Friday, February 9, 2018

Hotuba ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Hafla ya Mabalozi

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA ALIYOINDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA VIONGOZI WA TAASISI
ZA KIMATAIFA KUKARIBISHA MWAKA MPYA 2018
IKULU, DAR ES SALAAM, 9 FEBRUARI, 2018

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

Mheshimiwa Brahin Salem Buseif, Balozi wa Saharawi na Kaimu Kiongozi wa Mabalozi nchini;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa, 

Mabibi na Mabwana:

Habarini za Jioni. Karibuni sana hapa Ikulu. Nawashukuru, Waheshimiwa Mabalozi, kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria hafla hii, ambayo kwenye utamaduni wa kidiplomasia, imezoeleka duniani kote. Tanzania na sisi tumekuwa tukifanya hafla hii kila mwaka; na bila shaka, tutaendelea kuifanya. Hata hivyo, napenda kuwaarifu kwamba, mwaka huu, huenda ukawa wa mwisho kwa hafla hii kufanyika hapa Dar es Salaam. Tunatarajia, kuanzia mwakani, kufanyia Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu.
Hivyo basi, niwaombe, Waheshimiwa Mabalozi, mwakani, mjiandae kuja Dodoma, ambako viongozi wengi wa Serikali tayari wamehamia, ikiwa ni pamoja na Mawaziri, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Mimi pia natarajia kuhamia mwaka huu. Dodoma ni pazuri na ni katikati mwa nchi yetu.  Napongeza Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma, ambapo mwezi Desemba 2017, walifungua Ofisi zao za Muda. Hongereni sana. Nawasihi Mabalozi wengine ninyi muige mfano huu wa Umoja wa Mataifa; na napenda kuwaarifu kuwa Serikali itagawa bure viwanja mjini Dodoma, ambapo kila Ofisi ya Kibalozi itapata Ekari 5.5.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Hivi sasa ni takriban mwezi mmoja na siku kadhaa umepita tangu kuanza kwa Mwaka Mpya 2018. Kwa utamaduni wetu sisi Watanzania, mwaka ukianza, hadi mwezi Machi, huwa tunaendelea kupeana heri ya mwaka mpya. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutumia fursa hii, kuwawatakia heri ya Mwaka Mpya wa 2018, ninyi Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, familia pamoja na watumishi wenu.  Aidha, naomba mnifikishie salamu zangu za Heri ya Mwaka Mpya 2018 kwa Wakuu wa Nchi pamoja na Taasisi na Mashirika, ambayo mnayawakilisha vizuri hapa nchini.

Nafahamu kuwa, kwa baadhi yenu, hii ni mara ya kwanza kushiriki katika hafla hii hapa Tanzania. Napenda nirudie tena kuwakaribisha sana nchini kwetu. Tanzania ni nchi nzuri; watu wake ni wakarimu na ina vivutio vingi vya utalii. Nina uhakika, mmeshasikia kuhusu Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, pamoja na Mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Lakini, mbali na vivutio hivyo, vinavyotambulika ulimwenguni kote, tunavyo vivutio vingine vingi vizuri. Mti mrefu zaidi Barani Afrika upo hapa nchini, tena karibu kabisa na Mlima Kilimanjaro. Aidha, tuna Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni kubwa zaidi nchini na inasifika kwa kuwa na tembo wengi. Vilevile, tunayo Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo inasifika kwa kuwa na aina nyingi za maua ya ndwele ya asili ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani; na pia Maporomoko ya Mto Kalambo, kule Rukwa, ambayo ni ya pili kwa kuwa na kina kirefu Barani Afrika, baada ya yale ya Tugale yaliyopo nchini Afrika Kusini. Hivyo basi, nawahimiza, mkipata muda, tembeleeni vivutio hivyo ili mjionee uzuri wa Tanzania. Tunawaomba pia muwahamasishe wananchi wenu kuja kutembelea vivutio vyetu.

Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, duniani kote, katika kipindi cha mwanzo wa mwaka kama hiki; ni jambo la kawaida kufanya tafakari ya masuala ya mwaka uliopita na kupanga mikakati ya mwaka mpya. Kwetu sisi Tanzania, Mwaka 2017, ulikuwa wenye mafanikio makubwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa; japo changamoto nazo zilikuwepo.
Mathalan, katika ngazi ya kitaifa, mwaka jana, tuliendelea kutekeleza Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka mitano wa 2016/17 – 2020/2021, unaolenga kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Na katika kutekeleza Mpango wetu, tuliweka pia mkazo katika kushughulikia matatizo yaliyokuwa yakitukwamisha katika kupiga hatua za kimaendeleo. Kama mjuavyo “Ukitaka kupata maendeleo, badala ya kuongeza tu bidii, jambo la kwanza unatakiwa kushughulikia au kurekebisha mambo yanayokukwamisha kupata maendeleo”. Mathalan, ukitaka kujitosheleza kifedha, njia nzuri sio kuongeza bidii ya kutafuta fedha, bali unatakiwa kwanza kudhibiti matumizi ya kile kidogo unachokipata. Na vilevile, ukitaka kupungua unene, njia nzuri sio kuanza kufanya mazoezi, bali ni kuacha kufanya mambo yanayosababisha uwe mnene.
Kwa kuzingatia hilo, mwaka 2017, tuliendelea kushughulikia matatizo yenye kuikwamisha nchi yetu kupata maendeleo. Tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi na uporaji wa rasilimali zetu. Kama mnavyofahamu, miongoni mwa mambo yanayozikwamisha nchi za Afrika kupata maendeleo ya haraka kiuchumi, Tanzania ikiwemo, ni vitendo vya rushwa, ukwepaji kodi na uporaji wa rasilimali. Ripoti ya Jopo la Umoja wa Afrika, ambalo liliongozwa na Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, iliyotolewa mwaka 2015, ilibainisha kuwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo, zimepoteza takriban Dola za Marekani trilioni 1.8, wastani wa Dola za Marekani bilioni 50 – 80 kwa mwaka. Aidha, Ripoti hiyo iliendelea kueleza kuwa, hivi sasa, nchi za Afrika, kila mwaka, zinapoteza wastani wa Dola za Marekani bilioni 150 kutokana na rushwa, wizi, ukwepaji kodi na uporaji wa rasilimali.
Hivyo basi, katika mwaka 2017, tumeendelea kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo. Tumepitisha sheria ya kulinda na kusimamia rasilimali zetu ili ziweze kuinufaisha nchi yetu. Ni wazi kuwa hatua hii huenda haikuwafurahisha baadhi ya watu, lakini ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu. Hivyo, ilikuwa ni lazima tuichukue. Sambamba na hilo, tumeendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi, na hivyo kuweza kuongeza ukusanyaji mapato. Mathalan, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2017, tulifanikiwa kukusanya kodi kiasi cha shilingi trilioni 7.87, sawa ongezeko la asilimia 8.45 ukilinganisha na mapato ya kipindi kama hicho mwaka 2016. Lakini, kubwa zaidi ni kwamba, mwezi Desemba 2017, mapato ya kodi yaliyokusanywa ni shilingi trilioni 1.66. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa hapa nchini. 
Kutokana na hatua tunazozichukua, uchumi wetu umeendelea kuimarika. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8, na hivyo kuifanya nchi yetu kuongoza katika Ukanda wetu wa Afrika Mashariki, lakini pia kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa Barani Afrika. Tulifanikiwa pia kudhibiti mfumko wa bei, ambapo mwezi Desemba 2017 ulifikia asilimia 4. Kwa ujumla, wastani wa mfumko wa bei nchini mwaka jana ulikuwa chini ya asilimia 5.5, kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika. Akiba ya fedha za kigeni nayo imeongezeka; na tumeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za jamii, hususan zile zenye kuwagusa wananchi wengi kama vile afya, elimu na maji. Na hii, bila shaka, ndio moja ya sababu iliyoifanya nchi yetu itajwe kuongoza kwa uchumi shirikishi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Mbali na kushughulikia matatizo ya rushwa, wizi, ukwepaji kodi, n.k.; tumeendelea kushughulikia changamoto nyingine zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya nchi yetu. Kama mnavyofahamu, ukiachilia mbali vitendo vya rushwa pamoja na wizi na ubadhirifu wa rasilimali, changamoto nyingine kubwa inayokabili Bara la Afrika, ni tatizo la kukosekana kwa miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Mathalan, kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika (Africa Progress Report) ya mwaka 2015, watu zaidi ya milioni 600, ambao ni takriban nusu ya watu wote wa Bara la Afrika, hawatumii umeme. Takwimu pia zinaonesha kuwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, zote kwa pamoja, ukiondoa Afrika Kusini, zinatumia umeme kidogo ukilinganisha na nchi ya Hispania. Aidha, matatizo haya ya umeme yanachangia kushusha kwa asilimia 2.4 Pato la Afrika. Lakini, ukiachilia mbali umeme, gharama za usafirishaji Barani Afrika ni kubwa ukilinganisha na Mabara mengine kutokana na ama kukosekana au udhaifu wa miundombinu ya usafiri.  Mambo haya yote kwa pamoja, ndio yanasababisha mchango wa Bara la Afrika kibiashara na uwekezaji duniani kuwa mdogo sana.
Kwa kutambua hilo, tumeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya usafiri pamoja na upatikanaji wa umeme. Sehemu kubwa ya nchi hivi sasa imeunganishwa kwa barabara; na nyingine zinaendelea kujengwa. Aidha, mwaka 2017 tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma. Reli hii baadaye itaungana na reli za kwenda nchi za Burundi na Rwanda. Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma chenye urefu wa kilometa 712 tayari umeanza na utagharimu kiasi cha shilingi trilioni 7.062, zote zitatolewa na Serikali yetu. Aidha, hivi karibuni, wakati wa ziara ya Rais Kagame wa Rwanda, tumekubaliana kuanza ujenzi wa kipande cha kutoka Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda. Sambamba na hayo,  tunaendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege vikubwa vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro pamoja na vingine takriban 11 katika mikoa mbalimbali lengo likiwa kukuza sekta yetu ya utalii. Vilevile, tunafanya upanuzi mkubwa na kuboresha utendaji wa bandari zetu kuu za Dar es Salaam na Mtwara kwa gharama ya takriban shilingi trilioni 1.1. Tunatekeleza miradi hii kwa vile takriban asilimia 90 ya shehena ya mizigo inayokuja hapa nchini upitia kwenye bandari hizi. Bandari hizi, hususan ya Dar es Salaam, inategemewa pia na nchi nyingine jirani. Sambamba na bandari hizo, tunaiboresha Bandari ya Tanga, hususan baada ya nchi yetu pamoja na Uganda kuingia makubaliano ya kutekeleza mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Ujenzi wa Bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,415 utaanza mwaka huu, ambapo, kama mtakavyokumbuka, mwaka jana, mimi na Rais Museveni wa Uganda tuliuwekea jiwe la msingi.
Kuhusu umeme, tunaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme. Mwaka 2017, tumeanza Awamu ya Tatu ya kupeleka Umeme Vijiji, ambapo tunatarajia kufikisha umeme kwenye vijiji 7,873. Lengo letu ni kwamba, ifikapo Mwaka wa Fedha 2020/2021, vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na miudombinu ya umeme. Tunatekeleza pia miradi mikubwa ya kuzalisha umeme, hususan kwa kutumia gesi yetu asilia. Aidha, mwaka huu, tunatarajia kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia maji wa Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka ikifika mwaka 2020, nchi yetu angalau iwe Megawati 5,000 kutoka Megawati 1,460 za sasa. Nafahamu kumekuwa na maneno maneno kuhusu mradi wetu wa Stiglier’s Gorge; ukihusishwa na uharibifu wa mazingira katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Ukweli ni kwamba, hakutakuwa na uharibifu wowote.  Tumefanya tathmini ya kina ya mazingira, na tumeweka mikakati ya kudhibiti uharibifu. Zaidi ya hapo, mradi huu, utatekelezwa katika eneo dogo sana. Ni chini ya asilimia 4 ya eneo zima la Hifadhi ya Ruaha. Hivyo, hakuna uwezekano wowote wa kuathiri mazingira ya eneo hilo.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Kuhusu azma yetu ya kujenga viwanda, kwa ujumla, tunaendelea vizuri. Kama mjuavyo, duniani kote, hakuna nchi imewahi kupata maendeleo ya kiuchumi bila kutegemea viwanda. Na mnafahamu pia kuwa, sekta ya viwanda ni muhimu katika kupiga vita umaskini na tatizo la ajira. Hivyo basi, mwaka 2017 tumeendelea na jitihada za kujenga uchumi wa viwanda nchini. Na napenda niwaarifu kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, takriban viwanda 3,500 vimejengwa. Na vingine vingi vinaendelea kujengwa. Nitumie fursa hii, kuishukuru sekta binafsi ya hapa nchini na kutoka nje kwa namna ilivyoitikia vizuri wito wa Serikali yetu wa kujenga viwanda. Nafahamu kuwa kuna baadhi ya watu wanaeneza uzushi kuwa sisi hatuipendi sekta binafsi. Hiyo sio kweli hata kidogo. Tunaipenda sekta binafsi na tunathamini na kutambua mchango wao. Na tunafahamu kuwa katika dunia ya sasa sekta binafsi ni mhimili muhimu katika kujenga uchumi.
Kwa sababu hiyo, tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi ya hapa nchini na ile ya nje. Tutaendelea pia kushughulikia vikwazo mbalimbali vinavyoikabili sekta hii, ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera na sheria zetu pale inapobidi; kuongeza vivutio vya uwekezaji na biashara; kushughulikia matatizo ya urasimu, rushwa, utitiri wa kodi, n.k. Hivyo basi, nahimiza sekta binafsi kuendelea kuwekeza hapa nchini. Na niwaombe Waheshimiwa Mabalozi, nanyi wahimizeni wafanyabishara kutoka nchi zenu kuja kuwekeza hapa nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za uwekezaji. Ukiachilia mbali sekta ya viwanda, tuna fursa kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, ujenzi wa miundombinu, huduma, n.k. Aidha, nchi yetu ina soko kubwa. Tunapakana na nchi takriban 8, lakini pia sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na halikadhalika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu wapatao milioni 500. Hili ni soko kubwa kwa mwekezaji yeyote.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
          Kimataifa, mwaka 2017, nchi yetu imeendelea kushiriki kikamilifu kwenye masuala mbalimbali katika ngazi ya Kikanda, Bara na duniani kwa ujumla. Kama mnavyofahamu, msingi mkuu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kuimarisha ujirani mwema, ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Hivyo, tumeendelea kutekeleza Sera hiyo. Mimi pamoja na viongozi wenzangu, tumefanya ziara na kushiriki kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa. Binafsi, mwaka jana, nilihudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika na kutembelea nchi ya Uganda. Aidha, tulipata bahati ya kutembelewa na viongozi kadhaa wa nchi na taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn; Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Dkt. Makhtar Diop; Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim; na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mhe. Tao Zang; pamoja na viongozi wengine wengi. Wakati wa ziara hizo, tuliweza kufikia makubaliano mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano, hususan kwenye nyanja za kiuchumi.
Mwaka jana pia, tumeendelea kushirikiana na nchi pamoja na taasisi nyingine za kimataifa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Kanda, Bara na dunia yetu kwa ujumla. Na moja ya changamoto hizo ni suala la migogoro. Kama mnavyofahamu, tangu imepata uhuru, mwaka 1961, nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta amani Barani Afrika na duniani. Tumeshiriki na tunaendelea kushiriki katika harakati za usuluhishi wa migogoro ya     Burundi, DRC, n.k. Tunafarijika kuona kuwa amani nchini Burundi inaendelea kuimarika; na tunaendelea kuwahimiza wahusika kwenye migogoro nchini DRC, Sudan Kusini, n.k., kumaliza tofauti walizonazo ili kuweza kurejesha amani kwenye nchi zao.
Mbali na ushiriki wetu katika usuluhishi wa migogoro, nchi yetu, hivi sasa, ina vikosi kwenye misheni za kulinda amani nchini DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Nitumie fursa hii, kuzishukuru nchi na taasisi za kimataifa zilizotutumia salamu za rambirambi na pole kufuatia tukio lililotokea tarehe 8 Desemba 2017 la kuuawa kwa askari wetu 15 na wengine 43 kujeruhiwa, wakati wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini DRC. Tukio hili, kwa hakika, liliacha majonzi na simanzi kubwa kwa Watanzania. Hata hivyo, napenda niseme kuwa, pamoja na majonzi makubwa tuliyopata, halijatukatisha tamaa wala kutuyumbisha kama nchi yetu. Tutaendelea kushiriki katika harakati za kutafuta amani mahali popote duniani, na tutaendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Tunaushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuunda Timu kuchunguza chanzo cha tukio la tarehe 8 Desemba, 2017. Tunaihimiza Timu iliyoundwa kukamilisha mapema uchunguzi wake, ili chanzo kijulikane, wahusika wafahamike na hatimaye sheria ifuate mkondo wake.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Katika mwaka huu wa 2018, Tanzania itaendelea kutekeleza Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Tutazidisha mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu. Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan ya usafiri na nishati ya umeme.  Tutaboresha huduma mbalimbali za kijamii, hususan elimu, afya a maji.
Sambamba na hayo, tutaendelea kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa. Tutakuwa wanachama waaminifu wa taasisi za Kikanda, katika Bara na kimataifa, ambazo sisi ni wanachama. Tutaendelea kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro; na vikosi vyetu vitandelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Vilevile, tutaendelea kutekeleza mipango na malengo mbalimbali ya kikanda, kibara na kidunia, ikiwemo Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo Endelevu ya 2030. Na moja ya malengo ya dunia tuliyopanga kutekeleza, ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 ni kuzuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Katika kufikia azma hii, tumeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi, ambapo tumelenga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 6 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hivyo basi, tunawaomba mtuunge mkono.  
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Nafahamu, katika hafla kama hii, hotuba huwa haziwi ndefu. Lakini leo, nimeeleza mengi. Nimefanya hivyo, kwa kuwa, kama nilivyosema awali, hii huenda itakuwa mara ya mwisho kwa sherehe hizi kufanyika hapa Dar es Salaam. Mwakani ni Dodoma. Na kwa sababu hiyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu nieleze masuala matatu ya mwisho.
Suala la kwanza; muda mfupi uliopita, nimeeleza kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Na napenda kusisitiza tena kuwa tutaendelea kushiriki kwenye misheni hizo. Hata hivyo, wakati nikisisitiza hilo, napenda kueleza masikitiko yetu kuhusu uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani. Ni kweli, uendeshaji wa misheni za kulinda amani ni gharama kubwa. Lakini, ni ukweli pia usiopingika kuwa, hakuna gharama inayozidi maisha ya watu na umuhimu wa amani. Tanzania tunauona uamuzi huu utadhoofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro; na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro. Hivyo basi, tunauomba Umoja wa Mataifa pamoja na Nchi Tano Wanachama wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa kutafakari upya uamuzi huo.
Suala la pili, ni kuhusu uamuzi wetu wa hivi karibuni wa kujitoa kwenye Mpango wa Majaribio wa Kutafuta Suluhu ya Kudumu ya Tatizo la Wakimbizi (Comprehensive Refugee Response Framework – CRRF). Kwanza kabisa, napenda kueleza kuwa, nchi yetu, tangu imepata Uhuru mwaka 1961, imekuwa ni miongoni mwa nchi zenye kupokea wakimbizi wengi. Mpaka sasa tunaendelea kuwapokea; na bila shaka, tutaendelea kuwapokea, lakini ni wale tu wenye kustahili; na kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Nchi yetu pia imeweka historia duniani kwa kuwa ya kwanza kutoa uraia kwa wakimbizi wapatao 150,000 kwa wakati mmoja. Hakuna nchi imewahi kufanya hivyo. Hata hivyo, kutokana na sababu za usalama, tumelazimika kujitoa kwenye Mpango wa CRRF, ambao pamoja na masuala mengine, unaelekeza kutolewa kwa ardhi kwa ajili ya wakimbizi, kuwaruhusu kutembea mahali popote na kutoa vibali vya ajira. Tumejitoa kwa sababu tunadhani kuwa, katika kipindi hiki cha sasa ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za usalama, ikiwemo ugaidi, kushamiri kwa biashara ya binadamu na makosa mengine ya kimataifa, utekelezaji wa Mpango huu unaweza kuleta madhara makubwa ya kiusalama kwa nchi yetu. Lakini, mbali na hilo, tumesita kuendelea na Mpango huu kutokana na uzoefu tulioupata wakati tulipotoa uraia kwa wakimbizi 150,000. Wakati tunatoa uraia, jumuiya ya kimataifa iliahidi ingetoa fedha za kuwapatia makazi na masuala mengine muhimu. Lakini, mpaka sasa, hakuna fedha iliyotolewa; na badala yake tumeanza kushawishiwa tukope fedha za kuwahudumia wakimbizi. Hali hii imetukatisha tamaa; na bila shaka mtakubaliana nasi kuwa, kukopa fedha kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi kutaibebesha Serikali yetu mzigo mkubwa.  Hivyo, tunaiomba jumuiya ya kimataifa ielewe uamuzi wetu wa kujitoa.
Suala la tatu na la mwisho ni kuhusu taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania, ambazo zimejihusisha kwenye matukio ya uhalifu. Taarifa hizi kwa hakika zimetusikitisha sana sisi kama Taifa, kwa sababu zinachafua jina na sifa nzuri ya nchi yetu. Hata hivyo, ningependa kufafanua kuwa, kimsingi, meli hizo si za kwetu; zimesajiliwa tu hapa Tanzania. Kama mnavyofahamu, usajili wa meli za nje ni jambo la kawaida na linafanywa na nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo, kutokana na matatizo yaliyojitokeza, Serikali imeamua kuchukua hatua. Tumesitisha usajili wa meli zote 470 zilizosajiliwa hapa nchini zenye kupeperusha bendera yetu, na tumeanza kufanya uchunguzi wa kina kuthibitisha uhalali wa shughuli zao. Zile zitakazobainika kukiuka sheria na taratibu, tutazifutia usajili. Sambamba na hilo, tumesitisha usajili wa meli mpya kutoka nje mpaka pale itakapotangazwa tena. Tumechukua hatua hizo, ili nchi yetu isiwe kichaka cha kujificha wahalifu.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu, kwa kurudia tena kuwashukuru kwa kuhudhuria hafla hii. Aidha, nawashukuru kwa namna ambavyo nchi zenu na mashirika mnayowakilisha yanashirikiana na nchi yetu katika nyanja mbalimbali: kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiulinzi na usalama, n.k. Mchango wenu ni mkubwa sana. Bila ninyi, huenda mambo mengi tuliyotekeleza mwaka jana, yasingewezekana. Hivyo basi, tunawashukuru sana; na kupitia kwenu, tunaendelea kuziomba nchi na taasisi mnazoziwakilisha ziendelee kutuunga mkono. Kwa upande wetu, tutazidi kuimarisha uhusiano wetu na nchi, mashirika na taasisi zenu.
Baada ya kusema hayo, napenda kurudia tena kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya 2018. Uwe mwaka wa Amani na Mafanikio.

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”


Tanzania yaendelea kupunguza vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru na tozo mbalimbali


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania yaridhia kufuta tozo ya Dola za Kimarekani 40 kwa wasafirishaji wa mizigo

Tanzania imeridhia kufuta tozo ya Dola za Kimarekani 40 (USD40) inayotozwa kwa kila stika kwenye magari yanayosafirisha mizigo kwenda nje ya nchi. Hatua hii imefikiwa kwenye Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Arusha

Akizungumza katika Mkutano huo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema Tanzania imefikia hatua hii ikiwa ni moja ya jitihada za kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini na Jumuiya kwa ujumla.

Tozo hii imekuwa ikitozwa kwa kipindi cha muda mrefu kwa malori yanoyosafirisha mizigo kwenda sehemu mbalimbali nje ya mipaka ya nchi. Baada ya tathimini Serikali imebaini kuwa tozo hii inasababisha usumbufu na kuongeza gharama kwa wasafirishaji wa mizigo. Hata hivyo hatua hii inaendelea kuifanya Tanzania kuwa mtekelezaji mzuri wa makubaliano na itifaki mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano huu uliofanyika kwa kipindi cha siku tatu tarehe 7 hadi 9 Februari 2018, pamoja na mambo mengine ulilenga kujadili na kutatua vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru (NTBs) ambavyo vimekuwepo kwa muda mrefu katika Jumuiya. Mkutano huu umefikia tamati leo katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.

Taratibu za kuanza kufuta tozo hii zinaanza kutekelezwa mara moja.


-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
 9 Februari 2018


Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe. CharleS Mwijage(Mb) akifuatilia Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea.

Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe. CharleS Mwijage(Mb) akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki 

Mkutano ukiwa unaendelea

Katibu Mkuu Mambo ya Nje akutana na Mwakilishi wa Aga Khan

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kulia) akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Aga Khan, Bw. Amin Kurji alipomtembelea katika Ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Februari 2018.
Mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Bw. Kurji yalijikita katika kujadili masuala ya ushirikiano na shughuli za maendeleo ambazo zimekuwa zikifanywa na Shirika la Aga Khan nchini katika kuhudumia wananchi hususan katika sekta ya Afya na Elimu. 


Mazungumzo yakiendelea, kulia ni wajumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Thursday, February 8, 2018

Kufanyika kwa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji

Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha, na Uwekezaji unaendelea kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Masharik Jijini Arusha. Mkutano huu unafanyika kwa muda wa siku tatu  tarehe 7 hadi 9 Februari, 2018.

Pamoja na mambo mengine Mkutano huu unatarajiwa kufanya mambo yafuatayo:
·         Kujadili kuhusu vikwazo vya biashara vya muda mrefu visivyo vya kiushuru

·         Kupokea taarifa ya mwenendo wa sasa wa soko kati ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EU-EAC);

·         Kupokea taarifa ya Biashara na Uwekezaji ya mwaka 2016 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Taarifa hii inaainisha mafanikio, changamoto na kutoa mwenendo wa biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na

·         Kupokea na kuridhia mwongozo wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) ambao utatoa utaratibu wa namna ya kuviendesha vituo hivyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkutano huu unafanyika ili kujadili na kutoa ufumbuzi wa masuala mbalimbali kama ilivyoagizwa kwenye Mikutano iliyopita ya Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mkutano huu unafanyika katika ngazi tatu; ngazi ya Wataalamu, ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye katika ngazi ya Mawaziri.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
 8 Februari 2018





Kaimu Mkurugezi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Bernard Haule akizungumza kwenye Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezajia la Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Wajumbe kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano 

Naibu Katibu Mkuu, Biashara na Uwekezaji Tanzania bara  Prof. Joseph Buchweishaija (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Bw. Ally K. Juma (kulia), wakifuatilia Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji katika ngazi ya Matibu Wakuu

Sehemu ya Wajumbe kutoka nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki Wakifuatilia Mkutano

Naibu Katibu Mkuu wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Bw. Ally K. Juma akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji ngazi ya Makatibu Wakuu

Mkutano wa Pamoja kati ya Wizara na Ubalozi wa China nchini wafanyika

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akifungua Mkutano wa Pamoja kati ya Wizara na Ubalozi wa China hapa nchini uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, tarehe 8 Februari,2018. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango - Zanzibar, Bw. Khamis Mussa Omar, wengine ni watendaji  na Maafisa kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Lengo la Mkutano huu pamoja na mambo mengine ni kukubaliana njia ya kufuatilia utekelezaji wa masuala mbalimbali katika maeneo ya Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Akiongea katika Mkutano huu Prof. Mkenda amesema juhudi hizi zitasaidia kufuatilia na kugundua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali kati ya Tanzania na China na kuzitatua kwa pamoja ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ambayo Tanzania na China tumekubaliana katika maeneo mbalimbali, ili wananchi wa nchi hizi mbili kunufaika na Ushirikiano huu wa kihistoria. Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi na Maafisa kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali Serikali.
Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda ( wa kwanza kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Ustralasia Bibi Justa Nyange, Bw. Joseph Kiraiya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkrugenzi Mkuu wa EPZA Kanali Mstaafu Joseph Simbakaria na wengine ni Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali wakifuatilia Mkutano huo.
Balozi wa China nchini Mheshimiwa Wang Ke, ( katikati) akiongea katika Mkutano huo, wengine ni Maafisa kutoka Ubalozi wa China nchini alioambatana nao.

Sehemu ya Maafisa kutoka Wizarani na Taasisi nyingine za Serikali wakifuatilia Mkutano huo.

      Picha ya Pamoja

Sunday, February 4, 2018

WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA NCHINI KOREA KUSINI

 AAHIDI USHIRIKIANO WENYE TIJA KWA MAENDELEO YA WANANCHI WOTE


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameahidi kusimamia uimarishwaji wa uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ili wananchi wa pande zote mbili wapate manufaa.

Waziri Mahiga ameyasema hayo alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu ambapo siku ya mwisho aliitumia kikamilifu kukutana na taasisi za umma za biashara na viwanda, Benki ya Exim ya Korea pamoja na makampuni binafsi yanayojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Amesema kuwa miaka 25 ya kwanza ya uhusiano wetu na Jamhuri ya Korea ilijikita kwenye kuweka misingi imara ya uhusiano wa kidiplomasia ambapo nchi zetu zilikuwa zinajiimarisha kama mataifa huru. “Sasa ni wakati wa kushamiri kiuchumi tuone sekta binafsi zinavyoshiriki katika kukuza uchumi, wananchi wa Tanzania waje kwa wingi nchini Korea kujifunza masuala ya teknolojia, uhandisi na hata usanifu na ubunifu. Huu ndio uhusiano wenye tija kwa mataifa yetu”. Mheshimiwa Waziri alisema.

Akizungumza na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea, Mheshimiwa Mahiga mbali na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kutoa mikopo na misaada nchini Tanzania, Waziri Mahiga alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli sasa imejikita kwenye mapambano dhidi ya rushwa na ujenzi wa viwanda ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu. Kwasasa Benki hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji mikoa mbalimbali ya Tanzania ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mahiga alifafanua kuwa ajenda ya Mheshimiwa Magufuli ya viwanda, haiwezi kukamilika bila kuwa na miundombinu ya msingi kama vile uzalishaji wa umeme wa kutosha na ukuaji wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano ambapo Korea Kusini ni wabobezi kwenye masuala hayo.

Alitumia fursa hiyo kumkaribisha Bw. Chang na timu yake kwenda Tanzania kufanya tathmini ya miradi tunayoshirikiana nao, lakini pia miradi mipya kwenye sekta ya uchukuzi kama ujenzi wa Standard Railway Gauge “SRG” kutoka Isaka hadi Kigali, n.k. ambayo ni miradi ya kipaumbele kwa sasa kwa taifa letu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Chang alisifu utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli, na Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania na kusema kuwa utendaji kazi wa aina hii ni wa kupigiwa mfano barani Afrika, na umekuja wakati muafaka tunapoingia kwenye hatua nyingine ya uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi zetu mbili. Aidha aliongeza kuwa, wakati umefika sasa wa kufanya kazi, nay eye yuko tayari kufanya kazi na Tanzania kwani Serikali yake, imetoa kipaumbele kwa nchi hii.  

Korea Exim Bank ni taasisi ya Serikali inayosimamia mikopo na misaada ya Jamhuri ya Korea inayotoa kwa nchi nyingine. Katika kipindi cha miaka minne (tangu 2016 hadi 2020), Korea Kusini kupitia taasisi hiyo, imeongeza mikopo ya maendeleo kwa bara la Afrika kwa asilimia 20. Uamuzi wa Serikali iliyokuwa madarakani mwaka 2016 wa kuichagua Tanzania kupokea kiasi kikubwa cha msaada huo kuliko nchi nyingine ya Afrika, umeendelezwa na Serikali iliyopo sasa madarakani ya Mheshimiwa Moon Jae-in, Rais wa Jamhuri ya Korea.

Ujumbe wa Mheshimiwa Augustine Mahiga pia ulikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Judong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya Korea (Korea Chamber of Commerce and Industries KCCI), ambapo Waziri Mahiga aliwasisitiza kuja Dar es salaam kuangalia fursa zilizopo ili kuwashawishi wanachama wao kutafuta bidhaa na masoko nchini Tanzania.

Akielezea umuhimu wa KCCI kuzuru Tanzania na kujifunza soko la biashara, Bw. Edwin Rutageruka Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE aliyeongozana na ujumbe wa Mheshimiwa Waziri Mahiga, alisema njia nzuri ya kupata picha halisi ni kupitia  Maonesho ya Biashara ya Saba Saba. Hivyo alitumia fursa hiyo kualika ujumbe wa KCCI kushiriki kwenye maonesho ya 42 yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 Juni – 10 Julai, 2018.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mheshimiwa Mahiga pia alikutana na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa makampuni ya DOHWA, ambao wamejikita kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli n.k. Makampuni mengine ni KORAIL, STX Engine, KTMI & STX Offshore pamoja na GS E&C, ambao wote wameonesha nia ya kuwekeza au kufanya biashara nchini Tanzania. Ujumbe mkuu kwa taasisi na makampuni hayo ulikua ni kupanua fursa za ushirikiano wa biaashara na uwekezaji, ubadilishanaji wa ujuzi na ujengaji uwezo wa wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu.

Pamoja na kuzungumza na makampuni ya umma na sekta binafsi yaliyoorodheshwa hapo juu, ziara ya Mheshimiwa Augustine Mahiga, ilimuwezesha kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ambapo alihutubia mamia ya wafanyabiashara wa Korea kuhusu utayari wa Tanzania kushirikiana na nchi hiyo kibiashara.

Mkutano huo uliopewa kauli mbiu ya “Eplore Tanzania” ulifuatiwa na mikutano midogo midogo iliyowakutanisha baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini ili kuangalia kwa ukaribu maeneo ya ushirikiano. Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini na mwenzake wa Korea Kusini nchini Tanzania wameazimia kuendeleza makongamano hayo ya kila mwaka ili kuwa na ushirikiano wa karikiano wa karibu wa kibiashara kwa mataifa hayo mawili kwa maendeleo ya wananchi wote.  

Wajumbe wengine walioongozana na Mheshimiwa Waziri Mahiga nao walipata fursa ya kuhutubia hadhara hiyo kuhusu Tanzania ambapo Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Investment Centre alitoa utangulizi kuhusu uwekezaji Tanzania; Kanali (mstaafu) Joseph Simbakalia, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA alizungumzia maeneo ya kipaumbele kwenye maeneo maalum ya uwekezaji nchini Tanzania. Naye Bi. Nasriya Nassor, Mkurugenzi wa Promosheni wa Taasisi ya Uwekezaji Zanzibar alitoa taarifa fupi kuhusu Zanzibar kama kivutio cha utalii ndani ya Tanzania na eneo linalopendelewa na watalii wengi duniani.

Jamhuri ya Korea, kama inavyojulikana rasmi na Umoja wa Mataifa, ni mojawapo ya nchi zinazofanya vizuri zaidi duniani kiuchumi kwa sasa. Viashiria vya uchumi vinaonyesha uchumi wa nchi hiyo utaendelea kukua kwa viwango kutokana na jitihada za dhati za viongozi wa nchi hiyo za kufuta kabisa umaskini kwa wananchi wao. Kwa sasa wastani wa pato kwa mtu “per capital income” inakadiriwa kuwa zaidi ya US$ 34,000, ukilinganisha na US$ 22,670 mwaka 2012. Baada ya vita ya Korea kwenye miaka ya mwanzo ya 1950, nchi ya Korea Kusini ilikua maskini kuliko nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania ambapo wastani wa pato kwa mtu ilikua na US$67.

Mheshimiwa Mahiga anatarajiwa kurejea nyumbani baada yakuhitimisha ziara hiyo aliyosema italeta faida sio tu kwa wafanyabiashara, ila kwa jamii kwa ujumla. Nchi hii ni tajiri sana kiuchumi; lakini utajiri wake mkubwa pia uko kwenye taaluma ya rasilimali watu, hivyo kwa Tanzania kufanikiwa kufungua ubalozi hapa, sasa tumefungua milango ya ushirikiano wa karibu, kuliko ilivyokuwa mwanzo. Tuchangamke tuige mfano wa uchapa kazi wao, na sisi tutaondoka kwenye umasikini Waziri Mahiga alisema kwa kumalizia, kabla ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon, uliopo mjini Seoul, Jamhuri ya Korea.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul, Korea Kusini,
3 Februari 2018.


Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri Mahiga nchini humo. 

Exim Bank Business Meeting 4: Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini. 

 Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI).  

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI). Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda Masuka.  

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimkabidhi zawadi ya majani ya chain a kahawa za Tanzania Bw. Choi Jong-won, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Dong Myeong ya Korea Kusini.  


Thursday, February 1, 2018

Waziri Mahiga Afungua Kongamano la Kwanza la Biashara Jamhuri ya MheKorea

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia mamia ya wafanyabiashara waliofurika kwenye Ukumbi wa Hana kuhudhuria Kongamano la Kwanza la Biashara lililofanyika Mjini Seoul Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari, 2018.
Mheshimiwa Matilda Masuka Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Jamhuri ya Korea akitoa neno la ukaribisho wakati wa Kongamano la Kwanza ambalo liliandaliwa na Ubalozi wa Tanzania. 


Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, akitoa taarifa kuhusu mazingira ya uwekezaji Tanzania na fursa zinazoweza kupatikana kwa wawekezaji wa Korea Kusini iwapo wataamua kuja kuwekeza Tanzania.

Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries akishuka kutoka kwenye eneo la kuhutubia ambapo alitoa mwelekeo wa biashara baina ya Korea Kusini na Afrika na hatimaye fursa za kufunguka biashara na uwekezaji baina ya Korea Kusini na Tanzania. Alisihi wanachama wa taasisi hiyo kongwe ya biashara nchini humo, kuangalia Tanzania kama mshirika imara kiuchumi barani Afrika.


Bw. Masuka, ambaye ni mume wa Mheshimiwa Balozi Matilda Masuka akiendesha kongamano hilo ambapo mwanafunzi Mtanzania anayesoma Seoul, akitafsiri kwa lugha ya Kikorea.

Mheshimiwa Waziri Mahiga akiwa kwenye meza kuu kabla ya Kongamano kuanza.



Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania akitoa mada wakati wa Kongamano hilo lililofanyika Jijini Seoul Korea Kusini tarehe 31 Januari 2018.

Kanali (Mstaafu) Joseph Simbakalia, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA Eneo Maalum la Uwekezaji, akitoa mada wakati wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea. Kongamano hilo lilifanyika sambamba na ufunguaji rasmi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo tarehe 31 Januari, 2018.