Serikali imefafanua hatua yake ya kuvitaka vyombo
vya habari vya Kimataifa vinavyotaka kuvitumia vyombo vya habari vya
Tanzania kurusha matangazo yake yana lengo la kutambua vyombo hivyo
vinashirikiana vyombo gani vya hapa nchini na sio kuvizuia kutangaza na
kuendesha vipindi vyake hapa nchini kama inavyoripotiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Uingereza hapa
nchini Dkt. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari
vya Kimataifa zimekwishatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni ya
kutangaza na kuendesha vipindi vyao.
"Leo nimekutana na Balozi mteule wa Uingereza
hapa nchini Dkt. David Concar na kumueleza lengo la kusajili vyombo vya Habari vya
kimataifa lilikuwa ni kutaka kujua ni chombo gani cha kimataifa kinashirikiana
na chombo gana hapa nchini lakini pia ilikuwa ni matakwa ya kisheria," Amesema Prof. Kabudi
Kuhusu suala la mabadiliko ya sheria za asasi za
kiraia (NGOs) na vyama vya siasa Prof. kabudi amefafanua kuwa lengo lake
lilikuwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi
hizo pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za
kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha makundi yenye nia ovu
na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia
hizo kupenyeza fedha zao.
Balozi mteule wa Uingereza Dkt. David Concar amesema mazungumzo yao mbali
na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna
ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya
kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo
vya habari.
Katika tukio jingine pia Waziri wa mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana
na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark hapa nchini Balozi Mette Norgaard
ambapo mbali na suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 28 hapa
nchini,wamejadili pia masuala yanayohusu mashirikiano katika sekta za elimu, afya,
biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
akimkabidhi Balozi mteule wa Uingereza nchini, Dkt. David Concar nakala za sheria
ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
akimuonesha Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini, Dkt. David Concar namna
magazeti yanavyo ripoti habari za uchaguzi mkuu bila upendeleo
Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akiongea na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette
Norgaard Dissing-Spandet akimueleza jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo jijini
Dar es Salaam