Mwishoni
mwa wiki, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilijadili ajenda ya Afya na Sera ya
Mambo ya Nje ambapo pamoja na mambo mengine lilipitisha azimio linalotathmini
utayari wa nchi wanachama kukabiliana na magonjwa ya milipuko na dharura
nyingine za kiafya.
Katika
mjadala huo, wazungumzaji wengi walisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo
ya afya, hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati zisizo na uwezo wa
kutosha wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Aidha, walieleza umuhimu wa
kung’amua mafunzo muhimu ya janga la ugonjwa wa Ebola uliosababisha maafa makubwa
katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Akichangia
katika mjadala huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Bw. Noel Kaganda, Afisa
Mwandamizi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa alibainisha kuwa pamoja na jitihada zilizolenga kuimarisha
sekta ya afya katika kipindi kilichomalizika cha utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama
vile upungufu wa madaktari na wauguzi; vifaa finyu na vichakavu; na mazingira yasiyo
salama.
Alisisitiza
kuwa, jitihada za kuboresha afya ya binadamu, hususan ya akina mama na watoto,
lazima ziendelezwe kwa ufanisi zaidi katika muktadha wa Agenda ya Maendeleo
Endelevu hadi kufikia mwaka 2030.
Aliongeza
kuwa pamoja na kuzuia vifo vya watoto wachanga, ambavyo idadi yake ulimwenguni
kwa mwaka 2015 imefikia milioni 6, sawa na vifo 16,000, jumuiya ya kimataifa
haina budi kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya
milipuko kama vile Ebola na mengineyo, ambayo yanaweza kuathiri jamii nyingi
duniani kufuatia kushamiri kwa utandawazi na uharibifu wa mazingira
unaosababishwa na binadamu.
Pamoja
na kusisitiza kuwa wananchi wote wapatiwe huduma bora za afya, Tanzania iliunga
mkono mapendekezo ya ripoti ya wa Shirika la Afya Duniani kuhusu ulinzi na
ustawi wa watumishi katika sekta ya afya.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, watumishi wengi wa sekta ya afya wanazalilishwa na
kushambuliwa wakiwa kazini na wanaathirika na majanga mengine kama vile Tsunami
na matetemeko ya ardhi. Tanzania ilisema kuwa vitendo hivyo vinachangia katika
kuzorota kwa sekta ya afya, hivyo ilitaka vikomeshwe mara moja. Pia ilipendekeza
wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria katika ngazi ya kitaifa na
kimataifa.
Vilevile
ilitaka watumishi wa sekta ya afya wapatiwe mafunzo na zana za kujilinda na
maambukizi, ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kadhalika ilisisitiza
umuhimu wa mashirikiano baina ya nchi wanachama na wadau wengine wa afya, kama
vile Shirika la Afya Duniani, yenye lengo la kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo
wa kukabiliana na dharura za kiafya.
Taarifa
ya Shirika la Afya Duniani imekuja siku chache kabla ya jopo la Ngazi ya Juu
lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupendekeza namna bora ya
kukabiliana na magonjwa ya milipuko duniani. Jopo hilo linaloongozwa na Rais
Mstaafu wa awamu ya nne, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, linatarajia kuwasilisha taarifa yake mwezi Januari 2016.
Katika
hatua nyingine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeazimia kufanya mkutano wa
ngazi ya juu kuhusu “antimicrobial resistance - AMR” kwa lengo la kubaini kiini
cha magonjwa sugu kama kama ilivyo kwa baadhi ya jamii za ugonjwa wa Kifua
Kikuu.
=Mwisho=