Saturday, January 26, 2019

Mawaziri wa Tanzania na Uganda wajadili Ujenzi wa Bomba la Mafuta

Ujumbe wa Tanzania uliokwenda nchini Uganda kwa ajili ya ya mkutano wa majadiliano ya ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghfi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga, ujumbe huo kutoka kulia ni Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Mhe. William Lukuvi(Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb), Waziri wa Nishati; Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria na Mhe. Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Uganda. 
Mkutano wa Bomba la Mafuta ghafi ulifanyika Kampala Uganda kuanzia tarehe 21 hadi 25 Januari 2019. Mkutano huo ulianza kwa ngazi za Wataalam, Makatibu Wakuu na kuhitimishwa kwa ngazi ya Mawaziri. Mkutano ulienda vizuri na upo katika hatua nzuri ya majadiliano ili kuanza utekelezaji. Pande zote mbili zimekubaliana mambo mbalimbali ya msingi ambayo.yanafungua na kuandaa njia za utekelezaji wa Mradi.

Mhe. Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Uganda (kushoto) akiwa katika kikao cha wataalamu cha kujadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akichangia jambo katika mkutano huo.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mkutano huo kumalizika. kushoto kwake ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya adini wa Uganda, Mhe. Irene Muloni.

Tanzania na Bosnia na Herzegovina Kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kulia) na Mwakilishi wa Kudumu wa Bosnia na Herzegovina katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ivica Dronjic wakiweka saini Makubaliano ya kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bosnia na Herzegovina. Makubaliano hayo ambayo yatazingatia Mkataba wa Vienna wa masuala ya mahusiano ya kidiplomasia wa Mwaka 1961 uliwekwa saini New York, Marekani tarehe 25 Januari 2019.  
Afisa wa Ubalozi, Bibi Lilian Mukasa akitoa maelekezo ya namna Waheshimiwa Mabalozi watakavyosaini Makubaliano ya kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi zao.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kulia) na Mwakilishi wa Kudumu wa Bosnia na Herzegovina katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ivica Dronjic wakibadilishana Nyaraka ya Makubaliano baada ya wawili hao kuweka saini.




Friday, January 25, 2019

Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India
Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini zimeshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 nchini India yajulikanayo kama OTM 2019 [Outbound Travel Mart-2019] kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za soko la utalii nchini humo.
Maonesho hayo maarufu na makubwa kabisa katika ukanda wa Asia-Pasifiki yalianza tarehe 23 Januari, 2019 na yamemalizika leo tarehe 25 Januari, 2019, Maonesho haya hufanyika kila mwaka katika Jiji la Mumbai na kushirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani.
Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Kituo cha Kutangaza Utalii wa Zanzibar India [Zanzibar Tourism Promotion Centre]. Kwa upande wa kampuni binafsi ni Leopard Tours, Zara Tours, Ngarawa Hotel and Resort, DOTCOM Safaris Ltd na Jackal Adventures.
Katika Maonesho hayo, Banda la Tanzania limeibuka Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award].
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda amesema kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya utalii walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Washiriki wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na kufanya biashara.
Akiwa katika maonesho hayo, Balozi Luvanda alieleza kuwa maonesho yalisaidia washiriki kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida zake. Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Tunategemea idadi ya watalii kutoka India wanaokwenda Tanzania itaongezeka mara dufu baada ya kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] moja kwa moja kutoka Tanzania kuja India ambapo zinategemewa kuanza kabla ya mwezi wa Juni 2019.

‘Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award]”, alisema Balozi Luvanda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
25 Januari 2019
Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Utalii wa India, Mhe. K. J. Alphons akiwa katika banda la Tanzania. Kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiwa na washiriki wengine katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 23 Januari, 2019

Picha ya pamoja ya washiriki baada ya kupokea Tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa Banda bora la maonesho lilipambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The Winner of Best Decoration Award] katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 25 Januari, 2019.

Wageni mbalimbali wanatembelea banda la Tanzania ili kupata maelezo kuhusu vivutio vya utalii nchini.

Wageni katika banda la Tanzania wakipata maelezo kuhusu fursa na vivutio vya utalii nchini.




Naibu Waziri awasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa majukumu kwa Kamati ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Kipindi cha Julai hadi Desemba, 2018 mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) (hawapo pichani) kilichofanyika kwenye Ofisi za Bunge, Dodoma tarehe 25 Januari, 2019. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Mhe. Mussa Azan Zungu akizungumza wakati wa kikao kati ya Wajumbe wa Kamati ya NUU na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kulia ni Katibu wa Kamati
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Salum Mwinyi Rehani akichangia jambo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto ni Mhe. Ruth Mollel, Mjumbe wa Kamati hiyo.
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Fakharia Shomar Khamis nae akichangia hoja wakati wa kikao kati ya Kamati ya NUU na Wizara
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi kutoka Wizarani wakifuatilia kikao


Wakurugenzi kutoka Wizarani wakisoma nyaraka mbalimbali wakati wa kikao

Juu na chini ni Wakurugenzi kutoka Wizarani
Wajumbe wa Kamati ya NUU wakifuatilia kikao
Kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Prosper Mbena akichangia jambo wakati wa kikao
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Janeth Masaburi nae akichangia jambo
Mhe. Mboni Mhita ambaye ni Mjumbe wa Kamati akitoa ushauri kwa Wizara kuhusu kuboresha masuala mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi


Mjumbe wa Kamati ya NUU, Mhe. Shamsi Vuai Nahodha nae akizungumza
Wajumbe wa Kamati wakifuatilia kikao
Watumishi kutoka Wizarani wakifuatilia kukao

Thursday, January 24, 2019

Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya heshima nchini India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan akitunukiwa Tuzo ya Juu (Pravasi Bharatiya Samman Award ) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind tarehe 23 Januari, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu wa Mauritius, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh nchini humo.
Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind akihutubia katika hafla ya kuhitimisha Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India [15thPravasi Bharatiya Divas 2019] uliofanyika tarehe 23 Januari, 2019 katika mji wa Varanasi, Uttar Pradesh nchini India 
Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkubwa wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh, India
Picha ya pamoja



Mama Shamim Khan katika picha ya pamoja na Afisa Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Dkt. Kheri Goloka baada ya kupokea Tuzo tarehe 23 Januari, 2019.
=======================================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Yah: Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya juu ya heshima na Mhe. Ram Nath Kovind, Rais wa India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima (Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India (15th Pravasi Bharatiya Divas 2019) uliofanyika kwenye mji wa Varanasi, Uttar Pradesh tarehe 23 Januari, 2019.

Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi  uliwahusisha viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya India akiwemo Waziri Mkuu wa Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Sushma Swaraj, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje ya India, Mhe. Gen [Dr.) V. K. Singh na Waziri Kiongozi wa Jimbo la Utter Pradesh, Mhe. Yogi Adityanath.

Mama Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii hususan katika masuala ya akina mama na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini. 

Wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind alieleza kutambua mchango mkubwa wa Mama Shamim Khan katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na Serikali ya Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zao. Aidha, alimpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake, Mama Shamim Khan alimshukuru sana Rais Kovind na kueleza kufarijika kwake kwa kutunukiwa Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake. Aidha, Mama Shamim Khan alipongeza juhudi za Serikali ya India kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na India na amemuomba Mhe. Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za Serikali ya Mhe.Rais Dkt. John P. Magufuli katika kuwaletea maendeleo watanzania.

Tuzo hiyo hutolewa kwa raia wenye asili ya India ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mama Shamim Khan bali kwa Tanzania kwa ujumla.  Mama Shamim Khan aliongozana na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dkt. Kheri Goloka kwenye hafla hiyo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
24 Januari 2019





Wednesday, January 23, 2019

Balozi wa Tanzania, Ujerumani awasilisha hati za utambulisho nchini Bulgaria

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye anawakilisha pia nchini Bulgaria , Mhe. Dkt. Abdallah Posi akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Bulgaria, Mhe. Rumen Radev. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya nchi hiyo hivi karibuni.
Mhe. Balozi Dkt. Posi akizungumza na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho
Mhe. Balozi Dkt. Posi akiagana na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho


Mhe. Balozi Dkt. Posi akiwa mbele ya gwaride la heshima alipowasili Ikulu ya Bulgaria kwa ajili ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa nchi hiyo.

Thursday, January 17, 2019

Tanzania kushiriki Maonesho ya Biashara ya Dunia ya EXPO 2020


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania kushiriki Maonesho ya Biashara ya Dunia ya EXPO 2020

Tanzania itashiriki Maonesho ya Dunia ya Biashara (Expo 2020 yatakayofanyika Dubai kuanzia mwezi Oktoba 2020 na kumalizika mwezi April 2021.

Uwekaji saini wa Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho hayo ulifanywa tarehe 16 Januari 2019 na Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk.

Kwa upande wa UAE, mkataba huo uliwekwa saini na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo, Mhe. Balozi Mbarouk alieleza kuwa Serikali inayapa umuhimu mkubwa maonesho hayo kwa kuwa ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kwenye sekta za uwekezaji, biashara, viwanda, utalii na mila na utamaduni.

Aidha, Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020 alieleza kuwa amefurahishwa na hatua ya Tanzania kusaini Mkataba huo ambapo itatoa fursa kwa nchi kujiandaa mapema na taratibu nyingine za ushiriki.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo,` kitakachofuata ni utayarishaji wa simulizi ya maudhui ya maonesho (pitch story) ambayo inatakiwa kuthibitishwa na Kamati ya Kitaifa ya Tanzania ya DUBAI Expo 2020. Simulizi ya maudhui hayo yatahusu vipaumbele vya Tanzania kama vile maendeleo ya viwanda, miundombinu, masuala ya biashara na uwekezaji, utalii, kilimo, elimu, afya, sanaa na utamaduni.  Simulizi ya maudhui pia itatumika katika kusanifu muonekana wa banda la maonesho la Tanzania.

Tanzania inakuwa miongozi mwa nchi washiriki zipatazo 100 ambazo tayari zimesaini Mkataba wa Ushiriki tangu Dubai ilipochaguliwa kuwa mwenyeji wa maonensho hayo.

Wengine walioshuhudia uwekaji saini wa Mkataba huo ni Bw. Ali Jabir Mwadini, Kansela Mkuu, Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai; Bi Samira Ahmed Diria, Afisa Ubalozi; na kwa upande wa DUBAI EXPO 2020 ni  Bi Manuela Garcia Pascual, Mkurugenzi wa Washiriki wa Kimataifa na Bi. Esther Omondi, Meneja wa Nchi/Afisa dawati la Tanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
17 Januari 2019

Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakiweka saini Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Dunia (Dubai Expo 2020. Uwekaji saini huo ulifanyika Dubai tarehe 16 Januari 2019.  
Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakionesha Mkataba mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.
Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wao.

Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakibadilishana mawazo mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.

Wednesday, January 16, 2019

DKT. NDUMBARO ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO UBALOZI WA NIGERIA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) akisaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Nigeria hapa nchini kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Alhaji Shehu Shagari kilichotokea tarehe 28 Desemba 2019. Dkt. Ndumbaro alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Dkt.Sahabi Isa Gada. Tukio hilo limefanyika jijini Dar Es Salaam katika Ubalozi wa Nigeria hapa nchini.  
Balozi Gada akimwelezea jambo Dkt. Ndumbaro wakati wa mazungumzo.
Sehemy ya Maafisa wa Ubalozi wa Nigeria nchini wakisikiliza kwa makini mazungumzo kati Dkt. Ndumbaro na Balozi Gada (hawapa pichani).
Dkt. Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Gada na maafisa wa Ubalozi huo.
Dkt. Ndumbaro akiagana na Balozi Dkt. Gada. 





Balozi wa Italia atembelea Wizara ya Mambo ya Nje


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni. Wawili hao walijadiliana umuhimu wa kuibua maeneo mapya ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia hussusan katika sekta ya biashara na uwekezaji.  Dkt. Mahiga alitumia fursa hiyo pia kueleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Balozi Mengoni akimwelezea jambo Dkt. Mahiga


Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Magabilo Murobi pamoja na Bi Happyness Lwangisa wakifuatilia na kunukuu mambo muhimu ya mazungumzo hayo.