TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Mambo ya Nje imejipanga kutekeleza
Sera ya Uchumi wa Viwanda
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza
malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Kauli hiyo ilitolewa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi
kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Waziri Mahiga alieleza kuwa Wizara inatakiwa
kuweka Sera na mikakati ya utekelezaji kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya
Viongozi wa juu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli.
“Sera ya Serikali ya awamu ya tano ni kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda, hivyo Sera yetu ya Mambo ya Nje lazima ijikite
katika diplomasia ya uchumi wa viwanda”. Dkt. Mahiga alieleza.
Dkt.
Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka watumishi kuhakikisha kuwa Wizara inatekeleza
majukumu yake kwa kujiwekea ratiba ya kuyakamilisha kwa kuzingatia hotuba za
Mhe. Rais Magufuli alizozitoa wakati wa
ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikao cha Mabalozi na
Mhe. Rais Magufuli na kikao cha watumishi wa Wizara na Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amesema
kuwa Wizara yake imejipanga ipasavyo kuhakikisha kwamba jukumu la
kuchochea uchumi wa nchi kupitia Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika
diplomasia ya uchumi inatekelezwa kikamilifu.
Prof. Mkenda alisema Wizara kwa kushirikiana na
ofisi zake za Ubalozi, licha ya changamoto mbalimbali inazokutana nazo, lakini
imekuwa ikitafuta fursa za uwekezaji, mitaji, masoko, utalii na elimu na
kuzileta nchini ili kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa
nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020.
Alizitaja Balozi chache zilizoleta
wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji nchini
kuwa ni pamoja na Balozi za Tanzania nchini China, Ufaransa, Korea
Kusini, Kenya, Ujerumani na Israel. "Balozi wetu China, Mhe. Mbelwa
Kairuki ametafuta taasisi za kifedha kwa ajili ya kuzikopesha benki za Tanzania ili zikuze mitaji
ya kutoa mikopo kwa wawekezaji. Aidha, Serikali ya Ujerumani imefungua ofisi
maalum kwa ajili ya kuratibu na kusaidia shughuli za kibiashara na uwekezaji
hapa nchini" Prof. Mkenda alisema.
Prof. Mkenda alisifu jitihada zilizofanywa na
Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya hivi karibuni za kuandaa maonesho ya bidhaa za
viwanda vya hapa nchini yaliyofanyika jijini Nairobi tarehe 25 - 28 Aprili
2018. Alisema maonesho hayo ya kipekee yalikuwa na mafanikio makubwa ambapo
wafanyabiashara walioshiriki waliingia makubaliano na wafanyabiashara wa Kenya
ya kupeleka bidhaa zao nchini Kenya.
"Tunatakiwa tuondoe vikwazo vya kufanya
biashsra, kuondoa vikwazo hivyo haina maana Tanzania iwe gulio la kuuzia bidhaa
kutoka nje, bali wafanyabiashara wetu wanatakiwa kuchangamkia masoko ya nje ili
wauze bidhaa zao kwa wingi nje ya nchi", Katibu Mkuu alisisitiza.
Katibu Mkuu alisema ili watumishi waweze kutimiza
malengo ya Wizara yakiwemo ya kuvutia wawekezaji kutoka nje, Wizara imejipanga
kuwawezesha watumishi kupata elimu, ujuzi, teknolojia na uzoefu unaohitajika
kutimiza majukumu hayo.
Kuhusu suala la kupeleka watumishi kwenye vituo
vya Ubalozi, Katibu Mkuu alieleza kuwa Wizara itatekeleza jukumu hilo kwa haki
kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa ambavyo ni weledi, ujuzi na mahitaji ya
Balozi husika. “Wizara haitapeleka watumishi vituoni kutokana na shinikizo au
kuangalia sura, kabila na dini ya mtu ili kuondoa malalamiko yaliyokuwepo kwa
muda mrefu Wizarani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
05 Mei, 2018
|