TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MABALOZI WA TANZANIA WATEMBELEA MRADI MKUBWA UMEME WA JULIUS
NYERERE
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kubuni, kutekeleza na kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mabalozi hao kutoka nchi 42 za uwakilishi duniani kote wametoa pongezi hizo tarehe 14 Agosti 2019 walipoutembelea mradi mkubwa wa kufua umeme wa Julius Nyerere uliopo Wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Akizungumza na Vyombo vya Habari kwa niaba ya Mabalozi wengine, Kiongozi wa Mabalozi hao, Mhe. Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Umoja wa Afrika amesema kuwa Serikali ya Awamu ya tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ya kupigiwa mfano kwa hatua kubwa iliyofikiawa katika maendeleo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake.
"Kwa dhati na kwa heshima kubwa tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua hizi kubwa za maendeleo ikiwemo kubuni na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa mengi kwa nchi yetu. Sisi mabalozi tunaoiwakilisha Tanzania nje tunaona fahari na tunajivunia kuwa na Rais mchapakazi na tunatembea kifua mbele tunapoiona miradi mikubwa kama hii ikitekelezwa ndani ya nchi yetu”, amesema Balozi Aziz.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Abdallah Possi alieleza kuwa Mabalozi wanaunga mkono jitihada hizi za Serikali na wapo tayari kuendelea kusaidia jitihada hizo ikiwa ni pamoja na kuwaleta nchini wawekezaji na wataalam wenye tija kwa taifa.
Akiwasilisha mada kuhusu mradi huo wa Julius Nyerere utakaozalisha umeme wa Megawatt 2115 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Stephen Manda amesema kuwa mradi huo ambao ni wa nne kwa ukubwa barani Afrika na wa kwanza Afrika Mashariki utakamilika ifikapo mwaka 2022.
Aliongeza kusema kwamba, mradi huo unasimamiwa na watanzania kwa asilimia mia moja na kugharamiwa na Serikali ambapo kiasi cha shilingi trilioni 6.5 zimetengwa kukamilisha mradi huo. Kati ya fedha hizo tayari Serikali imewalipa wakandarasi wa mradi huo ambao ni Kampuni za Arab Contractors na Elsewedy Electric za nchini Misri kiasi cha shilingi trilioni 1.7 ambayo ni asilimia 15 ya fedha zote za mradi huo.
Akielezea faida za mradi huo Mhandisi Manda alisema zipo za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Kiuchumi mradi huo utaongeza uzaishaji viwandqni kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika na hivyo kuzalisha ajira kwa vijana. Pia mradi huo utakuza utalii kutokana na maeneo pembezoni mwa bwawa hilo kuwa na nafasi ya kujengwa hoteli na fukwe za kupumzikia. Kijamii Mhandisi Manda amesema kuwa, mradi huo hadi sasa umewawezesha wananchi wa Rufiji kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa uhakika kama vile maji, umeme kutokana na mradi huo kupita kwenye eneo lao.
Kuhusu utunzaji mazingira, Mhandisi Manda alieleza kuwa, tahmini ya kina kuhusu mazingira yanayozunguka mradi huo imefanywa na kuwaomba Mabalozi kusaidia kutoa elimu zaidi ili kufuta dhana inayoenezwa kuwa mradi huo utaharibu mazingira. Alifafanua kuwa, Mradi huu pamoja na mambo mengine utachangia utunzaji mazingira kwa kiasi kikubwa kwenye eneo lotelinalouzunguka kwani kutokana na umeme utakaozalishwa wananchi hawataendelea kukata miti kwa ajili ya nishati ya kuni. Pia mradi huo utasaidia kutunza mazingira ya eneo hilo kwa kudhibiti mafuriko yaliyokuwa yanatokea kwenye ukanda wa eneo hilo.
Mradi huo mkubwa wa umeme ulibadilishwa jina na kuitwa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere wakati wa uwekwaji wa jiwe la msingi uliofanywa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Julai 2019 ili kuenzi maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa na ndoto ya kujenga bwawa hilo wakati wa utawala wake.
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi wapo nchini kuanzia tarehe 14 hadi 22 Agosti 2019 kwa ajili ya kushiriki Kikao Kazi chao Maalum pamoja na Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serial,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
15 Agosti 2019
|
Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, (wakwanza kushoto) akifuatilia uwasilishwaji wa taarifa ya hatua za maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa bwawa la Julius Nyerere (2115MW) unaotekelezwa na Serikali wilayani Rufiji.
|
|
Mabalozi wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi katika mataifa mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara na Wafanyakazi wa Mradi ,katika moja ya njia ya chini (tunnel) katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere lililopo katika hifadhi ya Selous wilayani Rufiji. Mabalozi walitembelea maradi huo kujionea hatua mbalimbali za maendeleo ya utekelezaji. Mradi huu unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano unatarajia kuzalisha Megawati 2115 baada ya kukamilika kwake mwaka 2022.
|
|
Mhe. Nahim Azizi Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia akizungumza mara baada ya kuwasili eneo la ujenzi wa mradi |
|
Mabalozi wakisikliza maelezo kuhusu ujenzi wa mradi kutoka kwa Mhandisi Stevene Manda |
|
Mabalozi wakisikiliza hotuba fupi ya ukaribisho kutoka Mhe. Juma Abdallah Njwayo Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi |