Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Mhe. Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 09
Januari 2023 amekutana kwa mazungumzo kwa nyakati tofauti na wageni mbalimbali
waliomtembelea ofisini kwake Mtumba
jijini Dodoma
Wageni hao ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui; Mwakilishi Mkazi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Mahoua
Parums; Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Bianadamu na Watu, Mhe. Jaji Iman
Aboud na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Watoto (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna.
Akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Dkt. Tax
amempongeza Mhe. Balozi Nabil Hajlaoui kwa hatua ya Ubalozi huo kufungua ofisi
jijini Dodoma ikiwa ni ishara ya Ufaransa katika kuuunga mkono harakati za Serikali
ya Tanzania za kuimarisha makao makuu ya nchi Dodoma.
“Mhe. Balozi nchi zetu zimekuwa na uhusiano wa kirafiki
uliodumu tangu Tanzania ilipopata uhuru wake, na tumeendelea kuungana mkono
katika ngazi ya nchi na hata kimataifa, na kwa hili mnalolifanya hapa Dodoma
linadhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wetu,” alisema Dkt. Tax
Akizungumza katika kikao hicho Balozi wa Ufaransa alisema
nchi yake imeamua kufungua ofisi ya ubalozi jijini Dodoma kama njia mojawapo ya
kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa pamoja kuunga mkono hatua ya
Serikali ya kuhamishia makao makuu yake jijini humo.
Ameongeza kusema mwezi Juni 2023 Ufaransa inatarajia
kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Paris hadi Dar es Salaam
kupitia Zanzibar. Itakumbukwa kuwa mwaka 2021 Shirika hilo lilianzisha safari
zake Zanzibar kupitia Nairobi, Kenya.
Amesema kuanzishwa kwa safari hizo za moja kwa moja
zitawawezesha watalii kutoka Ufaransa kuja moja kwa moja nchini na hivyo
kupunguza urefu wa safari na hivyo kufanya watalii na wafanybiashara wengi kuja
kuangalia fursa na kutembelea vivutio vya utalii nchini kwa urahisi.
Mhe. Balozi pia amesema Ubalozi pia utaendeloea kutoa
mafunzo ya lugha ya kifaransa kwa watumishi wa umma ambapo ikwa kuanzia
wanaendelea na mafunzo hayo kwa watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Ulinzi na katika Chuo cha Idara ya
Uhamiaji mjini Moshi.
Mhe. Balozi pia ameongelea nia ya nchi yake kuunganisha
nguvu na Tanzania katika sekta ya nishati mbadala ili kuiwezesha Tanzania
kujitosheleza na nishati hiyo nchini na hivyo kukuza uchumi wake.
Katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja
wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Mahoua Parums, Mhe. Dkt.
Tax amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika hilo katika zoezi
linaloendelea la kuwarejesha kwa hiari wakimbizi kwenye nchi zao za asili.
Kwa upande wake, Bi. Parums ameipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi licha ya changamoto mbalimbali
zilizopo. Amesema Shirika lake linathamini mchango huo wa kibinadamu wa
Tanzania kwa wakimbizi hao na kwamba litaendelea kushirikiana na Serikali
katika kuwarejesha kwa hiari wakimbizi wa Burundi.
Akizungumza na Mhe. Jaji Iman wa Mahakama ya Afrika ya
Haki za Bianadamu na Watu, Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali ya Tanzania kama
mwenyeji wa Mahakama hiyo iliyopo Arusha itaendelea kutekeleza makubaliano ya
mkataba wa uenyeji kama ulivyoainisha.
Naye Jaji Iman amemhakikishia ushirikiano Dkt. Tax na
kwamba wanaipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wa
uenyeji ambapo hadi sasa Mahakama hiyo
imepatiwa eneo la ukubwa wa ekari 25 kwa ajili ya kujenga ofisi zake za kudumu
jijini Arusha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNICEF nchini ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza kikamilifu mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayohusu masuala ya haki za watoto ikiwemo afya, elimu na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mhe. Dkt. Tax akiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Iman |
Sehemu ya ujumbe wa Mhe. Dkt. Tax ukifuatilia mazungumzo kati yake na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna |
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna akimpatia Mhe. Dkt. Tax maelezo ya zawadi ya picha kabla ya kumkabidhi |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.