Wednesday, January 31, 2018

Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Korea Kusini


Mheshimiwa Augustine Phillip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akilakiwa na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mazungumzo ya kikazi tarehe 31 Januari 2018. 


Mheshimiwa Augustine Mahiga na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa wakiwa kwenye mazungumzo ya kikazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari 2018. Wakwanza kushoto ni Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea. Wakwanza kulia ni Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea





Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania akimkabidhi zawadi ya picha ya mlima Kilimanjaro na kinyago cha mnyama waziri mwenzake wa Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Kang Kyung-hwa baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi baina ya nchi hizo mbili. 


Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi. Wakwanza kulia ni Mheshimiwa Balozi Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bi. Bertha Makilagi, afisa dawati wa Korea Kusini, Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo  ya Nje ya Korea Kusini na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tuesday, January 30, 2018

WAZIRI MAHIGA AANZA ZIARA YA SIKU 3 NCHINI KOREA KUSINI

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akipokelewa na maua na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Jamhuri ya Korea Kusini. Kushoto ni Ndugu Masuka, mume wa Balozi Masuka. 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI MAHIGA KOREA KUSINI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

                                                                                                                                                                                                                                                                                
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Jamhuri ya Korea Kusini yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea ya Kusini.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon Mjini Seoul, Mheshimiwa Waziri Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya GS E&C Bw. Min Jeong na timu yake inayoshugulikia uwekezaji na biashara nchini Tanzania.

Waziri Mahiga aliyeongozana na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) na Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji  cha Tanzania alielezea utayari wa Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama ule wa ujenzi wa reli ya kisasa ya viwango vya kimataifa wa “Standard Gauge Railway” inayohusisha makampuni makubwa ya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Jeong alielezea kuwa Kampuni ya GS E&C iliyojikita kwenye ujenzi wa miundombinu ya viwango vya kimataifa, ufuaji na usambazaji wa umeme, usafishaji wa mafuta n.k., sasa imejipanga pia kushiriki katika Ujenzi wa SGR (kupitia ushirikiano na kampuni ya Uturuki (awamu ya 3-5), na Ujenzi wa Daraja la Selanda.

Mbali na mpango huo, kwa sasa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu kwenye mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul, imeshiriki katika Mradi ya Umeme nchini Tanzania wa Dar-Arusha “Transmition Line”.

Waziri Mahiga alisisitiza nia ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kusimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Viwango na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Vilevile alitumia fursa hiyo kumuelezea Mkurugenzi Jeong na timu yake kuhusu mpango wa uendelezaji wa ujenzi wa reli hiyo ya viwango kutoka Isaka hadi Kigali, mpango ambao ulitangazwa na Waheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli na Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Tanzania na Rwanda hivi karibuni.

Mheshimiwa Mahiga alimhakikishia mkurugenzi huyo na kundi la makampuni anayoyaongoza, ushirikiano wake na kumkaribisha kuwekeza zaidi nchini Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya umeme na miundombinu mingine.

Kampuni ya GS E&C ni miongoni mwa makampuni kumi “Top Ten” yanayofanya vizuri zaidi nchini Korea Kusini inayokusanya faida ya kiasi cha $10 bilioni kwa mwaka.

Mheshimiwa Waziri Mahiga ambaye yupo nchini hapa kuanzia leo tarehe 30 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2018, kufuatia mwaliko wa Mhe. Dkt. Kang Kyung-wha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea anatarajiwa pia kuzindua Kongamano la kwanza la wafanyabiashara, kufungua majengo ya Ubalozi wa Tanzania na kufanya mazungumzo maalum na mwenyeji wake Waziri Kang Kyung-wha.

Mheshimiwa Mahiga atatumia sehemu kubwa ya ziara hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na makampuni makubwa yalikwisha onesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania. Mwishoni mwa ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mahiga anategemewa kutembelea Chuo cha Taifa cha Diploamasia cha Korea Kusini, kabla ya kurejea nchini Tanzania.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul, Korea Kusini,

30 Januari 2018.


Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na wawakilishi wa kampuni ya GS E&C waliofika hotelini kwake na kufanya naye mazungumzo ya kikazi kwenye Mji Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Seoul. Pichani wawili ni Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni hayo Bw. Min Jeoung. 





Ujumbe wa Mheshimiwa Mahiga ukiongozwa na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE wakiwa kwenye mazungumzo na wawakilishi wa makampuni ya GS E&C.

Picha ya Pamoja

Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Singapore

Kaimu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akizungumza na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Tan Puay Hiang alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao yalijikita katika kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuweza kuinua uchumi wa mataifa hayo.
Mazungumzo yakiendelea.

Mhe. Tan Puay Hiang akimkabidhi Balozi Mwinyi zawadi ya kitabu.

Picha ya pamoja Kaimu Katibu Mkuu, Mhe. Balozi Tan Puay Hiang, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Luhangisa (kulia) na Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wa Singapore, Bw. Lucien Hong(kushoto) 

Naibu Waziri akutana na Balozi wa Singapore nchini

 Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba akizungumza na Balozi wa Singapore nchini Mhe. Balozi Tan Puay Hiang, alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam, tarehe 29/11/2018. 
Katika mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Kolimba alishukuru Serikali ya Singapore kwa misaada wanayoitoa kwa Tanzania hasa katika eneo la elimu, Mhe. Dkt Suzan alitumia nafasi hiyo kumwalika Balozi huyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyo nchini ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Watalii kutoka nchi hiyo kutembelea Tanzania. 
Kwa upande wake Mhe. Puay Hiang aliikaribisha Tanzania kujifunza Singapore hasa katika eneo la Utalii na alimhakikishia Mhe. Waziri kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali.

Mhe. Dkt Suzan Kolimba na Mhe. Balozi Puay Hiang wakiendelea na mazungumzo, wanaofuatilia ni Bw. Emmanuel Luangisa; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia (Kushoto), Bw. Charles Faini Msaidizi wa Naibu Waziri ( Mwisho kushoto) na Bw. Lucien Hong Mkurugenzi msaidizi kutoka ubalozi wa Singapore ( kulia).    
                                     
Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo.

Monday, January 29, 2018

Mhe. Naibu Waziri amuaga Balozi wa Zimbabwe.

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Suzan Kolimba akimkabidhi zawadi Balozi wa Zimbabwe nchini anayemaliza muda wake Mhe. Balozi Edzai Chimonyo katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika Serena Hotel tarehe 29/01/2018. 

Katika hafla hiyo Mhe. Dkt Suzan alimshukuru kwa ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote alichokuwa Balozi hapa nchini na kumtakia heri katika majukumu yake mapya. Mhe. Balozi  alimshukuru Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Ushirikiano mkubwa alioupata wakati akitekeleza majukumu yake hapa nchini.

Waheshimiwa Mabalozi, Mhe. Brahim Buseif Balozi wa Sahara Magharibi nchini (wa kwanza kushoto) na Mhe. Benson Keith Chali Balozi wa Zambia Nchini wakifuatilia hafla hiyo

Mhe. Naibu Waziri Dkt Suzan Kolimba akiteta jambo na Mhe. Balozi Edzai Chimonyo katika hafla hiyo.


 Baadhi ya Maafisa kutoka Wizarani Bi. Elizabeth Mutunga na Bi. Robi Bwiru wakifuatilia hafla hiyo.

 Bw.Ayoub Mdeme Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika (Kulia) na Bw. Martin Tavenyika kutoka Ubalozi wa Zimbabwe nchini (kushoto) wakiwa katika hafla hiyo.

Bw. Suleiman Saleh Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika akiteta jambo na Mhe. Thamsanga Dennis Msekelu Balozi wa Afrika Kusini nchini, anayefuatilia ni Mhe. Balozi Edzai Chimonyo.

Maafisa kutoka Wizarani Bw. Charles Faini na Bi. Mercy Kitonga nao wakiwa katika hafla hiyo.

Friday, January 26, 2018

Mhe. Hamad Rashid akutana na Naibu Waziri wa Kilimo wa China

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohammed akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Mhe. Dkt. QU DONGYU walipokutana katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijijni Dar es Salaam tarehe 26 Januari, 2018 kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikino katika sekta ya kilimo na uvuvi kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na China.  Mhe. Dkt. QU DONGYU yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Mazungumzo kati ya Mhe. Hamad Rashid na Mhe. Dkt. QU DONGYU yakiendelea huku wajumbe wa China na Tanzania wakifuatilia.
Mhe. Hamad Rashid na Dkt. QU kwa pamoja wakipitia baadhi ya nyaraka za ushirikiano


Picha ya pamoja kati ya Mhe. Hamad Rashid na Dkt. QU DONGYU pamoja na wajumbe wengine walioshiriki kikao hicho. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki
Mhe. Hamad Rashid akiagana na Dkt. QU DONGYU mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Thursday, January 25, 2018

Naibu Waziri wa Kilimo wa China atembelea Tanzania


Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt.Charles Tizeba ( Katikati mwenye kipaza sauti), akiongoza mazungumzo wakati wa Mkutano na Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Mhe. DK QU DONGYU(hayupo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC) tarehe 25 Januari,2018. 
Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania China Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki ( wa kwanza kulia), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt.Thomas Kashilila, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (wa pili kutoka mwisho kushoto). 

Katika majadiliano hayo pande zote mbili zimekubaliana kuundwa kikosi kazi ambacho kitakuwa na kazi ya kuhakikisha maeneo waliyokubaliana kushirikiana yanatekelezwa, kikosi kazi hicho kitahusisha wataalam kutoka Tanzania na China. Baadhi ya maeneo ambayo China na Tanzania watashirikiana ili kuinua kilimo cha Tanzania ni; kuboresha miundombinu ya Kilimo kama vile Scheme za Umwagiliaji, ushirikiano kati ya chuo cha Kilimo cha Sokoine na vyuo vya kilimo vya China, kushirikiana katika tafiti mbalimbali, China kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani katika mazao, masoko n.k. Mhe. DONGYU  anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 28, Januari,2018. 


Naibu Waziri wa Kilimo wa China Mhe. DK QU DONGYU ( wa tatu kulia mwenye kipaza sauti) akielezea jambo katika mazungumzo hayo, kushoto kwake ni balozi wa China nchini Mhe. Balozi Wang Ke na wengine ni ujumbe wa watalaam waliongozana na Mhe. Waziri DONGYU

  Waziri wa Kilimo kutoka China Mhe. DK QU DONGYU pamoja na ujumbe aliongozana nao wakifuatilia mazungumzo
Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkutano.

Tuesday, January 23, 2018

Timu Maalum ya ADB yatembelea Tanzania



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Aldof Mkenda (kulia) akiwa katika mazungumzo na Bw. Alieu Jeng- Mjumbe wa Timu kutoka Bank ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank), walipomtembelea Wizarani tarehe 22 Januari,2018
Timu hiyo yenye jumla ya wajumbe watatu ambao watakuwa nchini kwa lengo la kujadiliana na Serikali kuhusu maeneo ya vipaombele ambayo wanaweza kusaidia kupitia bajeti yao ya 2018/2019. wakiwa nchini watakutana na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa mujibu wa wajumbe hao, bajeti hii itazingatia zaidi kusaidia Serikali kupitia maeneo  ya vipaombele yaliyoanishwa  ili kuwezesha Sekta binafsi kuweza kuchochea uchumi wa nchi kupitia biashara na Uwekezaji katika maeneo mbalimbali.  wajumbe hao waliwasili tarehe 14 Januari, 2018 na wanatarajiwa kuondoka tarehe 27 Januari,2018.


 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Aldof Mkenda (kulia), akiendelea na mazungumzo na wajumbe wa Timu kutoka ADB ambao ni Bw.Alieu Jeng(Kushoto), Bw. Frsncois Nkulikiyimfura anayefuata na mwisho kushoto ni Bi.Eline Okuozeto

Katibu Mkuu, timu ya ADB na Wataalam kutoka Wizarani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo




Monday, January 22, 2018

Israel kusaidia sekta ya afya nchini Tanzania


Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Dkt. Otilia Flavian Gowelle akiwa katika mazungumzo na Naibu Balozi wa Israel nchini, Mhe. Michael Baruch Baror kabla ya wawili hao hawajasaini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya Afya kati ya Tanzania na Israel.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Dkt. Otilia Flavian Gowelle pamoja na Naibu Balozi wa Israel nchini, Mhe. Michael Baruch Baror wakiweka saini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya Afya kati ya Tanzania na Israel. Makubaliano hayo yataanza kwa kuijengea uwezo hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma ambapo Israel itasaidia ujenzi wa Kitengo cha dharua na mifupa pamoja na ujenzi wa Kitengo cha kisasa cha wagonjwa mahututi (ICU).
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Dkt. Otilia Flavian Gowelle pamoja na Naibu Balozi wa Israel nchini, Mhe. Michael Baruch Baror wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilisha zoezi la uwekaji saini. Watatu kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda.

Balozi wa Zimbawe atembelea Wizara ya Mambo ya Nje


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba akisalimiana na Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania anayemakiza muda wake, Mhe. Idzai Chimonyo ambaye alifika ofisini kwa Mhe. Naibu Waziri kwa ajili ya kuaga.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania anayemakiza muda wake, Mhe. Idzai Chimonyo.
Mazungumzo yanaendelea

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania anayemaliza muda wake, Mhe. Idzai Chimonyo. Wengine katika picha ni Afisa Dawati wa Zimbabwe, Bibi Halima Abdallah na Afisa Ubalozi wa Zimbabwe, Bw. Martin Tavenyika.

WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA COMORO


Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe, Sylvester Mabumba (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Comoro, Bw. Said Mohamed Omar (wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi wa vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group pamoja na wajumbe waliofuatana nao katika ziara maalum ya kufungua na kuzitangaza fursa zilizopo Tanzania na Comoro.

================================================
WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA COMORO

Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba alipokea ujumbe wa Clouds Media Group uliowasili visiwani humo  tarehe tarehe 20 Januari 2017 kwa ziara maalumu ya siku tatu ikiwa na lengo la kushirikiana na Ubalozi kuzitangaza fursa mbalimbali zinazopatikana Visiwani humo kwa Watanzania.   

Ujumbe huo wa Clouds Media Group ukiongozwa na Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji, Bw. Ruge Mutahaba uliwasili Comoro kufuatia mualiko wa Ubalozi wa Tanzania hapa Comoro ambapo lengo lake lilikuwa ni kuja kufanya tathamini ya kuzindua Jukwa la Fursa (FURSA EXPO) Visiwani Comoro kama sehemu ya kuendeleza kampeni za kuwapatia vijana wa Kitanzania taarifa muhimu kuhusiana na fursa za uwekezaji na biashara.

Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro kwa kushirikiana na Ujumbe wa Clouds Media Group umelenga ifikapo mwezi Aprili 2018 kupanua mianya ya uwekezaji nchini Comoro pamoja na kuhakikisha kwamba masoko ya uhakika yanapatikana kwa ajili ya bidhaa za Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo Uchumi wa Tanzania unaelekea kuwa ni uchumi wa Viwanda.

Aidha, Mhe. Balozi akiwa ameambatana na ujumbe wa Clouds Media Group alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na wadau kutoka sekta mbalimbali za Serikali ya Comoro, Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kufungua maeneo mapya ya ushirikiano sambamba na kuhakikisha vijana wananufaika na ushirikiano baina ya nchi na nchi ulioanzishwa na mataifa yao” alisema Mhe. Balozi

Aidha, Mhe. Balozi alielezea anataraji ziara hiyo italeta matokeo chanya na kwamba kuzinduliwa kwa jukwaa la FURSA EXPO ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo inalenga kwenye Diplomasia ya Uchumi na kwamba kupitia jukwaa hilo bidhaa za Tanzania zinauhakika wa kuingia kwenye Soko la Comoro kwani nchi ya Comoro inaitegemea Tanzania kwa kiasi kikubwa katika mahitaji yake mbalimbali.

Pia ujumbe wa Clouds Media Group ulitumia nafasi hiyo kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Visiwani Comoro, Ndg. Said Mohamed Omar, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Kitaifa ya Utalii, Ndg. Mouzamildine Youssouf pamoja na Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Vijana. Katika mazungumzo hayo, wajumbe walionesha nia ya kutaka kushirikiana kwa pamoja katika kuendesha kampeni itakayoibua maeneo muhimu ya kimkakati ambayo Vijana wa Kitanzania na wale wa KiComoro wanaweza kushirikiana.

Naye Bw. Ruge Mutahaba kwa upande wake alieleza kufurahishwa na fursa mbalimbali zinazopatikana Comoro na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Visiwani hapa kuhakikisha kwamba FURSA EXPO Comoro inafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa lengo la kuinua uchumi wa vijana wa Kitanzania na wa KiComoro.



Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya comoro pamoja na Wajumbe kutoka clouds Media Group wakiwa katika mazungumzo ya pamoja  na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Comoro, Bw. Mouzamildine Youssouf.