Tuesday, January 31, 2023

UBALOZI WA UFARANSA WAFUNGUA OFISI NDOGO JIJINI DODOMA


Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipowasili eneo la Kilimani jijini Dodoma kwa ajili ya kufungua rasmi Ofisi ndogo ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa katika makao makuu tarehe 31 Januari 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui wakati nyimbo za Taifa za Tanzania na Ufaransa zikipigwa  alipowasili eneo la Kilimani jijini Dodoma kwa ajili ya kufungua rasmi Ofisi ndogo ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa katika makao makuu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na  Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui akizindua rasmi Ofisi ndogo ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa katika eneo la Kilimani jijini Dodoma 



Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui akizungmza wakati wa uzinduzi rasmi wa Ofisi ndogo ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa katika eneo la Kilimani jijini Dodomaakisikilizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rose Senyamule wa (kwanza kushoto) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa jijinii Dodoma 

Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa ofisii ya Uwakilishi ya Ubalozi wa ufaransa wakifuatilia tukio hilo

Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax baada ya kukamilika kwa hafla ya uzinduzi wa  Ofisi ndogo ya Uwakilishi ya Ubalozi wa Ufaransa jijini Dodoma  tarehe 31 Januari 2023

 




 


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) ameupongeza Ubalozi wa Ufaransa nchini kwa kufungua Ofisi Ndogo ya Uwakilishi jijini Dodoma na kuzihamasisha Balozi nyingine kuendelea kuitikia wito wa kuhamia Makao Makuu ya Nchi.

Akizungumza katika ufunguzi wa Ofisi hiyo, Mhe. Dkt. Tax amesema anaupongeza ubalozi huo kwa kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alioutoa mwanzoni mwa mwaka 2023 wa kuwasihi Mabalozi kuhamia Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma.

“Tuko hapa kwa ajili ya kufungua Ofisi ndogo za Uwakilishi za Ubalozi wa Ufaransa nchini, baada ya Serikali kuhamia rasmi Dodoma, ofisi hii ni ya tatu baada ya zile za Ujerumani na China, niwapongeze sana kwa uamuzi wenu huu, mmeiunga mkono Serikali katika kuhamia kwake hapa Dodoma’, alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax ameuhakikishia na kuuahidi Ubalozi huo kuwa, Serikali itatoa msaada wowote watakaouhitaji ili kuiwezesha ofisi hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha ndoto ya kuwa na ubalozi kamili inakamilika.

Amesema  hatua ya kufunguliwa kwa Ofisi hiyo ni muhimu katika kuimarisha uhusiano na urafiki uliopo baina ya Tanzania na Ufaransa  na kwamba ina dhamira ya kuupeleka uhusiano huo katika ngazi nyingine.

Ameeleza kuwa tayari Serikali imewapatia viwanja na hati Balozi zote na Taasisi za Kimatifa zenye uwakilishi nchini na kuongeza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika jiji la Dodoma ili kuhakikisha Jiji hili linakuwa na miundombinu na huduma bora za kijamii zinazotosheleza mahitaji ya wakazi wake wote.

Ameongeza kusema ana imani kuwa wito wa Serikali wa kuhamia makao makuu ya nchi utaenziwa na kuungwa mkono na Balozi na Mashirika ya Kimataifa na kuihakikishia jumuiya ya wanadiplomasia nchini kuwa Serikali itatoa msaada wowote utakaohitajika ili kurahisisha uhamiaji wao jijini Dodoma.

Naye Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Nabil Hajloui amesema Ufaransa imefungua Ofisi yake jijini Dodoma ikiwa ni hatua za kuunga mkono uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao Makuu yake jijini humo, lakini pia kurahisisha huduma mbalimbali za kibalozi kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani.

Amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uhusiano kwa manufaa ya pande zote mbili na kuahidi kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itaendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada zake za kuboresha na kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania kupitia Sekta za Maji, Nishati, Afya, Kilimo na Elimu kwa Tanzania Bara na Zanzibar

Kufunguliwa kwa Ofisi hizo kunafanya Dodoma kuwa na ofisi tatu za Ubalozi baada ya zile za Ujerumani na China. Ofisi hizo ambazo zipo eneo la Kilimani jijini Dodoma zitatoa huduma mbalimbali kwa Serikali na wananchi wote kwa ujumla na zinajumuisha pia Ofisi za Shirika la Msaada la Ufaransa la Agence Francaise de Development (AFD).

 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.