Friday, December 25, 2015

Waziri Mahiga awasilisha ujumbe maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Rais Nkurunziza

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Rajabu Gamaha mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum wa Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini humo.
Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza akimkaribisha Waziri Mahiga alipowasili kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum kwake. Pembeni ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Gamaha.
Waziri Mahiga akimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Spika, Mhe. Aghaton Rwasa alipokutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Burundi, Mhe.Paschal Nyabenda (aliyekaa kushoto kwa Waziri Mahiga)

==================================== 



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi kwenye Ikulu yake jijini Bujumbura, Burundi kufuatia maagizo ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki ikiwa ni hatua ya Tanzania kutafuta suluhu ya kisiasa ya migogoro iliyojitokeza baina ya Serikali na vikundi vinavyo hatarisha amani nchini humo.
Kwenye mazungumzo yao yaliyodumu takriban saa mbili, Mhe. Mahiga alimueleza Rais Nkurunziza azma ya Rais Magufuli kuamsha mazungumzo ya kisiasa ya kuleta amani na kwamba tayari msuluhishi aliyeteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Kaguta  Museveni ameanza maandalizi ya uzinduzi wa mazungumzo hayo yatakayofanyika Entebe, Uganda tarehe 28 Desemba 2015. Waziri Mahiga pia alieleza maoni yake kuhusu hali ya utulivu aliyoiona kwa kipindi cha takriban saa 24 alizokuwa Jjijini Bujumbura na kwamba hakusikia sauti za milipuko wala silaha zozote.
Mhe. Nkurunziza alimshukuru mjumbe huyo wa Rais Magufuli na kumhakikishia ushiriki wa Burundi akieleza kuwa mazungumzo ya Entebe yatasaidia kuleta amani na mshikamano baina ya wananchi wa Burundi. Hata hivyo Mhe. Nkurunziza alisisitiza kuwa ili mazungumzo hayo yawe na tija ni lazima yawe muendelezo wa mazungumzo ya ndani ambayo yeye na Serikali yake wamekwisha yaanza. Aliongeza kuwa ni matumaini yake kuwa makundi yote nchini humo wataungana kwenye mazungumzo hayo yatakayojumuisha asasi za kiraia, kidini, vyama vya siasa na makundi mengine ili kujadili mustakabali wa taifa lao kwa pamoja.
Pamoja na kuridhia ushiriki wa Burundi kwenye mchakato huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Nkurunziza alieleza kuwa yeye na Serikali yake wako tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kutathmini hali ya usalama nchini mwake.  Hivi karibuni Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilitangaza kupeleka vikosi vya askari elfu tano nchini Burundi kufuatia kile kilichodaiwa kuwa viashiria vya mauaji ya kimbari kama yale yaliyofanyika nchini Rwanda miaka ya tisini.
Rais Nkurunziza alisema uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umewashtua wao Serikalini na hata Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wanaohoji sababu za umoja huo kupeleka jeshi kubwa nchini humo. Burundi imekuwa ikishirikiana na Umoja wa Afrika kwenye ulinzi wa amani ambapo ina vikosi vya askari zaidi ya elfu sita nchini Somalia na Afrika ya Kati.
Naye Spika wa Bunge la Burundi Mhe. Paschal Nyabenda alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo wa Umoja wa Afrika. Mhe. Nyabenda ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD nchini humo alimweleza Mhe. Mahiga kuwa misingi ya kukataa ukabila imeainishwa kwenye katiba ya nchi hiyo na makubaliano ya Arusha ambapo inalazimisha taasisi zote ziwe na uwakilishi na pengine uwiano sawa kati ya Wahutu na Watusi. Akielezea muundo wa Bunge lake ambalo lina asilimia 60 kwa 40 ya uwakilishi wa Wahutu na Watusi Mhe. Nyabenda alisema kuwa Makamu wa Kwanza wa Spika Mhe. Agathon Rwasa anatoka kwenye kabila la Wahutu na Makamu wa Pili wa Spika, Mhe. Edouard Nduwimana anatokea kwenye kabila la Watusi.
Naibu Spika wa Kwanza wa Bunge hilo Mhe. Agathon Rwasa ambaye pia alishiriki kwenye mazungumzo hayo alisema kuwa wakati umefika sasa kwa Burundi kuangalia mbele na kwa manufaa na maendeleo ya vizazi vijavyo. Alisifu maendeleo aliyoyashuhudia nchini Tanzania ambapo alisisitiza yamekuwepo kutokana na amani nchini humo.
Akiwa nchini Burundi, Mhe. Mahiga na ujumbe wake walikutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Usalama wa Raia na Mambo ya Ndani ambapo alipokea taarifa ya Waziri Mhe. Alain Guillaume Bunyoni kuhusu hali ya usalama nchini humo tangu Rais Nkurunziza alipochaguliwa na chama chake kugombea tena nafasi ya Urais mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa upande wake Waziri Mahiga alisifia jitihada zilizowekwa na Wizara hiyo hususan kwenye upande wa ulinzi wa raia na mali zao na kusisitiza umuhimu wa Wizara hiyo na Serikali nzima kuwaelezea wananchi na jumuiya za Kimataifa kwa ujumla jitihada za Serikali kuleta amani nchini humo.
Ziara ya siku mbili ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania ilianzia Entebe, nchini Uganda ambapo Mhe. Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Mhe. Dkt Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye ameanza maandalizi ya mazungumzo ya amani chini ya uenyekiti wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
25 Desemba, 2015
                                                                                     




 

Wednesday, December 23, 2015

Taarifa kwa Vyombo vya Habari




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHE. DKT.AUGUSTINE MAHIGA NCHINI BURUNDI NA UGANDA
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augistine Mahiga (Mb), atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika nchi za Uganda na Burundi kuanzia tarehe 23 Desemba, 2015.

Ziara hiyo ya Mhe. Mahiga inafanyika kufuatia maelekezo ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kumtaka kwenda kufuatilia hali nchini humo ili kuiwezesha Jumuiya kushughulikia mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini Burundi.

Akiwa Uganda, 2015, Mhe. Mahiga atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye anaendelea na jukumu  la usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa wa Burundi kwa niaba ya Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda.

Aidha, Mhe. Waziri atakutana na Mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Burundi, Ndg. Jamal Benomar.

Mhe. Waziri atasafiri siku hiyo hiyo kuelekea Bujumbura, Burundi ambapo atakutana na wadau mbalimbali wa mgogoro huo kabla ya kukutana na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi. Mhe. Waziri atarejea Dar es Salaam tarehe 24 Desemba, 2015 baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam
23 Desemba, 2015

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na  Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga akizungumza kwa mara ya kwanza kwenye mkutano uliomkutanisha na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa nchini. Mkutano huo ulikuwa na lengo la Waziri kujitambulisha ambapo pia alitoa taarifa mbalimbali ikiwemo umuhimu wa ushirikiano wa Tanzania na nchini mbalimbali; hali ya kisiasa huko Zanzibar baada ya uchaguzi na mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi.
Sehemu ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao, wa kwanza kushoto ni Balozi wa Rwanda nchini, Mhe. Eugene Segore Kayihura (wa kwanza kushoto), Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Mark Children (wa pili kutoka kushoto), Balozi wa Oman nchini Mhe. Soud Al Mohammed Al-Ruqaish
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini nao wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya Mabalozi na Makaimu Balozi waliohudhuria mkutano huo. Balozi wa China nchini Mhe. Lu Youqing (wa pili kutoka kulia kwenye mstari wa pili), Naibu Balozi wa Misri, Bw. Moataz Kareem Elbahnasawi (wa kwanza kulia mstari wa mbele).
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Dkt. Suzan Kolimba naye alipata fursa ya kujitambulisha kwa Mabalozi na Wakuu hao wa Mashirika.
Sehemu nyingine ya Mabalozi wakimsikiliza Naibu Waziri Kolimba (hayupo pichani) alipokuwa akijitambulisha kwao. 
Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki, Mhe. Joyce Mapunjo na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika nao wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga (hayupo pichani). 
Sehemu ya Wakurugenzi wa iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bi. Amisa Mwakawago na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bw. Abdallah Mtibora
Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Bi. Mindi Kasiga akizungumza
Sehemu ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka iliyokuwa Wizara ya Afrika Mashariki
Waziri Mahiga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya  mazungumzo na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa, na Wakuu wa Mashariki ya Kimataifa nchini.
Waziri Mahiga (kushoto) akisalimiana na Naibu Balozi wa Misri, Bw. Moataz Kareem Elbahnasawi (katikati) na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Itifaki, Bw. James Bwana
Naibu Waziri akisalimiana na Balozi wa Demokrasia ya Kongo Mhe.Halfan Juma Mpango
Waziri Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa nchini 

Picha ya pamoja



Tuesday, December 22, 2015

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akimkaribisha Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Dkt. Lu Youqing  alipofika Wizarani kwa ajili ya kumpongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa huo mpya na pia kuzungumzia masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na China. Pembeni ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki.
Balozi Lu Youqing akizungumza na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu mwenendo wa ushirikiano kati ya Tanzania na China ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa nchini kwa ushirikiano na China.
Balozi Mbelwa na Bw. Thobias Makoba, Msaidizi wa Waziri wakifuatilia mazungungumzo kati ya Mhe. Dkt. Mahiga na Balozi Lu (hawapo pichani)
Sehemu ya ujumbe kutoka Ubalozi wa China wakifuatilia mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea
Picha ya pamoja

Monday, December 21, 2015

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi Wateule wa Korea na EU nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea nchini, Mhe. Song Geum-young. Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 21 Desemba, 2015.
Mhe. Dkt. Mahiga akiwa kwenye mazungumzo na Balozi Song Geum-young mara baada ya kupokea nakala za hati za utambulisho.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) akiwa na Bw. Thobias Makoba (kulia), Msaidizi wa Waziri  pamoja na Bw. Khatib Makenga (katikati), Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Song Geum-young (hawapo pichani)
Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. James Bwana akimpatia utaratibu  Balozi Song Geum-young kabla ya kuwasilisha Nakala zake za Utambulisho kwa Mhe. Waziri

 .......Nakala za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa EU

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akimkaribisha  Balozi Mteule wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Mhe. Roeland Van De Geer alipofika Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Mhe. Waziri. Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 21 Desemba, 2015.
Mhe. Dkt. Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa  Balozi Mteule wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Mhe. Roeland Van De Geer.
Mhe. Dkt. Mahiga akizungumza na Balozi Mteule wa EU, Mhe. Roeland Van De Geer
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Joseph Sokoine akiwa na Bi. Felister Rugambwa wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Mahiga na Balozi Roeland Van De Geer  (hawapo pichani)