Tuesday, June 10, 2014

Waziri Membe kushiriki Mkutano kuhusu Ukomeshaji Udhalilishaji wa Kijinsia mjini London

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Uingereza imemwalika Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ukomeshwaji wa Udhalilishaji wa Kijinsia kwenye Maeneo yenye Migogoro (“End Sexual Violence in Conflict”) utakaofanyika mjini London, Uingereza kuanzia tarehe 10 hadi13 Juni, 2014.

Mwaliko huo unakuja kufuatia mchango mkubwa wa Tanzania katika kufanikisha kuwepo kwa Tamko la Umoja wa Mataifa linalohusu suala hilo (Declaration of Commitment to End Sexual Violence in Conflict).Vile vile itakumbukwa kuwa, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia vikosi vya kulinda amani katika maeneo yenye migogoro Barani Afrika ambayo pia yana wahanga wengi wa udhalilishwaji wa kijinsia.

Pamoja na masuala mengine, Mkutano huo utajadili hatua za kuchukua ili kumaliza tatizo la udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro; mchango au nafasi ya vijana katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro; kiwango cha udhalilishaji wa kijinsia unatokea katika maeneo yenye migogoro na kuweka makubaliano ya kimataifa ya namna ya kutekeleza  mikakati iliyomo katika maazimio ya G8 na Umoja wa Mataifa; na kusikia matatizo na athari za udhalilishaji wa kijinsia katika migogoro moja kwa moja kutoka kwa Wahanga.

Pia washiriki watajadili changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na udhaifu unaotokana na kutoadhibiwa kwa wanaofanya vitendo hivyo.
Mkutano huo utazikutanisha nchi zilizoathiriwa na migogoro, nchi wahisani, Umoja wa Mataifa, Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi za Kijamii na wadau wengine.

Aidha, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Membe atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Mark Simmonds. Miongoni mwa masuala watakayozungumza ni kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza.

IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
10 JUNI, 2014

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.