Tuesday, June 1, 2021

BALOZI MULAMULA AWASILISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI BUNGENI JIJINI DODOMA

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo amewasilisha bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika Mkutano wa Bajeti unaoendelea jijini Dodoma. 

Akiwasilisha bungeni hotuba hiyo Balozi Mulamula ameeleza kuwa ili Wizara iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, analiomba Bunge Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 192,265,438,000. Kati ya fedha hizo shilingi 178,765,438,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 13,500,000,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

Aidha Balozi Mulamula ameyataja majukumu ambayo Wizara imeyapa kipaumbele kuyatekeleza katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, kama ifuatavyo;

  • Kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha balozi zetu kuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji, upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na kuvutia watalii; 
  • Kuendelea kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa;
  • Kuendelea kuweka mazingira wezeshi, kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ili kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya nchi;
  • Kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Taifa letu ndani na nje ya nchi;
  • Kuendelea kushawishi na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi moja moja, jumuiya za kikanda na kimataifa;
  • Kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani duniani na maendeleo kupitia Umoja wa Mataifa;
  • Kuendelea kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya balozi zetu ili kupunguza gharama na kuleta mapato kwa Serikali;
  • Kuendelea kufungua ofisi za Balozi na Konseli Kuu mpya katika nchi za kimkakati;
  • Kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC);
  • Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara, masuala ya uhusiano wa kimataifa na utangamano wa kikanda; 
  • Kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na
  • Kuendelea kusimamia rasilimali watu na fedha Makao Makuu ya Wizara na Balozini.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha bajeti ya Wizara, jumla ya shilingi 192,265,438,000 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. 
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  (Mb) Naibu Waziri (wa kwanza kushoto mstari wa mbele) na Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu (Watatu kutoka kushoto mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti. 

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Sehemu ya Watendaji wa Wizara na Wageni Waalikwa wakiwa tayari kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika picha ya pamoja Wageni waliofika bungeni jijini Dodoma kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akijibu maswali Bungeni baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022

Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitambulishwa Bungeni, kabla ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk Naibu Waziri wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea Bungeni 

Saturday, May 29, 2021

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI TANZANIA JENERALI VENANCE MABEYO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA- PRETORIA

 Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, ametembelea Ubalozi wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini.


Jenerali Mabeyo yupo Nchini Afrika Kusini kuhudhuria sherehe za kumuaga Mkuu Majeshi wa Afrika Kusini Jenerali SZ Shoki zilizofanyika kitaifa Jana Mjini Pretoria. Kuhudhuria sherehe hizi,ni utaratibu uliowekwa  na nchi wanachama wa Jumuiya za SADC ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha  mashirikiano  hususan katika nyanja ya Diplomasia ya Ulinzi (Defence Diplomacy) na Amani katika eneo Ia nchi za SADC.

 

Jenerali Mabeyo, alikaribishwa Ubalozini na Mhe. Balozi Mej. Jen. Gaudence Milanzi (Mst) na watumishi wa Ubalozi Mhe. Balozi Milanzi alitoa taarifa fupi ya eneo la uwakilishi ya Afrika Kusini, Botswana na Falme ya Lesotho.

 

Mhe. Balozi alieeza kuwa hali ya uwakilishi inaridhisha kiulinzi na kiusalama, Ubalozi umeendelea kukuza mashirikiano na nchiza eneo la uwakilishi ikiwa ni pamoja na SADC. Kwa kufuata miongozo ya sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kuendeleza Diplomasia ya kisiasa na kutekeleza Diplomasia ya uchumi.

 

Upande wake Jenerali Mabeyo alielezea ziara yake kwa ujumla nchini Afrika Kusini imekuwa ni ya mafanikio, na pia kuna mambo kama ambayo kama Mkuu  wa Majeshi ameona yanafaa kuigwa ili kuboresha utendaji wa Jeshi la Tanzania.

 

Jenerali Mabeyo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya  Muungano  wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan, amelenga kuendeleza maendeleo ndani na nje ya nchi mfano katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania na mwelekeo  unaelekeza kuimarisha  Diplomasia kwa  kujenga mahusiano na nchi duniani kwa   kuimarisha Diplomasia ya siasa na Diplomasia ya uchumi.

 

Jenerali Mabeyo alimsihi Balozi na watumishi wa Ubalozi kuhakikisha kuwa wanaielewa na kuisimamia dira ya Diplomasia kama ilivyoainishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuweza kutelekeza majukumu yao kwa wepesi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi wakati alipotembelea ubalozi huo Jijini Pretoria


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akiwa kwenye kikao na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na watumishi wa Ubalozi wakati alipotembelea ubalozi huo Jijini Pretoria


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na watumishi wa Ubalozi  



MAWAZIRI SEKTA YA BIASHARA EAC WAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VISIVYO VYA KIBIASHARA

Na mwandishi wetu, Arusha

Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki lakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kuimarisha biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo.

Awali akifungua mkutano Jijini Arusha Ijumaa, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawawezesha mawaziri kupitia na kujadili miongozo ambayo itasaidia kuboresha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara.  

Aidha, Mhandisi Mlote ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kanuni na sheria ya Afrika Mashariki, vikwazo visivyo vya kibiasha baina ya nchi na nchi vimekuwa vikizuia ukuaji wa biashara hivyo ni muhimu kupitia mkutano wa baraza la mawaziri kuangalia namna ya kuviondoa ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndani ya jumuiya.

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana mambo mengi ya msingi ikiwemo kuendelea kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi.

“Tumezungumza pia kuhusu ushiriki wetu katika kufanya biashara na Uingereza kwa kuzingatia kuwa Uingereza siyo sehemu Jumuiya ya Ulaya, lakini pia tumezungumzia suala la EAC kujiunga na jumuiya ya biashara ya Afrika ambayo sisi Tanzania tupo katika hatua kadhaa na kuona kuwa na sisi tunajiunga na jumuiya hiyo mwaka huu,” Amesema Prof. Mkumbo

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amesema kuwa mawaziri wamekubaliana kutoa msukumo wa biashara katika jumuiya ya afrika mashariki lizingatiwe na kupea kipaombele na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara katika nchi mbalimbali.

“Pamoja na mambo mengine, pi tumekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru (Non-tarrif barriers) viondolewe kwani vimekuwa vikikwamisha biashara bila sababu za msingi, na kuangalia jinsi ya kuwekeza kwenye eneo la uwekezaji ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvutia wawekezaji” amesema Mhe. Mwambe    

Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na maamuzi ya ripoti ya mawaziri wa fedha, ripoti ya kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati ya uwekezaji.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya Mhe. Betty Maina, Waziri wa Viwanda na Biashara, - Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.

Wengine ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Mhe. Beata Habyarimana, Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Mhe. Grace Choda, pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Balozi Jeremie Banigwaninzigo.

Mkutano huu ni maelekezo ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini Kenya tarehe 04 hadi 05 Mei, 2021.

Waziri wa Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo akifafanua jambo katika mkutano wa Baraza la kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki leo jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe. Kulia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban. Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya, Mhe. Betty Maina akiwasilisha hoja kwenye mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote

Ujumbe wa Uganda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)

Ujumbe wa Rwanda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)

Ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)




  

NAIBU WAZIRI MBAROUK; TANZANIA ITAENDELEA KUHESHIMU NA KUTAMBUA MCHANGO WA WALINDA AMANI KOTE DUNIANI.

Tanzania inaendelea kuheshimu na kuthamini mchango na kazi kubwa inayofanywa na Walinda Amani kote duniani. Haya yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo pia aliongoza zoezi la uwekaji mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa. “lengo kuu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchangia vikosi vyake kwenye Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika maeneo yenye migogoro na wananchi wa maeneo hayo wanarejea kwenye shughuli zao za kila siku” Naibu Waziri Mbarouk.

Tanzania inashikilia nafasi ya 13 kwa wingi wa idadi ya askari miongoni mwa nchi 122 zinazochangia vikosi kwenye Umoja wa Mataifa. Kutoka nchi za Afrika, Tanzania inashikilia nafasi ya 7 kati ya nchi 35 zinazochangia vikosi vya kulinda amani. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2021, Tanzania ilikuwa na jumla ya Askari 1,481 kwenye Misheni sita za ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani. 

Aidha, Naibu Waziri Mbarouk ameeleza furaha kuona Umoja wa Mataifa (UN) umetambua mchango na umuhimu wa vijana ambao ndio hutoa mchango mkubwa katika misheni za kulinda amani. “Nafurahi kuona UN wanatambua mchango wa vijana kupitia maazimio ya Baraza la Usalama Na. 2250 (la mwaka 2015) kuhusu vijana, amani na usalama; Azimio Na. 2419 (la mwaka 2018) kuhusu kuwajumuisha vijana kwenye majadiliano na utekelezaji wa makubaliano ya amani; na Azimio Na. 2535 (la mwaka 2020) ambalo hutaja hatua za utekelezaji za ajenda ya vijana, amani na usalama kwenye maeneo ya operesheni za amani”. ameeleza Naibu Waziri Mbarouk 

Licha ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hushiriki pia katika jitihada za kuimarisha amani kwa nchi zinazotuzunguka kuupitia mitangamano ya kikanda kama vile, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akihutubia hadhira iliyojitokeza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akikagua gwaride kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiweka mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.

Friday, May 28, 2021

WAZIRI MULAMULA AHIMIZA KASI NA WELEDI KATIKA UTENDAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mkutano na watumishi wa Wizara jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine mkutano huu ulilenga kutoa maelekezo kwa watumishi wa Wizara ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, pia kusikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa Watumishi ili kuzipa suluhisho la kudumu.  

Waziri Mulamula ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwahimiza watumishi wa Wizara kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kujituma ili kukidhi matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita na Watanzania kwa ujumla. “Watanzania wanamatarajio makubwa na Wizara yetu, tunajukumu kubwa la kuhakikisha tunatimiza matarajio yao hivyo ni lazima tufanye kazi kwa kujituma na weledi zaidi, pia kuacha kufanya kazi kwa mazoea” Waziri Mulamula. 

Aidha, Waziri Mulamula ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa Wizara inatafuta fursa mbalimbali za masomo ya muda mfupi na mrefu ili kuwaongezea ujuzi watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao. Sambamba na hilo, Waziri mulamula ameleza kuwa Wizara inadhamira ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili kuwaogezea hali katika utendaji. “Natambua kuwa ufanisi katika Wizara hii hauwezi kupatikana iwapo mazingira ya ufanyaji kazi sio mazuri. Kupitia kwa Katibu Mkuu, tuna dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuhakikisha upandishwaji wa vyeo unakamilika na kuhakikisha kuwa watumishi wanapata stahili zao ipasavyo na kwa wakati” Waziri Mulamula

Kwa upande wake Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara amewasisitiza Watumishi kufanya kazi kwa ubunifu na kwa umoja ili kuendelea kukuza mahusiano ya kiuchumi na mataifa, jumuiya za kikanda na taasisi nyingine za kimataifa. Balozi Sokoine ameongezea kusema ni vyema watumishi wa Wizara kuendelea kuungana na kushirikiana vyema katika kulinda uchumi na masilahi mapana ya Taifa. Vilevile kuhakikisha kuwa balozi zetu zinakuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji na upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zetu.

Waziri Mulamula na Balozi Sokoine wamekutana na Watumishi wa Wizara kwa mara ya kwanza tokea walipoteuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nyadhifa zao. Mkutano huu pia ulihusisha Ofisi za Balozi zinazoiwalikilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara. Wengine walioketi, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine (kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex B.D.J Mfungo (kulia)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea baina yake na Watumishi wa Wizara uliofanyika jijini Dodoma

Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula na Watumishi wa Wizara


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano
Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Waziri Mulamula na Watumishi wa Wizara

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara.

Thursday, May 27, 2021

MAWAZIRI BIASHARA, VIWANDA, FEDHA NA UWEKEZAJI KUKUTANA KESHO JIJINI ARUSHA

 Na Mwandishi wetu, Arusha

Baraza la Mawaziri la kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili wanategemea kukutana kesho tarehe 28 Mei 2021 Jijini Arusha kujadili masuala mbalimbali ya kukuza biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo. 

Mkutano huo wa Mawaziri umetanguliwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) wa Jumuiya hiyo uliofanyika leo jijini Arusha ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamepokea na kujadili ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti za baraza la kisekta la mawaziri wa fedha, ripoti ya kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati ya uwekezaji.

Mkutano wa Makatibu Wakuu wa leo tarehe 27 Mei 2021 utafuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa kisekta tarehe 28 Mei 2021 jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) ngazi ya Makatibu Wakuu, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki kutoka Kenya, Dkt. Kevit Desai akiongea na wajumbe wa mkutano ulifanyanyika leo Jijini Arusha


Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Bw. Doto James akifafanua jambo katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha. Kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Prof. Godius Kahyarara na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban. 


Ujumbe wa Burundi ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha


Ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha 


Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) leo Jijini Arusha

Wajumbe wakifuatilia mkutano