Monday, September 7, 2020

PROF. KABUDI AMUAGA BALOZI WA IRAN NCHINI TANZANIA

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amemuaga Balozi wa Iran nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Akiongea katika hafla ya kumuaga balozi wa Iran iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi amempongeza Balozi Farhang kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yake na Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amemuahidi Balozi Farhang kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Iran katika sekta za elimu, afya na utalii kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania nakuahidi ushirikiano kutoka kwetu, nakutakia kila la kheri katika maisha yako nje ya Tanzania na ni imani yangu kuwa utakuwa balozi mzuri wa Tanzania duniani," Amesema Prof. Kabudi

Kwa upande wake Balozi Farhang ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Balozi Farhang ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya Iran na Tanzania na amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Balozi wa Iran Mhe. Mousa Ahmed Farhang akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati alipokuwa anamuaga baada ya kumaliza muda wa uwakilishi nchini 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Iran aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro, Balozi wa Iran aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang

Saturday, September 5, 2020

PROF. KABUDI, BALOZI IBUGE WASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO KUFUTIA KIFO CHA RAIS WA ZAMANI WA INDIA

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wamesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa India nchini kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa Taifa hilo Shri Pranab Mukherjee kilichotokea tarehe 31 Agosti 2020.

 Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi ubalozi wa India nchini, Jijini Dar es Salaam Prof. Kabudi ametoa pole kwa wananchi wote wa India na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu na wastahimilivu wakati huu wa msiba wa kiongozi wao mstaafu.

 "Kusaini kitabu cha maombolezo ni ishara ya ushirikiano wetu, umoja wetu na undugu wetu na ndugu zetu wa India. Kifo cha Rais Shri Pranab Mukherjee kinawahusu pia watanzania kwa sababu Tanzania na India zina uhusiano mzuri, imara na wa muda mrefu ulianzishwa na baba wa Taifa Mwl. Julias Nyerere pamoja na Mahatma Gandhi,” amesema Prof. Kabudi

 Rais Shri Pranab Mukherjee ni miongoni mwa viongozi wa zamani wa India waliowahi kufanya kazi katika Serikali ya Waziri Mkuu wa Zamani Indira Gandhi aliyewahi kukabidhiwa nyadhifa mbali mbali ikiwemo Waziri katika Sekta tofauti.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa India nchini Tanzani. Pembeni yake kulia ni Balozi wa India nchini Mhe. Shri Sanjiv Kohli  


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa India nchini Tanzania

 

Friday, September 4, 2020

TZ YAIHAKIKISHIA UINGEREZA NA JUMUIYA YA KIMATAIFA UCHAGUZI HURU, HAKI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeihakikishia Uingereza pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa uchaguzi mkuu unaotegemewa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2020 utafanyika kwa amani, uhuru na haki.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar   

Prof Kabudi amesema kuwa paamoja na mambo mengine, amemhakikishia balozi mteule wa Uingereza nchini Mhe. Concar kuwa mchakato wa uchaguzi nchini unaendelea vizuri sana ambapo mikutano ya kampeni imeanza kwa ngazi zote (ngazi ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani) na mpaka sasa kampeni zinaendea vizuri.

"kama ilivyoada ya watanzania nimemhakikishia kuwa uchaguzi huu utafanyika kwa amani na utulivu na mwisho wa siku maamuzi yatakayotolewa na watanzania ya kuamua nani awe diwani, nani awe mbunge na nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yataheshimiwa na watanzania wote," Amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi mteule Mhe.David Concar amesema kuwa katika maongezi yao mbali na kugusia suala la uchaguzi pia wameongelea namna ya kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Uingereza na mazingira bora ya kuvutia zaidi wawekezaji kuja nchini,kukuza biashara hususani baada ya Uingereza kujitoa katika jumuiya ya Umoja wa Ulaya na pia kusaidia maendeleo katika maeneo ya afya,maji pamoja na elimu.

Katika hatua nyingine Prof. Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Pakistan hapa Nchini Mhe. Mohamed Saleem.

Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi amesema kutokana na Pakistan kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika viwanda vya mbolea wamekubaliana kuangalia namna ya kushirikiana ili kujenga viwanda vingi vya mbolea hapa nchini pamoja na kufanya biashara ya moja kwa moja ya zao la chai badala ya kupitia katika masoko ya minada ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Balozi wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim amesema atahakikisha kuwa Tanzania na Pakistan zinaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zote mbili ili kuweza kunufaika na furza za kukuza uchumi.

Hafla ya mabalozi wateule kukabidhi hati za utambulisho pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge.  

Balozi mteule wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam

Balozi mteule wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi 


Balozi mteule wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim 



Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge (kulia) akifuatilia maongeza mara baada ya Mabalozi wateue kuwasilisha hati za utambulisho kwa Waziri Prof. Kabudi  

Naibu Katibu Mkuu aongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye majadiliano ya biashara baina ya EAC na Uingereza

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Mwinyi Talib Haji akifuatilia kikao cha  kuajadili namna bora ya kuendelea na majadiliao ya biashara baina ya Afrika Mashariki na Uingereza kilichokuwa kikiendelea kwa njia ya mtandao (Video Conference).

Dkt. Haji ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikoa cha Kanda cha Makatibu Wakuu wa Jamuiya ya Afrika Mashariki kujadili namna bora ya kuendelea na majadiliano ya biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Uingereza.

Lengo la majadiliano baina ya Afrika Mashariki na Uingereza ni kuwa na Mkataba wa Biashara utakaowezesha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuuza bidhaa kwenye Soko la Uingereza na Uingereza kwenye Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia tarehe 01 Januari, 2021.

Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu imekuwa mshirika mzuri wa biashara kwa nchi ya Uingereza. Hata biashara hiyo biashara hiyo awali imekuwa ikifanyika kwa kufuata sheria, miongozo na taratibu za Umoja wa Ulaya. Kufauatia hatua ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya imeenda sera na mwongozo mpya utakao  ifanya nchi hiyo kuendelea kufanya biashara na Mataifa mbalimbali. 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji akiachangia  hoja wakati wa kikao.
Kikao kikiendelea 

Tanzania kuwania nafasi ya Ujumbe wa Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju amemnadi mgombea wa Tanzania anayewania nafasi ya ujumbe kwenye Kamati ya Ushauri ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for Commodities – CFC) alipotembelea Ofisi za Mfuko huo zilizoko mjini Amsterdam, Uholanzi tarehe 02 Septemba, 2020.

Balozi Kasyanju alikwenda CFC kufanya mazungumzo na pia kumpongeza rasmi Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe. Balozi Sheikh Mohammed Belal kwa kushika nafasi ya kuiongoza CFC kwa kipindi cha miaka minne, kazi aliyoianza rasmi mwezi Aprili 2020 baada ya kuchaguliwa kwa kauli moja kushika wadhifa huo wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Baraza la Uongozi la CFC uliofanyika tarehe 04 Desemba 2019. Katika mazungumzo yao Balozi Kasyanju alimhakikishia Mwenyeji wake huyo ushirikiano wa Tanzania kwa Taasisi yake na kutoa shukrani za dhati kufuatia mikopo yenye riba nafuu iliyotolewa kwa ajili ya kuboresha miradi mitatu inayoendelea hivi sasa nchini Tanzania.

Balozi Kasyanju aliitumia fursa hiyo sawia kumnadi mgombea wa Tanzania, Dkt. Jacqueline David Mkindi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa “Tanzania Horticultural Association (TAHA)” iliyoko mjini Arusha. Balozi Kasyanju alimuelezea Dkt. Mkindi kuwa ni kiongozi mahiri na mchapa kazi na akadhihirisha kwamba endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo ataiwakilisha vema Tanzania kwa kuwa mshauri bora na makini kwa CFC na Nchi zote Wanachama wa CFC na hivyo kuleta mwamko mpya kwenye Taasisi hiyo muhimu.

CFC iliundwa mwaka 1989 kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuboresha na kuleta maendeleo kwa jamii ya wakulima na wazalishaji wa bidhaa katika Nchi Zinazoendelea. Hivyo basi, CFC imejikita katika kutoa ufadhili wa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake zinazotokana na michango ya hiari ya Nchi Wanachama na Wafadhili.

Tanzania ni Mwanachama hai wa CFC na katika Taasisi hii inawakilishwa kwenye Baraza lake la Uongozi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kama Gavana; na Balozi wa Tanzania Nchini Uholanzi ambaye ni Gavana Msaidizi. Aidha, Tanzania imewahi kushika nafasi ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC na vile vile mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya CFC zaidi ya miaka 10 iliyopita. Hivyo, ni wakati mwingine muafaka kwa Tanzania kushika nafasi kwenye CFC hasa baada ya kutambua kwamba Mkurugenzi Mwendeshaji huyu mpya ameingia na nguvu mpya za kuleta mageuzi kwenye Taasisi yake na kuifanya iwe yenye tija zaidi kwa Wanachama wake.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea Taarifa ya Mwaka 2019 ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for Commodities – CFC) kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe. Balozi Sheikh Mohammed Belal, baada ya mazungumzo yao.

Balozi Irene Kasyanju akimkabidhi Mhe. Balozi Belal vipeperushi na majarida 20 yanayotangaza Utalii wa Tanzania yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kidachi kwa ajili ya kusambazwa kwa wadau.

Balozi Irene Kasyanju na Mhe. Balozi Belal wakiwa pamoja na wasaidizi wao Bi. Linda Mkony (kushoto), Mtumishi wa Ubalozi; na kulia ni Bw.Hector Besong, CFC Portfolio and Risk Manager.


 

Thursday, September 3, 2020

BALOZI WA TANZANIA NCHINI KENYA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS KENYATTA

 Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Stephen Simbachawene.

Hafla ya kuwasilisha hati za utambulisho imefanyika Ikulu jijini Nairobi ambapo pamoja na mambo mengine, Rais Kenyatta amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Balozi Simbachawene.   

Balozi Simbachawene amemhakikishia Rais Kenyatta kuwa ataendelea kuboresha mahusiano ya nchi hizo mbili za Tanzania na Kenya, kukuza biashara baina ya nchi hizo kwa kuboresha diplomasia ya uchumi kwa ujumla wake.  

Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta akiwa tayari kupokea hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Stephen Simbachawene 


Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Stephen Simbachawene

Wednesday, September 2, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AFANYA MAZUNGUMZO NA MRATIBU MKAZI WA UMOJA WA MATAIFA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini,
Bw. Zlatan Milišić
 alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 2 Septemba 2020.

Katika mazungumzo yao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa ambapo Balozi Ibuge alitoa shukrani kwa Shirika hilo kwa ushirikiano uliopo kati yake na Serikali hususan kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa upande wake, Bw. 
Milišić aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani na utulivu ambao ni chanzo cha uchumi wa nchi kustawi. Pia aliipongeza kwa kuendelea kuchangia vikosi vya ulinzi wa amani kwenye mataifa mbalimbali  yenye  migogoro duniani na kuitakia Tanzania uchaguzi wa amani na utulivu hapo mwezi Oktoba 2020.

Ujumbe wa Wizara ukimjumuisha Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bi. Prisca Mwanjesa, Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Ibuge na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Milišić (hawapo pichani)

Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Milišić mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge akiagana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Milišić mara baada ya mazungumzo kati yao.

 

Monday, August 31, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA KENYA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 31 Agosti 2020 kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye nyanja za diplomasia, biashara na uwekezaji. Pia Balozi Kazungu alitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya uchumi wa kati pamoja na kuongoza kwa mafanikio Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kadhalika aliitakia Tanzania uchaguzi wa amani na mafanikio hapo mwezi Oktoba 2020. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu

Sehemu ya ujumbe uliofuatana na Balozi Ibuge ukifuatilia mazungumzo. Kushoto ni Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Isaac Isanzu, Afisa Mambo ya Nje.

Balozi Dan Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha zinazowaonesha waasisi wa mataifa ya Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Uganda, Hayati Mzee Milton Obote. Balozi Ibuge alizipokea picha hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye aliahidiwa picha hizo na Serikali ya Kenya wakati wa ziara yake nchini humo mwezi Novemba 2019.

Mhe. Balozi Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha inayowaonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta. Picha hiyo ilipigwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Rais Kenyatta aliyoifanya hapa nchini mwezi Julai 2019.








 

Friday, August 28, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AZUNGUMZA NA BALOZI WA UBELGIJI NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Mhe. Peter van Acker. Mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kwa njia ya mtandao yalijikita kwenye kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji. Katika mazungumzo hayo, Balozi Ibuge aliishukuru Serikali ya Ubelgiji kupitia kwa Balozi huyo kwa ushirikiano mkubwa iliyoonesha kwa Tanzania katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID-19 na ushirikiano katika miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya maji kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 28 Agosti 2020 huku Balozi Ibuge akiwa jijini Dodoma na Balozi Peter van Acker akiwa jijini Dar es Salaam

Balozi Ibuge akimsikiliza Balozi Peter van Acker wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika kwa njia ya mtandao.

Balozi Ibuge akiwa na ujumbe aliofutana nao wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Mhe. Peter van Acker (hayupo pichani). Kulia ni Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Anthony Mtafya, Afisa Mambo ya Nje

Kikao kikiendelea

FURSA YA AJIRA KWA WATANZANIA - WHO, AUDA-NEPAD PAMOJA NA UN - HABITAT




 

Thursday, August 27, 2020

KATIBU MKUU BALOZI BRIGEDIA JENERALI WILBERT IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA ENG. STEVEN MLOTE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine Eng. Mlote alitoa taarifa fupi ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya Jumuiya ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara zinazoiunganisha nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, nishati na Vituo vya Kutoa Huduma Pamoja Mipakani (OSBPs)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote wakiwa katika mazungumzo. Wengine kutoka kulia ni Balozi Stephen P. Mbundi  Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama na Hangi Mgaka, Afisa Mambo ya Nje

Mazungumzo yakiendelea


Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Miundombinu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Kamugisha Kazaura, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo.

Thursday, August 13, 2020

TANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO WAKATI WA UENYEKITI WA SADC

 Tanzania imejivunia mafanikio yaliyopatikana wakati ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mafanikio hayo yameelezewa katika Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ulifanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam.

Kupitia mkutano huo, Prof. Kabudi  amekabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kwa Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica P. Clemente kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Verónica Nataniel Macamo Dlhovo   

Prof. Kabudi amesema pamoja na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19) jumuiya ya SADC imeendelea kufanya kazi zake, mikutano yake chini ya uongozi wa Tanzania kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kupitia njia ya mtandao (video conference)

"Nasema ni mafanikio makubwa kwa sababu Jumuiya nyingine za kikanda zimeshindwa kufanya hivyo, sisi ndiyo jumuiya pekee iliyoanza utaratibu huu wa aina hii ya mikutano kwa sababu kwetu tuliona COVID 19 ni changamoto ambayo haiwezi kutuzuia kufanya shughuli zetu,". Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa mbali na kupambana a janga la COVID 19, mafanikio mengine ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika jumuiya ya SADC, lugha nyingine ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.   

"Lugha ya Kiswahili kwa Tanzania ni lugha ya ukombozi wa Afrika, ndiyo lugha iliyotumika wakati wa kuwafundisha wapigania uhuru mbinu za kuwasiliana wakati wa ukombozi kwa mataifa ya Afrika," Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti wa SADC ni kusimamia na kukamilika kwa Mwongozo wa kusafirisha bidhaa na huduma kwa nchi wanachama katika kipindi cha (COVID-19). Mwongozo huo umelenga kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma mbambali baina ya nchi wanachama.

Tanzania imewezesha agenda ya viwanda kutekelezwa ambapo wakati wa COVID 19 tumeweza kuongeza uwezo wetu wa kutengeneza dawa kwa kuwa mataifa makubwa duniani mara baada ya kuibuka kwa covid 19 walisitisha kuuza dawa katika nchi nyingine ili wazitumie dawa hizo ndani ya nchi zao.

"Tunaimani kuwa msingi uliowekwa wakati wa COVID 19 utaimarisha jitiada zetu za kuwa na uchumi wa viwanda, uchumi wa kati na uchumi wa juu. Na sisi imekuwa jambo la faraja kubwa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya miaka mitano iliyokuwa imepangwa hapo awali," Amesema Prof. Kabudi.

"Chaguzi katika nchi za Malawi, Mauritius, Namibia zimefanyika kwa amani na utulivu. Ii imedhihirisha wazi kuwa demokrasia katika ukanda wetu inazidi kukua………haya yote ni mafanikio makubwa kwetu tukiwa mwenyekiti wa SADC," ameongeza Prof. Kabudi.

Nae Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica Clemente aliyemuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje Msumbiji, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya wakati wa Uenyekiti wake wa SADC.

Amefanya mambo makubwa kabisa kwa nchi wanachama wa SADC na amekuwa kama Mwalimu kwa nchi nyingine kutokana na maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wake akiwa mwenyekiti wa SADC.

"Sisi Msumbiji tunashukuru kwa kupokea Uenyekiti wa SADC na tunaahidi kujitahidi kadri ya uwezo wetu kuendeleza yale yote yaliyofanywa na Tanzania wakati akiwa Mwenyekiti, kwani Tanzania amekuwa mwalimu kwetu na nchi nyingine za SADC," amesema Balozi Monica.

Mkutano wa 40 wa baraza la mawaziri umehudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Afya , Maendeleoya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa wakifuatilia mkutano kwa njia ya Mtandao (Video Comnference) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akifungua mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia Mtandao (Video Comnference)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akikabidhi uenyekiti wa SADC ngazi ya mawaziri kwa Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica P. Clemente ambaye amemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje Msumbiji Mhe.Verónica Nataniel Macamo Dlhovo   

Baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao  jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa wakifuatilia mkutano kwa njia ya Mtandao (Video Conference) 
Baadhi ya maafisa waandamizi/Makatibu Wakuu wakifuatilia mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika leo kwa nnjia mtandao jijini Dar es Salaam 

Sunday, August 9, 2020

MKUTANO WA 40 WA SADC KUFANYIKA JIJINI DODOMA

Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Agosti, 2020 kwa njia ya mtandao (video conference) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.

 

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge amesema mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na vikao vya Kamati ya kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu na Mkutano wa Baraza la Mawaziri itakayoanza kufanyika tarehe 10 -13 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conference).

 

"Kulingana na taratibu na miongozo ya uendeshaji wa SADC, nafasi ya uenyekiti hushikiliwa na nchi wanachama kwa kupokezana kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Tanzania imekuwa Mwenyekiti tangu Mwezi Agosti, 2019 na inatarajwa kukabidhi Uenyekiti kwa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano huo. Aidha, itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Tanzania ilishika nafasi hii mwaka 2003," Amesema Balozi Ibuge.


Ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa sasa wa SADC,  atakabidhi Uenyekiti kwa Mheshimiwa Philipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 17 Agosti 2020 jijini Dodoma kwa njia ya Video Conference. 

 

Balozi Ibuge ameongeza kuwa, kwa kuwa kwa sasa Kiswahili ni moja kati ya lugha rasmi za mikutano ya SADC, lugha hiyo itatumika katika ngazi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri na ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali.

 

Aidha, Katibu Mkuu, Balozi Ibuge amesema kuwa, kutokana na janga la COVID-19 na  mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kufanya mikutano ya ana kwa ana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italazimika kukabidhi uenyekiti kwa njia ya mtandao ambapo Balozi wa Msumbiji hapa nchini atakabidhiwa uenyekiti kwa niaba ya nchi yake. Hali kadhalika, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji atakabidhi Uenyekiti kwa Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amesema kuwa mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Miaka 40 ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kukuza Maendeleo na kuhimili Changamoto zinazoikabili Dunia” ambapo kauli mbiu hiyo inatakiwa kutekelezwa na nchi zote Wanachama.

Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC wakiwa katika nchi zao. Nchi hizo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Mauritius, Jamhuri ya Madagascar na Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Zimbabwe.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam

 Mkutano ukiendelea jijini Dar es Salaam


Friday, August 7, 2020

SADC NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAJADILI, KUBORESHA RASIMU ZA NYARAKA ZA KISERA NA KIMKAKATI

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ngazi ya Makatibu Wakuu wamekutana na kujadili rasimu ya mpango mkakati elekezi mpya wa maendeleo wa kanda (2020 - 2030) pamoja na rasimu ya dira ya SADC (2020 - 2050) kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano ambae ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuangalia mambo mawili makubwa ambayo ni dhima ya SADC kuanzia sasa 2020 hadi 2050 pamoja na mpango mkakati wa SADC kuanzia mwaka 2020 - 2030 kwa sababu mpango mkakati wa SADC uliokuwa unatumika tangu mwaka 1992 umeisha muda wake. 

Nyaraka hizi mbili ni za muhimu sana kwa sababu hadi sasa hivi toka SADC ilipoanzishwa 1992 imefanya mambo makubwa lakini sasa ule mpango mkakati wake uliokuwa unatumika tangu mwaka 2010 na ambao ulihuishwa mwaka 2015 ukafika hadi 2020 umeisha muda wake hivyo ilikuwa ni muhimu kuandaa rasimu ya nyaraka hizi muhimu.

Ameongeza kuwa, rasimu za nyaraka hizo mbili zitawasilishwa kwenye mkutano wa 40 wa Wakuu wa nchi wanachama wa SADC na Serikali unaotegemewa kufanyika tarehe 17 Mwezi Agosti 2020 kwa njia ya mtandao.

Mpango Mkakati wa SADC ni mpango wa maendeleo wa kanda uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwaka 2003 jijini Dar es Salaam na ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2005 kwa kipindi cha miaka 15 (2005 - 2020). Aidha, mpango huo una vipaombele vinne ambavyo ni maendeleo ya viwanda na mtangamano wa soko, miundombinu bora, amani na usalama, pamoja na programu maalum.

Dira ya SADC 2020 - 2050 inatoa taswira ya Jumuiya kwa miaka 30 ijayo ambapo msingi wake ni amani, ulinzi, utulivu na utawala bora, uchumi wa kati unaoendeshwa na sekta ya viwanda na wanajumuiya wenye hali bora ya maisha. 

Hivyo dira ya SADC 2050 ni muhimu kwa maendeleo ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika hususan katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia 2030 na ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063.

Katika tukio jingine, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa UNHCR imekuwa na mchango mkubwa sana unaohusisha kulinda haki za wakimbizi lakini pia kuwarejesha wakimbizi nchini mwao. Pamoja na mambo mengine, mazungumzo yao yalilenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kwa ujumla. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi  Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifuatilia mkutano wa SADC ngazi ya Makatibu Wakuu wakati wakujadili rasimu ya mpango mkakati maendeleo wa kanda pamoja na rasimu ya dira ya SADC jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wakifuatilia mkutano
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Mwakilishi UNHCR nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula 
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki,Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam