Thursday, January 19, 2023

DKT. TAX AWAHAKIKISHIA MABALOZI USHIRIKIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewahakikishia Mabalozi wanaowakilisha hapa nchini kuendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu katika vipindi vyao vya uwakilishi.

Hayo ameyasema tarehe 19 January 2023 alipokutana kwa nyakati tofauti kwa mazungumzo na mabalozi wa Canada, Finland, Norway na Japan.

Akizungumza na Balozi wa Canada nchini, Mhe. Kyle Nunas amemueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Canada katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa ambayo ni pamoja na: Ulinzi na usalama, teknolojia ya habari na mawasiliano, ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na maboresho yake, na kutafuta suluhu ya pamoja katika changamoto zinazoukumba ulimwengu ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, ugonjwa wa UVIKO-19 na usuluhishi wa migogoro.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting, viongozi hao walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, kilimo, uwekezaji, viwanda na biashara, ulinzi na usalama, mazingira na maliasili na maboresho katika mifumo ya kodi.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Waziri Tax amemueleza kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa kabla ya uhuru wa Tanganyika na kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo ya mazingira, ulinzi na usalama, kilimo, kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya uchumi na uongozi, biashara na uwekezaji, nishati na maboresho katika mifumo ya kodi.

Kuhusu kikao na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Misawa Yasushi, mazungumzo yao yalijikita katika kuimashirisha ushirikiano kwenye masuala ya utamaduni, sanaa na michezo, biashara na uwekezaji, kuwajengea uwezo wanawake na walemavu, ujenzi wa miundombinu, biashara na viwanda, ujenzi wa miundombinu, elimu, afya na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Aidha, wamejadili juu ya umuhimu wa ulimwengu kuendelea kushirikiana katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ugonjwa wa UVIKO-19 na magonjwa yasiyoambukiza na ulinzi na usalama.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Tax alitumia fursa hiyo ya mazungumzo kuwahamasisha Mabalozi hao kuweka mikakati ya kuhamia Dodoma ikiwemo kuanza ujenzi wa ofisi zao katika viwanja walivyokabidhiwa na Serikali ili kuweza kutekeleza majukumu kwa karibu zaidi .

“Serikali ya Awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejidhatiti katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, hivyo kupitia ushirikiano wa kidiplomasia uliopo tutaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha pande zetu zote zinanufaika na ushirikiano huo” alisema Waziri Tax.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting wakiwa katika picha ya pamoja. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Swahiba Mndeme (wapili kulia) Bi. Agness Kiama Afisa Mambo ya Nje (wa kwanza kulia) na Afisa wa Ubalozi (wa kwanza kushoto)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Norway nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini Mhe. Misawa Yasushi walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Kyle Nunas yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Mhe. Kyle Nunas jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.