Tuesday, June 17, 2014

Balozi wa China nchini, Lu Youqing akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya watu wa China Li Yuanchao.

Balozi wa China nchini,Lu Youqing (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Watu wa China Mhe. Li Yuanchao katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini China ,Luteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo .

Balozi wa China nchini,Lu Youqing(kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Watu wa China Mhe. Li Yuanchao katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini China ,Luteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo na wakwanza kutoka kushoto ni  Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australia kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiruikiano wa Kimataifa Balozi Mbelwa Kairuki.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Balozi wa China nchini,Lu Youqing (hayupo pichani).

Mazungumzo yakiendelea


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA KATIBU MKUU, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU ZIARA YA MHE. LI YUANCHAO, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, NCHINI TANZANIA, DAR ES SALAAM
TAREHE 18 JUNI, 2014


·       Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje,
·       Ndugu waandishi wa Habari wa vyombo vya habari vya umma na binafsi,
·       Mabibi na Mabwana,

Ndugu Waandishi,
Tumekutana hapa leo kwa lengo la kufahamishana kwa muhtasari kuhusu ziara ya Mheshimiwa, Li Yuanchao, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, nchini. Makamu huyo wa Rais wa China, anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe 21 hadi 26 Juni 2014. Lengo la ziara hiyo, ni kuimarisha mahusiano ya karibu na ya kidugu kati ya nchi hizi mbili ambayo mwaka huu yamefikisha miaka hamsini tangu kuasisiwa rasmi mwaka 1964.



Ndugu Waandishi,
Mheshimiwa Li Yuanchao atawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro tarehe 21 Juni 2014 amnapo atatembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoa wa Arusha hususan Bonde la Ngorongoro tarehe 22 Juni 2014 na jioni atawasili jijini Dar es Salaam kuendelea na ziara yake hiyo.

Ndugu Waandishi,
Kama mnavyofahamu, ziara hii inakuja wakati muafaka ambapo tunaelekea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania. Kadhalika, huu ni mwendelezo wa ziara mbalimbali zinazofanywa na Viongozi wa ngazi za juu wa pande zote mbili ambazo zimekuwa ni chachu katika kufikiwa kwa makubaliano mbalimbali hususan ya kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Ndugu Waandishi,
Akiwa jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Li Yuanchao, atakutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa kati ya tarehe 23 na 26 Juni 2014 pamoja na kufungua Jukwaa la Kiuchumi kati ya Tanzania na China. Miongoni mwa Viongozi atakaokutana nao ni Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyeji wake Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vilevile, Mheshimiwa Li Yuanchao atatembelea Zanzibar tarehe 25 Juni 2014 ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Balozi Seif Idi, Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kurejea Dar es Salaam tarehe 26 Juni 2014 tayari kwa safari ya kuelekea nchini China.

Ndugu Waandishi,
Ikumbukwe kuwa, Tanzania na China si tu zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa lakini wamekuwa ni marafiki wakati wa shida na wa raha. Hili linadhihirishwa na mikataba takribani 17 ambayo nchi hizi mbili zilikubaliana mwezi Machi 2013 wakati wa ziara ya Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China nchini.

Hivyo, mazungumzo kati ya Mheshimiwa Li Yuanchao na viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa yatajikita zaidi katika kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.





Ndugu Waandishi,
Ni matumaini yangu mimi binafsi, Wizara pamoja na Serikali kwa ujumla kwamba wakati wote Mheshimiwa Li Yuanchao atakapokuwa nchini tutapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwenu na wadau wengine.

Itoshe tu kusema kwamba Tanzania na China zitaendelea kufanya juhudi za pamoja katika kuimarisha ushirikiano wa kirafiki, katika sekta mbalimbali, na kuhimiza uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi ili kunufaisha pande zote mbili.

Mwisho Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kunukuu kauli ya Mwalimu Nyerere, Mwasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba katika huu Ulimwengu tumekuwa na marafiki wengi sana lakini rafiki mmoja wa kweli ni Jamhuri ya Watu wa China.


……Ahsanteni Sana…


WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Juni 2014                                       Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.