi wa madarasa ya kufundishia katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam



Tuesday, January 24, 2023

DKT. TAX AZUNGUMZA NA WATUMISHI WA APRM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekutana na kuzungumza na watumishi wa taasisi ya Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax amewahakikishia ushirikiano watumishi wa APRM na kuwasihi kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kutunza siri pamoja na kuweka maslahi ya taifa mbele.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haiko nyuma katika katika kusimamia masuala ya utawala bora, hivyo yote mliyonieleza hapa tutayafanyia kazi,” alisema Dkt. Tax

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Usimamizi la APRM, Prof. Hasa Mlawa ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na APRM na kuahidi kuwa APRM itaendelea kufanya kazi kwa bidii nyakati zote kwa maslahi mapana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kufanya kazi na taasisi yetu ya APRM, tunaahidi kutekeleza maelekezo yote kwa maslahi mapana ya taifa letu,” alisema Prof. Mlawa 

Awali Mtaalam Kiongozi wa APRM, Dkt. Rehema Twalib alisema kuwa tangu Tanzania ilipojiunga na APRM imetoa fursa kwa wananchi kuwasilisha maoni yao, kuweka wazi (transparency) taarifa za nchi pamoja na kusaidia kuimarishwa kwa huduma za kijamii.

Mtaalam Kiongozi wa APRM, Dkt. Rehema Twalib akiongea wakati wa kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na wafanyakazi wa APRM katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Usimamizi la APRM, Prof. Hasa Mlawa akielezea jambo katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na wafanyakazi wa APRM katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na watumishi wa taasisi ya Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na watumishi wa APRM kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Picha ya pamoja 



WATANZANIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA NCHI WANAZOISHI

Watanzania wametakiwa kuwa mabalozi wazuri katika nchi za ugenini kwa kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hizo ili kulinda taswira nzuri ya nchi yao.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Mtanzania, Bw. Nemes Tarimo aliyefariki dunia nchini Urusi.

Dkt. Tax amesema Bw. Tarimo alikwenda nchini humo mwaka 2020 kwa ajili ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Business Informatics. Akiwa masomoni mwezi Machi 2022 Bw. Tarimo alitiwa hatiani kwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba (7) jela.

Dkt. Tax amesema akiwa gerezani, Bw. Tarimo alijiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi cha Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya vita kumalizika na alifikwa na umauti akiwa katika uwanja wa vita tarehe 24 Oktoba, 2022.

"Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, si ruhusa kwa raia wake kujiunga na Jeshi la nchi yoyote duniani zaidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)," alisema Dkt. Tax

Dkt. Tax amesema kuwa mwili wa marehemu umeondoka nchini Urusi tarehe 24 Januari 2023 na unatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwasiliana na Serikali ya Urusi ili kuhakikisha mwili wa Marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi. 

Mhe. Waziri ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania kwa ujumla kufuatia msiba huo na ameiombea roho ya marehemu Tarimo ilazwe mahali pema peponi.

Mhe. Waziri ameahidi kwa umma na Diaspora wa Tanzania wakiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha kuwa usalama wao unazingatiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi


Thursday, January 19, 2023

DKT. TAX AWAHAKIKISHIA MABALOZI USHIRIKIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewahakikishia Mabalozi wanaowakilisha hapa nchini kuendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu katika vipindi vyao vya uwakilishi.

Hayo ameyasema tarehe 19 January 2023 alipokutana kwa nyakati tofauti kwa mazungumzo na mabalozi wa Canada, Finland, Norway na Japan.

Akizungumza na Balozi wa Canada nchini, Mhe. Kyle Nunas amemueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Canada katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa ambayo ni pamoja na: Ulinzi na usalama, teknolojia ya habari na mawasiliano, ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na maboresho yake, na kutafuta suluhu ya pamoja katika changamoto zinazoukumba ulimwengu ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, ugonjwa wa UVIKO-19 na usuluhishi wa migogoro.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting, viongozi hao walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, kilimo, uwekezaji, viwanda na biashara, ulinzi na usalama, mazingira na maliasili na maboresho katika mifumo ya kodi.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Waziri Tax amemueleza kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa kabla ya uhuru wa Tanganyika na kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo ya mazingira, ulinzi na usalama, kilimo, kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya uchumi na uongozi, biashara na uwekezaji, nishati na maboresho katika mifumo ya kodi.

Kuhusu kikao na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Misawa Yasushi, mazungumzo yao yalijikita katika kuimashirisha ushirikiano kwenye masuala ya utamaduni, sanaa na michezo, biashara na uwekezaji, kuwajengea uwezo wanawake na walemavu, ujenzi wa miundombinu, biashara na viwanda, ujenzi wa miundombinu, elimu, afya na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Aidha, wamejadili juu ya umuhimu wa ulimwengu kuendelea kushirikiana katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ugonjwa wa UVIKO-19 na magonjwa yasiyoambukiza na ulinzi na usalama.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Tax alitumia fursa hiyo ya mazungumzo kuwahamasisha Mabalozi hao kuweka mikakati ya kuhamia Dodoma ikiwemo kuanza ujenzi wa ofisi zao katika viwanja walivyokabidhiwa na Serikali ili kuweza kutekeleza majukumu kwa karibu zaidi .

“Serikali ya Awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejidhatiti katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, hivyo kupitia ushirikiano wa kidiplomasia uliopo tutaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha pande zetu zote zinanufaika na ushirikiano huo” alisema Waziri Tax.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting wakiwa katika picha ya pamoja. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Swahiba Mndeme (wapili kulia) Bi. Agness Kiama Afisa Mambo ya Nje (wa kwanza kulia) na Afisa wa Ubalozi (wa kwanza kushoto)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Norway nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini Mhe. Misawa Yasushi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Kyle Nunas yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas jijini Dodoma

VACANCY AND CONSULTANCIES ANNOUNCEMENT AT THE AFRICAN DEVELOPMENT BANK



 

Saturday, January 14, 2023

RAIS DKT. SAMIA AWAHAKIKISHIA MABALOZI USHIRIKIANO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao hapa nchini.

Mhe. Rais Dkt. Samia alitoa ahadi hiyo tarehe 13 Januari, 2023 katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, katika sherehe hizo Mhe. Dkt. Samia alisema licha ya changamoto za uviko 19 zilizoikumba Dunia kwa ujmla, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa himilivu. “mfano kwa mwaka 2022 pato la taifa limekua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 4.3 mwaka 2021, na kwa mwaka 2023 tunategemewa utaongezeka na kufikia asilimia 5,” alisema Dkt. Samia

Rais pia aliwaeleza Mabalozi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ambapo alisema kuwa kuanzia Julai mpaka Novemba 2022 Miradi imeongezeka na kufika 132 yenye thamani ya dola bilioni 3.16 za Marekani ambayo ni ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.

“Mfano mzuri waheshimiwa mabalozi, Serikali inatarajia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Nyerere mwezi Juni mwaka 2024 likiambatana na miradi mingine mikubwa” Dkt. Samia alibainisha

Kadhalika, Rais Dkt. Samia akatoa wito kwa mabalozi wanazowakilisha nchi zao kuungana na Serikali kuhamisha ofisi zao katika Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma.

“Mnafahamu kwamba Dodoma ndiyo makao makuu rasmi ya nchi yetu na Serikali imehamia huko na tunachukua kila hatua kuhakikisha linakuwa Jiji la kisasa lenye huduma zote muhimu. Tunawaomba mfanye mipango ya kuhamia Dodoma ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali ambazo Serikali inatoa kabla ya kumaliza wakati wake,” aliongeza Rais Dkt. Samia.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi zao kila wakati kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi na Mashirika mnayoyasimamia kila wakati kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax 

Kwa upande wake kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha inafikia malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiongea na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kaatika Sherehe za Mwaka Mpya 2023 kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu tarehe 13 Januari 2023 Jijini Dar es Salaam



Friday, January 13, 2023

MFUKO WA PAMOJA WA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA OMAN KUANZISHWA

Tanzania kwa kushirikiana na Oman zinatarajia kuanzisha Mfuko wa Pamoja wa Uwekezaji (Joint Investment Fund) mwaka huu (2023). Mfuko huo pamoja na mambo mengine, unategemewa kunufaisha sekta za uvuvi, kilimo na madini.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja kati ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mbarouk amesema kuanzishwa kwa mfuko huo wa pamoja wa uwekezaji ni utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu na kuongeza kuwa uanzishwaji wake utasaidia kuinua uchumi wa mataifa yote mawili. “kuanzishwa kwa mfuko huu ni utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wetu wakuu ambapo Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzishwa kwa mfuko huo ilisainiwa mwezi Juni mwaka 2022 kwa lengo la kuinua uchumi wa pande zote mbili na kwa maslahi mapana,” alisema balozi Mbarouk.

Mkataba huo ulisainiwa wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi nchini Oman mwaka 2022.

Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan amesema kwa sasa hatua zote zimekamilika na mwaka huu 2023 mfuko huo unategemea kuanzishwa rasmi na kusaidia kuinua biashara na uwekezaji kwa maslahi ya mataifa yote mawili. “mfuko huu utaanza rasmi mwaka huu 2023 na tunategemea uwasaidie kuichumi wafanyabishara na wawekezaji wa mataifa yetu mawili,” alisema Balozi Al Shidhan

Mwezi Juni mwaka 2022, Tanzania na Oman zilisaini Hati sita za Makubaliano katika sekta za nishati, utalii, maliasili, elimu ya juu, mafunzo ya ufundi stadi na makumbusho. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Kikao cha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na  Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan




Wednesday, January 11, 2023

BALOZI FATMA ATETA NA BALOZI WA ALGERIA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Januari 2023. 

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walijadili kuhusu masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Algeria kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal aliongea kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Algeria na Tanzania hususani diplomasia ya kimataifa, kukuza na kuimarisha biashara, uwekezaji na utalii baina ya nchi zetu mbili.

“katika mazungumzo yetu leo, tumekubaliana kuendelea kuimarisha diplomasia baina ya mataifa yetu kwa maslahi mapana ya nchi zetu na kwa maendeleo ya wananchi wetu,” amesema Balozi Djellal .

Balozi Fatma amesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Algeria katika sekta mbalimbali kama vile za nishati, elimu, afya na miundombinu kwa maendeleo ya mataifa yote mawili.

Algeria ilifungua Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1964 ikiwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua ubalozi hapa nchini. Mwaka 1981 nchi hizi mbili zilianzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo imechangia kuimarisha na kukuza ushirikiano wake na Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimsikiliza Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Januari 2023

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal baada ya kumaliza mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal baada ya kumaliza mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mambo ya Nje Wizarani Bi. Khadija Othman. 

Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Ahmed Djellal akiagana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



TANZANIA YAAINISHA VIPAUMBELE VYAKE KWA MABALOZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam hawapo pichani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam wanaonekana mbele katika picha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (hayupo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na  waheshimiwa Mabalozi kutoka nchi za Ulaya na Amerika wanaoziwakilisha nchi  zao hapa nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na wajumbe wa menejimenti wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na baadhi ya waheshimiwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanisha vipaumbele vyake vya mwaka 2023 kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Vipaombele hivyo vimeainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Januari, 2023.

“Misimamo ya Tanzania ni kuwa hatufungamani na upande wowote lakini pia Tanzania ni muumini wa uendelezaji wa ushirikiano wa kimataifa na kikanda. Tumeelezana vipaumbele vya Serikali hususani utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na kuona ni jinsi gani mabalozi wanaweza kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote,” alisema Dkt. Tax

Dkt. Tax aliongeza kuwa amesisitiza umuhimu wa maboresho yanayofanywa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuboresha shughuli za kiuchumi, ambapo Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na wameridhika na maboresho yanayofanywa na Serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za kipaumbele zaidi ambazo Tanzania imeziainisha.

Kwa upande wake kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed ameishukuru Serikali kwa kuainisha vipaumbele vyake kwa mwaka 2023 na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa inafika malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023.

“Kwa niaba ya Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa, napenda kuahidi kuwa tutaendelea kushirikiana na wizara na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha inafikia viapombele na malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023,” alisema Balozi El Badaoui Mohamed

Mkutano huo ulilenga kufahamiana, kukumbushana na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Tanzania katika masuala ya Diplomasia na mahusiano yake na nchi na taasisi mbalimbali kwa wana jumuiya hao wa kidiplomasia wanaowakilisha hapa nchini.