WIZARA IMEJIPANGA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI: WAZIRI MEMBE
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sasa imejipanga katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi hususan katika kukuza biashara, kuhamasisha uwekezaji na kuvutia watalii kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Hayo yalisemwa na Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam alipozungumza na Waandishi wa Habari kuwaeleza mafanikio ya Wizara yake yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo maadhimisho yatafikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014.
Mhe. Membe alisema kuwa mara baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 Sera ya Mambo ya Nje ilijikita katika masuala ya ulinzi na usalama na pia ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo viongozi wengi kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika zikiwemo Namibia, Angola, Msumbiji na nyingine walitumia ardhi ya Tanzania katika kupigania uhuru wa mataifa yao.
Aliongeza kuwa, tangu kipindi hicho cha harakati za ukombozi hadi sasa Tanzania imeweka historia duniani katika utatuzi wa migogoro na ulinzi wa amani ambapo imekuwa mstari wa mbele kwenye kuchangia Vikosi vya kulinda amani katika nchi mbalimbali zinazokabiliwa na migogoro ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Comoro, Sudan (Darfur) na Lebanon.
“Katika kudumisha amani, vyombo vyetu vimevuka mipaka kisheria ili kuhakikisha amani inapatikana, hivyo ninatoa pongezi kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi nzuri ya ulinzi wa amani”, alisema Mhe. Membe.
Mhe. Membe aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara inakwenda vizuri katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ambapo kwa kushirikiana na Wizara, Idara na Taasisi nyingine imekuwa mstari wa mbele kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara wenye vigezo na sifa ambao wana nia ya kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo gesi. “Wizara inajitahidi kwenda duniani kutafuta wawekezaji, kwani ni kipindi cha kufanya hivyo, na wale wenye sifa na vigezo tunavyovihitaji watachukuliwa”, alisisitiza Mhe. Membe.
Aidha, Mhe. Membe alieleza kuwa, kutokana na hali ya amani na utulivu hapa nchini pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Uchukuzi, Utalii utaendelea kuongezeka.
Katika hatua nyingine, Mhe. Membe alisema kwamba ili kukuza vipaji vya michezo kwa vijana hapa nchini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inahamasisha Diplomasia ya Michezo kwa kuzishirikisha nchi marafiki katika kuchangia sekta hiyo kiufundi, kitaaluma, vifaa na masuala mengine yanayohusu sekta hiyo.
Alifafanua kuwa, kwa sasa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la sehemu za kufanyia mazoezi zenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya kuwawezesha wanamichezo kufanya mazoezi kabla ya kwenda kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Aidha, aliongeza kuwa kwa jitihada za Wizara nchi nne ambazo ni Uturuki, Ethiopia, China na New Zealand zimekubali kuwapokea wanamichezo 50 na Walimu wao kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kwa ajili ya kwenda kujifua tayari kwa kushiriki mashindano ya michezo ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Glasgow, Uingereza mwezi Jalai 2014.
“Kutokana na Tanzania kukosa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya mazoezi na ili kuwawezesha vijana wetu kufanya vizuri michezoni, Wizara ilianza kutafuta maeneo nje ya nchi kwa ajili ya mazoezi ambapo tayari nchi za Ethiopia, New Zealand, China na Uturuki zimekubali tupeleke vijana 50 kwa ajili ya mazoezi, nchi tatu kati ya hizo zitapokea vijana kumi kila moja na China itapokea vijana 20”. Alisisitiza Mhe. Membe.
Mhe. Membe alieleza kuwa ana imani mkakati huu utasaidia Tanzania kuanza kupata medali na pia utaamsha ari ya vijana kupenda na kushiriki michezo kikamilifu.
Wakati wa mkutano huo, Mhe. Membe pia alitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo Mgogoro wa Mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi ambapo alisema, baada ya kukutana na Jopo la Usuluhishi chini ya Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano hivi karibuni, nchi hizo mbili zimeachwa ziangalie faida na hasara za mpaka kupita katikati au pembezoni mwa Ziwa hilo. Hiki ni kikao cha kwanza cha usuluhishi ambapo pande mbili zilikutana ana kwa ana. Aidha, baada ya uchaguzi mkuu nchini Malawi mwezi Mei mwaka huu, kikao kingine kitapangwa.
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Mhe. Membe alisema kwamba Tanzania haina ugomvi na Rwanda na kwamba tatizo lililopo ni kutokuaminiana kunakotokana na mashitaka na madai ya uongo yanayotolewa na watu wasiozitakia mema nchi hizi. Hivyo alieleza kuwa Tanzania inaamini katika majadiliano ya amani na diplomasia ili kuweza kutatua tatizo hili.
Vile vile, Mhe. Membe alitumia fursa hiyo pia kuwaasa Watanzania wanaopata fursa ya kusafiri au kuishi nje ya nchi kujiepusha kufanya makosa ya jinai kwa kufuata sheria na taratibu za nchi wanazokwenda. Mhe. Membe aliyasema hayo kufuatia taarifa alizopokea wakati wa ziara yake nchini China hivi karibuni kuhusu vijana wadogo wa kike kutoka Tanzania wanajihusisha na biashara haramu ya ukahaba huko Guangzhou, China.
“Tuna Watanzania wapatao milioni tatu wanaoishi vizuri nje ya nchi, hata hivyo wapo wachache wanaofanya mambo mabaya kama ugaidi, ukahaba na biashara za madawa ya kulevya. Nawaomba sana Watanzania wanapokuwa nje waishi kulingana na sheria na taratibu za nchi hizo ili kujilindia heshima na utu na pia heshima ya nchi yetu”, alisisitiza Mhe. Membe.
-Mwisho-