Mazungumzo yakiendelea
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO
WA KATIBU MKUU, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA WAANDISHI
WA HABARI KUHUSU ZIARA YA MHE. LI YUANCHAO, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA WATU
WA CHINA, NCHINI TANZANIA, DAR ES SALAAM
TAREHE
18 JUNI, 2014
· Wakurugenzi wa Idara
na Wakuu wa Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje,
· Ndugu waandishi wa
Habari wa vyombo vya habari vya umma na binafsi,
· Mabibi na Mabwana,
Ndugu
Waandishi,
Tumekutana
hapa leo kwa lengo la kufahamishana kwa muhtasari kuhusu ziara ya Mheshimiwa, Li
Yuanchao, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, nchini. Makamu
huyo wa Rais wa China, anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe 21
hadi 26 Juni 2014. Lengo la ziara hiyo, ni kuimarisha mahusiano ya karibu na ya
kidugu kati ya nchi hizi mbili ambayo mwaka huu yamefikisha miaka hamsini tangu
kuasisiwa rasmi mwaka 1964.
Ndugu
Waandishi,
Mheshimiwa
Li Yuanchao atawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
tarehe 21 Juni 2014 amnapo atatembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoa wa
Arusha hususan Bonde la Ngorongoro tarehe 22 Juni 2014 na jioni atawasili
jijini Dar es Salaam kuendelea na ziara yake hiyo.
Ndugu
Waandishi,
Kama
mnavyofahamu, ziara hii inakuja wakati muafaka ambapo tunaelekea katika kilele
cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na
Tanzania. Kadhalika, huu ni mwendelezo wa ziara mbalimbali zinazofanywa na
Viongozi wa ngazi za juu wa pande zote mbili ambazo zimekuwa ni chachu katika
kufikiwa kwa makubaliano mbalimbali hususan ya kiuchumi kwa manufaa ya pande
zote mbili.
Ndugu
Waandishi,
Akiwa
jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Li Yuanchao, atakutana na kufanya mazungumzo
na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa kati ya tarehe 23 na 26 Juni 2014 pamoja na
kufungua Jukwaa la Kiuchumi kati ya Tanzania na China. Miongoni mwa Viongozi atakaokutana
nao ni Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mwenyeji wake Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile,
Mheshimiwa Li Yuanchao atatembelea Zanzibar tarehe 25 Juni 2014 ambapo atakutana
na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Balozi Seif Idi, Makamu wa Pili wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na kurejea Dar es Salaam tarehe 26 Juni 2014 tayari
kwa safari ya kuelekea nchini China.
Ndugu
Waandishi,
Ikumbukwe
kuwa, Tanzania na China si tu zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja mbalimbali
za kiuchumi na kisiasa lakini wamekuwa ni marafiki wakati wa shida na wa raha. Hili
linadhihirishwa na mikataba takribani 17 ambayo nchi hizi mbili zilikubaliana
mwezi Machi 2013 wakati wa ziara ya Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China nchini.
Hivyo,
mazungumzo kati ya Mheshimiwa Li Yuanchao na viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa
yatajikita zaidi katika kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo wa kiuchumi,
kisiasa na kijamii kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuibua maeneo mapya ya
ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.
Ndugu
Waandishi,
Ni
matumaini yangu mimi binafsi, Wizara pamoja na Serikali kwa ujumla kwamba wakati
wote Mheshimiwa Li Yuanchao atakapokuwa nchini tutapata ushirikiano wa kutosha
kutoka kwenu na wadau wengine.
Itoshe tu kusema
kwamba Tanzania na China zitaendelea kufanya juhudi za pamoja katika kuimarisha
ushirikiano wa kirafiki, katika sekta mbalimbali, na kuhimiza uhusiano na
ushirikiano wa kiuchumi ili kunufaisha pande zote mbili.
Mwisho
Ndugu
Waandishi wa Habari, napenda kunukuu kauli ya Mwalimu Nyerere, Mwasisi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwamba katika huu Ulimwengu tumekuwa na marafiki wengi sana lakini
rafiki mmoja wa kweli ni Jamhuri ya Watu wa China.
……Ahsanteni Sana…
WIZARA YA MAMBO YA
NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Juni
2014
Dar es Salaam.
|