TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Malkia wa Uholanzi Mhe. Maxima anatarajiwa
kuwasili nchini tarehe 11 Desemba, 2013 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Mhe. Maxima ambaye pia ni Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mfumo Jumuishi wa
Fedha katika Maendeleo atapokelewa na mwenyeji wake, Mke wa Rais, Mhe. Mama
Salma Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Baada
ya kuwasili, Mhe. Maxima atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam pamoja na
kushiriki katika Dhifa ya Kitaifa.
Aidha,
tarehe 12 Desemba 2013, Malkia Maxima atafanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Mhe. Mhandisi Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Saada
M. Salim na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu.
Siku
hiyo hiyo Mhe. Maxima atazindua rasmi Mfumo Jumuishi wa Fedha wa Taifa katika hafla
itakayofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Mfumo huo unalenga kuwanufaisha
Wanawake na Vijana, hususan katika kuchangia usalama wa chakula, kilimo na
maendeleo Vijijini.
Mhe. Maxima ataondoka Dar es Salaam tarehe 13 Desemba,
2013 kuelekea Dodoma ambako ataendelea na ziara yake kwa kutembelea mashamba ya
zabibu katika Kijiji cha Gawaye pamoja na kuzungumza na Wakulima. Mashamba hayo
yanasimamiwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Chakula Duniani (WFP), Shirika
la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo
(IFAD).
Mhe. Maxima anatarajiwa kuondoka nchini siku hiyo hiyo
jioni kurejea Uholanzi.
IMETOLEWA
NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR ES SALAAM.
10
DESEMBA, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.