Tuesday, January 26, 2021

RAIS WA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA SHIRIKISHO LA ETHIOPIA AHITIMISHA ZAIRA YAKE YA SIKU MOJA NCHINI


Mheshimiwa Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia leo tarehe 25 Januari, 2021 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini ambapo amepokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja wa ndege wa Chato, uliopo mkoani Geita. 
 
Baada ya mapokezi ya kitaifa Mhe. Zewde na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Mgufuli waliambatana kwenda kuendelea na ratiba ya mazungumzo baina yao, na baadaye wote kwa pamoja walijitokeza kuelezea umma wa Watanzania kupitia waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyojili na kukubaliana katika mazungumzo hayo.

Rais Magufuli kwa upande wake ameelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali kupitia ushirikiano na uhusiano mzuri uliodumu kwa muda mrefu  baina ya Nchi hizi mbili ikiwemo katika sekta ya biashara na uwekezaji. Mhe. Rais ameeleza kuwa kwa miaka ya hivi karibuni biashara kati ya Tanzania na Ethiopia imeendelea kuimarika madhalani, kwa mwaka 2016 biashara ilikuwa bilioni 3.07 na kufikia bilioni 13.55 kwa mwaka 2019/2020. Vilevile miradi 13 yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 14.57 kutoka nchini Ethiopia zimesajiliwa nchini kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amebainisha maeneo mengine ambayo Taifa litanufaika kutokana na ziara iliyofanywa na Rais Zewde wa Ethiopia nchini, kama vile;  fursa ya kufundisha kiswahili nchini Ethiopia, fursa ya mafunzo katika sekta ya usafiri wa anga ikiwemo urubani na ufundi wa ndege na fursa ya uwekezaji katika sekta ya viwanda vya kuzalisha bidhaa za ngozi nchini. Sambamba na hilo Rais Magufuli ameeleza kuwa amemweleza Rais Zewde kuhusu utayari wa Serikali wa kuwaachia huru wafungwa zaidi ya 1700 raia wa Ethiopia wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kuingia nchini kinyume na taratibu.

Kwa upande wake Rais Zewde ameeleza kuwa Tanzania ni rafiki wa wakati wote wa Ethiopia na ni nchi muhimu Kijiografia ambayo ni lango la kuingilia kanda na nchi zingine za Afrika. "Ethiopia inatambua mchango na ushawishi wa Tanzania hasa katika kutetea masalahi ya Afrika kwenye majukwaa mbalimbali ya Kimataifa" amesema Rais Zewde.  Rais Zewde amesema pamoja na mambo mengine ziara yake ililenga kuja kutoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuchaguliwa na kuaminiwa kwa mara nyingine na Watanzania kuiongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uchaguzi huru na wawazi. Aidha, Rais Zewde ameleeza utayari wake wa kukifanya kiswahili kuwa moja kati ya lugha nying zinazo zungumzwa nchini Ethiopia. 

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na hadhira iliyojitokeza kwenye mapokezi ya Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia mara baada ya kuhitimisha mazungumzo na Rais huyo. 

Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia akizungumza na hadhira iliyojitokeza na kushiriki katika mapokezi yake wakati akiwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Serikali ya Tanzania na Ethiopia
Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia akiwaaga Watanzania wakati anarejea nchini Ethiopia mara baada ya kuhitimisha ziara ya kikazi ya siku moja nchini.

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifurahia jambo wakati wa kumhaga Rais Zewde baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi nchini. 

Kwa Heri, Rais Zewde karibu tena wakati mwingine nchini Tanzania

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia wakikagua gwaride punde baada ya Rais Zewde kuwasili nchini.

Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia akipiga ngoma kwenye hafla ya mapokezi ya kumkaribisha alipowasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja
 
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mheshimiwa Sahle-Work Zewde Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia alipowasili njini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.