Tuesday, June 1, 2021

BALOZI MULAMULA AWASILISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI BUNGENI JIJINI DODOMA

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo amewasilisha bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika Mkutano wa Bajeti unaoendelea jijini Dodoma. 

Akiwasilisha bungeni hotuba hiyo Balozi Mulamula ameeleza kuwa ili Wizara iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, analiomba Bunge Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 192,265,438,000. Kati ya fedha hizo shilingi 178,765,438,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 13,500,000,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

Aidha Balozi Mulamula ameyataja majukumu ambayo Wizara imeyapa kipaumbele kuyatekeleza katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, kama ifuatavyo;

  • Kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha balozi zetu kuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji, upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na kuvutia watalii; 
  • Kuendelea kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa;
  • Kuendelea kuweka mazingira wezeshi, kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ili kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya nchi;
  • Kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Taifa letu ndani na nje ya nchi;
  • Kuendelea kushawishi na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi moja moja, jumuiya za kikanda na kimataifa;
  • Kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani duniani na maendeleo kupitia Umoja wa Mataifa;
  • Kuendelea kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya balozi zetu ili kupunguza gharama na kuleta mapato kwa Serikali;
  • Kuendelea kufungua ofisi za Balozi na Konseli Kuu mpya katika nchi za kimkakati;
  • Kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC);
  • Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara, masuala ya uhusiano wa kimataifa na utangamano wa kikanda; 
  • Kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na
  • Kuendelea kusimamia rasilimali watu na fedha Makao Makuu ya Wizara na Balozini.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha bajeti ya Wizara, jumla ya shilingi 192,265,438,000 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. 
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  (Mb) Naibu Waziri (wa kwanza kushoto mstari wa mbele) na Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu (Watatu kutoka kushoto mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti. 

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Sehemu ya Watendaji wa Wizara na Wageni Waalikwa wakiwa tayari kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika picha ya pamoja Wageni waliofika bungeni jijini Dodoma kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akijibu maswali Bungeni baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022

Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitambulishwa Bungeni, kabla ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk Naibu Waziri wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea Bungeni 
MUHTASARI WA HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI LIBERATA RUTAGERUKA MULAMULA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022

1.0 UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 20-20-21 na pia lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 20-21-22. Aidha, naomba Hotuba yangu yote kama ilivyo kwenye Kitabu cha Bajeti iingizwe kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard).

2. Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu siku ya leo. Kwa kuwa Hotuba hii ya Bajeti ni ya kwanza nikiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuongoza Wizara hii. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote na kwa kudra za Mwenyezi Mungu nitatekeleza majukumu yangu ipasavyo katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.

3. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, tarehe 17 Machi, 2021 Taifa lilipata msiba mzito wa kuondokewa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Taifa letu limepoteza viongozi wetu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mheshimiwa Balozi Mhandisi John William Hebert Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Naomba kutumia nafasi hii kuungana na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu waliotangulia kuwasilisha Hotuba zao kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais, familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa ujumla kwa misiba hii mizito. Wizara yangu inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa viongozi hawa katika kukuza diplomasia yetu.

4. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii pia kutoa shukrani za dhati kwa nchi marafiki na jumuiya ya kimataifa kwa kuonesha mshikamano, kutufariji na kushiriki nasi katika kipindi cha majonzi makubwa kwa Taifa letu.

5. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kutoa shukrani kwa Umoja wa Mataifa kwa uamuzi wake wa kuitisha kikao rasmi cha Baraza Kuu la Umoja huo kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia kikao hicho, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilielezea mafanikio makubwa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyopatikana chini ya Uongozi wa Hayati Dkt. Magufuli katika kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, maji, afya, nishati na miundombinu ya usafirishaji. Tunawashukuru sana.

6. Mheshimiwa Spika, vilevile, naomba kutoa pole kwako na Bunge lako Tukufu kufuatia vifo vya Waheshimiwa Khatibu Said Haji aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde; Mhandisi Atashasta Justus Nditiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Mkoa wa Kigoma; na Martha Jachi ambayo aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahala pema peponi. Amina.

7. Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa na kwa moyo mkunjufu napenda kutumia nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, nawapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), kwa kuaminiwa kuendelea kushika nafasi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

8. Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

9. Mheshimiwa Spika, tuna imani kuwa uongozi mpya utaendelea kudumisha tunu za Taifa na kuimarisha diplomasia ya nchi yetu.

10. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeweka historia ya kujivunia na kuigwa duniani kwa namna ilivyopata uongozi wa juu wa Serikali kwa kuzingatia misingi ya Katiba kufuatia vifo vya Viongozi Wakuu waliokuwa madarakani. Hatua hii ni kielelezo cha ukomavu, uimara wa demokrasia na kuzingatiwa misingi ya utawala wa sheria.

11. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake aliyowasilisha hapa Bungeni ambayo imetoa dira na mwongozo wa utekelezaji wa kazi za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20-21-22. Nawapongeza pia Waheshimiwa Mawaziri wenzangu walionitangulia kuwasilisha hotuba zao katika Bunge hili la Bajeti.

12. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa uongozi wako madhubuti katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb), Naibu Spika; Wenyeviti wa Bunge; na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi nzuri wanazozifanya kukusaidia kusimamia na kuendesha shughuli za Bunge.

13. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kuipongeza na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Uenyekiti wa Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), pamoja na Makamu wake Mhe. Vincent Paul Mbogo (Mb), kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kuishauri Serikali hususan Wizara yangu. Naomba nikiri kuwa miongozo na ushauri wao katika masuala mbalimbali umekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

14. Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwapongeza Waheshimiwa Eliadory Felix Kavejuru na Dkt. Florence George Samizi kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Wabunge wa Majimbo ya Buhigwe na Muhambwe, mtawalia. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa kuaminiwa kuwawakilisha wananchi katika Bunge hili Tukufu. Vilevile, nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wote walioteuliwa na Mheshimiwa Rais kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini. Kuteuliwa kwao ni kielelezo cha kuaminiwa na Mheshimiwa Rais katika kuwaletea maendeleo wananchi.

2.0 MISINGI YA SERA YA TANZANIA KATIKA UHUSIANO WA KIMATAIFA


15. Mheshimiwa Spika, historia ya nchi yetu imesheheni misingi imara inayoiwezesha kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ushawishi mkubwa kimataifa tangu Uhuru. Misingi ya nchi yetu kuheshimika kimataifa iliwekwa na Waasisi wa Taifa letu kwa kupinga na kulaani ubabe, uonevu na ukandamizaji popote pale ulipotokea duniani bila hofu. Hivyo, katika kusimamia misingi hiyo, tumeendelea kulinda uhuru wetu; kujiamulia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa; kulinda mipaka ya nchi yetu; kutetea haki; kuimarisha ujirani mwema; na kutekeleza Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote kama dira na msimamo wetu kwenye uhusiano na nchi nyingine katika jumuiya ya kimataifa.

3.0 TATHMINI YA HALI YA UCHUMI, SIASA, ULINZI NA USALAMA DUNIANI KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

16. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa fupi kuhusu hali ya uchumi, siasa, ulinzi na usalama duniani kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 kama ifuatavyo:

17. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya mwezi Januari 20-21, ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 20-20 ulipungua kwa asilimia 4.3 kutokana na janga la UVIKO-19 ambao uliathiri sekta nyingi za uchumi hususan uwekezaji, uzalishaji, upatikanaji wa huduma na biashara ya kimataifa. Kasi ya kupungua kwa ukuaji wa uchumi ilikuwa ndogo kwa asilimia 0.9 ikilinganishwa na makadirio ya awali ya asilimia 5.2. Aidha, kwa mwaka 20-21 uchumi wa dunia unakadiriwa kukua kwa asilimia 4 kutokana na kuanza kurejea kwa shughuli za kiuchumi katika nchi mbalimbali.

18. Mheshimiwa Spika, hali ya siasa, ulinzi na usalama imeendelea kuimarika katika maeneo mengi barani Afrika. Katika kipindi cha mwezi Julai, 20-20 hadi Aprili, 20-21 nchi za Benin, Burkina Faso, Côte d’Ivoire, Chad, Ghana, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Niger, Shelisheli, Guinea, Uganda na Jamhuri ya Kongo zilifanya uchaguzi. Tunawapongeza Waheshimiwa Marais wa nchi hizo kwa kuchaguliwa na tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali zao kwa lengo la kudumisha uhusiano baina ya nchi zetu.

19. Mheshimiwa Spika, taarifa ya kina inapatikana kwenye Aya ya 20 hadi 35 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

4.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

20. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 20-20-21, Wizara yangu iliendelea kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Muundo wa Wizara Toleo la tarehe 7 Julai, 20-18. Majukumu hayo yameainishwa kwenye Aya ya 36 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

21. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Wizara uliongozwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 20-15; Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 20-01; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 20-25; Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na miongozo mingine kama ilivyoainishwa kwenye Aya ya 37 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

22. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2020/21, Wizara ilipanga kukusanya shilingi bilioni mbili, milioni mia tano hamsini, laki nane na sabini na tisa elfu. Kati ya kiasi hicho shilingi milioni arobaini na saba, laki moja na sabini elfu ni makusanyo ya Makao Makuu ya Wizara,na shilingi bilioni mbili; na milioni mia tano na tatu na laki saba na elfu tisa ni makusanyo kutoka Balozi za Tanzania. Vyanzo vya mapato hayo ni uhakiki wa nyaraka, pango la majengo ya Serikali nje ya nchi na mauzo ya nyaraka za zabuni.

23. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 20-21, Wizara ilikusanya jumla ya shilingi milioni mia saba hamsini na sita, laki moja themanini na mbili elfu na themanini na mbili sawa na asilimia ishirini na tisa nukta sita ya lengo lililopangwa kwa Mwaka wa Fedha 20-20-21. Kupungua kwa mapato hayo kumetokana na kukosekana kwa wapangaji katika baadhi ya majengo ya Serikali kwenye Balozi za Tanzania kutokana na athari za uwepo wa janga la UVIKO-19 ambayo imesababisha kukosa wapangaji kutokana na kutokuwepo kwa biashara.

Fedha Zilizoidhinishwa

24. Mheshimiwa Spika, katika kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 20-20-21, Bunge lako Tukufu liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni mia moja na tisini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni mia moja sabini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida;na shilingi bilioni ishirini ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Katika fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, shilingi bilioni mia moja sitini na saba, milioni mia saba na kumi na saba, laki saba ishirini na tatu elfu ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo;na shilingi bilioni kumi na mbili na milioni thelathini na mbili, laki tisa na sitini na moja elfu ni kwa ajili ya Mishahara.

Fedha Zilizopokelewa na Kutumika

25. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 20-21 Wizara ilipokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi bilioni mia moja ishirini na saba, milioni mia sita arobaini na nane, laki tano arobaini na tisa elfu, mia tano kumi na tano. Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia sitini na tatu nukta tisa ya fedha zote za bajeti zilizoidhinishwa katika Mwaka wa Fedha 20-20-21. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni mia moja kumi na nane, milioni mia nane tisini na tatu, laki tatu kumi na tisa elfu, mia tisa arobaini na saba ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo sawa na asilimia sabini nukta tisa na shilingi bilioni nane, milioni mia saba hamsini na tano, laki mbili tisini na tisa elfu, mia tano sitini na nane ni kwa ajili ya mishahara sawa na asilimia sabini na mbili nukta nane.

26. Mheshimiwa Spika, katika fedha zilizotolewa, Wizara ilitumia kiasi cha shilingi bilioni mia moja na sita, milioni mia sita na moja, laki mbili hamsini elfu na mia tatu sawa na asilimia themanini na tatu nukta tano ya fedha zilizopokelewa. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni tisini na saba, milioni mia nane arobaini na sita, ishirini elfu na mia saba thelathini na mbili ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na shilingi bilioni nane, milioni mia saba hamsini na tano, laki mbili ishirini na tisa elfu, mia tano sitini na nane ni mishahara.

27. Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi mapitio ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 20-20-21 kama ifuatavyo:

4.1 Kusimamia na Kuratibu Masuala ya Uhusiano Baina ya Tanzania na Nchi Nyingine

28. Mheshimiwa Spika, mwezi Mei 20-21, Wizara iliratibu na kufanikisha Ziara ya Kitaifa ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya. Ziara hiyo ya kwanza ya Kitaifa tangu kuapishwa kwa Mheshimiwa Rais ililenga kuimarisha uhusiano wa kidugu na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili. Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais alihutubia Kikao Maalum cha Pamoja cha Bunge la Taifa na Bunge la Seneti la Kenya.

29. Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 20-21, Wizara iliratibu ziara ya Kikazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda. Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais na mwenyeji wake Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda walishuhudia uwekaji saini mikataba mitatu ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani - Tanga, Tanzania. Mikataba iliyosainiwa imeainishwa kwenye Aya ya 50 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

30. Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 20-21, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji hapa nchini kwa mwaliko wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika ziara hiyo, viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha ujirani mwema.

31. Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 20-21, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Sahle-Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia iliyofanyika nchini. Tanzania na Ethiopia zilikubaliana kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji; kubadilishana utaalam na uzoefu katika uendeshaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya ngozi za mifugo na Tanzania kuisaidia Ethiopia kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa na Chuo cha Diplomasia cha Ethiopia.

32. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 20-20, Wizara iliratibu ziara rasmi ya Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, Rais wa Jamhuri ya Malawi iliyofanyika nchini. Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, Tanzania na Malawi zilikubaliana kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Songwe/Kasumulu; ujenzi wa barabara ya Mpemba - Isongole – Mbozi -Chitipa - Mbilima; na Mamlaka ya Bandari Tanzania kufungua ofisi nchini Malawi. Nchi hizi pia zilikubaliana kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya pamoja ya kufua umeme na umwagiliaji katika Bonde la Mto Songwe.

33. Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba 20-20, Wizara iliratibu ziara ya Kikazi ya Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda iliyofanyika nchini. Katika ziara hiyo, Tanzania na Uganda zilisaini Hati ya Makubaliano Kuanza Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani - Tanga, Tanzania. Maelezo ya kina ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 46 hadi 61 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

34. Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 20-21, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mhe. Wang Yi, Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China iliyofanyika hapa nchini. Pamoja na masuala mengine Serikali ya nchi hiyo ilitoa msaada wa shilingi milioni mia tatu hamsini kwa ajili ya kununua vifaa vya karakana ya fani ya uvuvi katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA, Chato na Mwezi Mei, 20-21 imetoa msaada wa Shilingi bilioni thelathini na tano nukta tatu saba kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

35. Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 20-20, Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba kati ya Tanzania na China utakaowezesha Tanzania kuuza maharage aina ya soya katika soko la China. Kupitia Mkataba huo Tanzania inakuwa nchi ya 12 kuruhusiwa kuuza maharage hayo ambayo yana soko kubwa nchini humo. Kampuni 49 za Tanzania zimepata vibali vya kuuza maharage hayo katika soko hilo. Hadi kufikia mwezi Mei 20-21, zaidi ya tani mia moja na ishirini za soya zimekwishauzwa chini ya mpango huu.

36. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kufanikisha upatikanaji wa kampuni ya PT Indesso ya nchini Indonesia iliyojenga kiwanda cha kutengeneza mafuta yatokanayo na majani ya mimea katika eneo la Mgelema, Pemba kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Biashara la Zanzibar kwa gharama ya Dola za Marekani milioni moja nukta nne. Kiwanda hicho kilizinduliwa mwezi Septemba 20-20 na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Maelezo ya kina ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 62 hadi 72 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

37. Mheshimiwa Spika, kufuatia utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, Wizara imefanikisha Tanzania kuruhusiwa kuanza kuingiza nyama na bidhaa za nyama katika masoko ya nchi za Oman, Kuwait na Qatar. Vilevile, bidhaa hizo zitaanza kuuzwa nchini Saudi Arabia baada ya kukamilika kwa taratibu za kupata ithibati kutoka kwenye mamlaka za nchi hiyo. Aidha, mwezi Januari 20-21, Wizara ilifanikisha upatikanaji wa vibali kwa kampuni nane za Tanzania kuuza minofu ya samaki aina ya sangara katika nchi ya Saudi Arabia.

38. Mheshimiwa Spika, mwezi Januari 20-21, Wizara ilifanikisha uwekaji saini Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, Zanzibar. Mradi huo utajumuisha ujenzi wa eneo la kuhudumia mizigo; gati la meli za uvuvi; gati la meli za mafuta na gesi; chelezo kwa ajili ya matengezo ya meli; na mji wa kisasa katika eneo la Mangapwani. Mradi utakapokamilika utachochea ukuaji wa biashara na usafirishaji Zanzibar.

39. Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti 20-20, Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa mkopo wa Dola za Marekani milioni kumi na tano nukta tatu kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait kwa ajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji kwenye eneo la ukubwa wa hekta elfu tatu katika Bonde la Mto Luiche mkoani Kigoma. Mradi huo utaongeza uzalishaji wa mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga na hivyo kuinua kipato cha wakulima wa eneo hilo. Maelezo ya kina ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 73 hadi 81 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

40. Mheshimiwa Spika, mwezi Februari 20-21, Wizara iliratibu uwekaji saini Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni ya Tangen & Intertorco Group ya nchini Hispania kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Unguja; Bandari ya Mkoani, Pemba; na mradi wa kufua umeme kwa kutumia gesi. Hafla ya uwekaji saini makubaliano hayo ilishuhudiwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

41. Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba 20-20, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa 111 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya OACPS uliofanyika kwa njia ya mtandao chini ya uenyekiti wa Tanzania. Kupitia Mkutano huo, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 10 za Jumuiya hiyo zitakazonufaika na utekelezaji wa mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya samaki ujulikanao kama FISH4ACP unaogharimu shilingi bilioni mia moja na kumi. Katika mradi huo Tanzania imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya samaki aina ya migebuka na dagaa kutoka mkoa wa Kigoma.

42. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 20-20, Wizara iliratibu na kufanikisha kusainiwa kwa Mkataba kati ya Tanzania na Uswisi wa msaada wa shilingi bilioni thelathini na tisa nukta moja tano kugharamia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini na Mkataba wa shilingi bilioni nne nukta tisa tano ikiwa ni msaada wa kuchangia Mfuko wa Pamoja wa Afya. Pia, Wizara iliratibu kusainiwa kwa Mkataba kati ya Tanzania na Uswisi wa shilingi bilioni kumi na tano nukta nane ikiwa ni msaada kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Kutokomeza Malaria Awamu ya Kwanza; na Mkataba wa shilingi bilioni ishirini na nne nukta saba sita ikiwa ni msaada kwa ajili ya kutekeleza Programu yaKuimarisha Mfumo wa Kutoa Huduma za Afya Awamu ya Tatu. Misaada hiyo imeendelea kuchangia jitihada za Serikali katika kupunguza umaskini na kuboresha huduma za afya nchini.

43. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina ni kama inavyoonekana katika Aya ya 82 hadi 97 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.



4.2 Kuratibu Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa


Jumuiya ya Afrika Mashariki

44. Mheshimiwa Spika, mwezi Februari 20-21, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao. Katika Mkutano huo, Wakuu wa Nchi waliidhinisha lugha za Kiswahili na Kifaransa kutumika rasmi kwenye shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

45. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwezi Julai 20-20 hadi Aprili, 20-21 Tanzania ilitoa vyeti Thelathini na saba Elfu, Mia Moja Kumi na Moja vya uasili wa bidhaa kwa wafanyabishara wadogo wa Tanzania wanaofanya biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vyeti hivyo, vimewasaidia wafanyabiashara kupata unafuu wa kodi kwa kutolipa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazokidhi vigezo vya uasili wa bidhaa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

46. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki kama hatua ya mpito kuelekea Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Hadi kufikia mwezi Aprili 20-21, zoezi la kukusanya maoni na kutoa elimu kwa umma limefanyika katika nchi za Burundi na Uganda. Timu ya wataalam ya Jumuiya inayokusanya maoni kuhusiana na rasimu ya katiba hiyo itatembelea Tanzania mwezi Agosti 20-21. Maelezo ya kina yanapatikana kwenye Aya ya 98 hadi 138 ya Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

47. Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 20-21, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Troika Mbili wa SADC uliofanyika jijini Maputo, Msumbiji. Katika Mkutano huo Nchi Wanachama ziliazimia kuendelea kushirikiana kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kaskazini mwa Msumbiji hususan kwenye Jimbo la Cabo Delgado.

48. Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2021, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao. Pamoja na masuala mengine, mkutano huo uliridhia kuongeza wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mikutano ya kisekta ya SADC. Maelezo ya kina yanapatikana kwenye Aya ya 139 hadi 144 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Umoja wa Afrika

49. Mheshimiwa Spika, mwezi Februari 20-21, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa 34 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo, uliridhia ombi la Tanzania la kujumuisha lugha ya Kiswahili na uanzishaji wa Kituo cha Urithi wa Afrika jijini Dar es Salaam katika programu ya kutekeleza kaulimbiu ya mwaka 20-21 inayosema “Sanaa, Tamaduni na Urithi katika kufikia Azma ya Afrika Tuitakayo”. Maamuzi hayo yamejumuishwa kwenye shughuli za programu hiyo zinazotekelezwa na Umoja wa Afrika katika mwaka 20-21. Maelezo ya kina yanapatikana kwenye Aya ya 146 hadi 157 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Ushirikiano wa Kimataifa

50. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Kikao cha 46 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mwezi Machi 20-21. Katika Kikao hicho, Tanzania ilipata fursa ya kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu nchini ikiwa ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika kutoa haki ya elimu, huduma za afya, maji safi na salama pamoja na nishati.

51. Mheshimiwa Spika, Tanzania pia ilitumia Kikao hicho kuielezea jumuiya ya kimataifa kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 20-20 ambao kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifa letu uligharamiwa kwa fedha za ndani; na kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa haki, huru na wazi, uliozingatia misingi ya demokrasia na utawala bora, na ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu. Hatua hizi, zimesaidia kujenga mtazamo chanya kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu Taifa letu.

52. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba 20-20. Tanzania ilitumia fursa hiyo kuieleza jumuiya ya kimataifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa kuimarisha miundombinu ya reli, barabara, maji, nishati, afya na elimu. Vilevile, Tanzania ilieleza kuhusu hatua zinazochukuliwa katika kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma; kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma; na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

53. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina yanapatikana katika Aya ya 160 hadi 164 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

4.3 Kufuatilia na Kusimamia Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa na Hati za Makubaliano

54. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 20-20-21, Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano na kusimamia uwekaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano mbalimbali ya Kimataifa kama ilivyoainishwa kwenye Aya ya 165 hadi 166 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

4.4 Kuratibu Masuala ya Itifaki, Uwakilishi na Huduma za  Kikonseli

55. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine, Wizara imeendelea kuandaa na kuratibu ziara mbalimbali za Viongozi Wakuu wa Kitaifa nje ya nchi. Aidha, Wizara imeratibu na kufanikisha ziara za Viongozi wa Mataifa mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa waliokuja Tanzania kwa ziara rasmi, kushiriki  katika mikutano, makongamano na kutekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa. Maelezo ya kina yanapatikana kwenye Aya ya 167 hadi 178 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

4.5 Uratibu wa Watanzania Wanaoishi Nje ya Nchi (Diaspora)

56. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu masuala yanayohusu jamii za Diaspora ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Taifa. Kupitia jukumu hili, Tanzania imeendelea kunufaika na Diaspora ambapo kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania fedha zilizotumwa na Diaspora nchini kwa mwaka 20-20 zilikuwa ni Dola za Marekani milioni Mia Moja Themanini na tisa nukta Moja Tatu. Vilevile, katika kipindi hiki Diaspora wamenunua nyumba kupitia Shirika la Nyumba la Taifa zenye thamani ya shilingi milioni mia nne ishirini na tatu nukta nane.

4.6 Elimu kwa Umma

57. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa za ajira, elimu, biashara, uwekezaji na utalii zitokanazo na uanachama wa Tanzania katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa pamoja na mahusiano na nchi nyingine. Fursa hizo hutangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama inavyoonekana kwenye Aya ya 181 hadi 184 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti

4.7 Utawala na Maendeleo ya Watumishi

58. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia masuala ya utawala na maendeleo ya watumishi kwa lengo la kuboresha na kuimarisha utendaji wa kazi. Wizara ina jumla ya watumishi mia nne hamsini na tano wa kada mbalimbali. Kati yao watumishi mia mbili ishirini na nane wapo Makao Makuu ya Wizara na watumishi mia mbili ishirini na saba wapo kwenye Balozi za Tanzania. Katika kuimarisha utendaji kazi wa Wizara, masuala mbalimbali yanayohusu utawala na maendeleo ya watumishi yameendelea kusimamiwa kama ifuatavyo:

4.8 Mafunzo na Upandishaji Vyeo

59. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ambapo jumla ya watumishi mia mbili kumi na tisa walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi. Watumishi wanane walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi mia mbili kumi na moja walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Aidha, jumla ya watumishi mia mbili na nne wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo. Taarifa ya kina ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 187 hadi 190 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

4.9 Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara na Taasisi Zilizo Chini ya Wizara


60. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 20-20-21, Wizara ilitengewa bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni ishirini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopo ndani na nje ya nchi. Wizara inaendelea kufuatilia Wizara ya Fedha na Mipango fedha za bajeti ya maendeleo zilizopangwa kwa Mwaka wa Fedha 20-20-21 mara baada ya kukamilisha nyaraka za miradi hiyo kama taratibu zinavyoelekeza.

4.9.1 Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi Zilizo Chini ya Wizara

61. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kimeendelea kuendesha biashara ya mikutano; upangishaji wa nyumba na ofisi; na kutoa huduma ya afya kupitia hospitali inayomilikiwa na kituo hicho.

62. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Diplomasia kinaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa Wizara/Taasisi na Mashirika ya Serikali, mashirika na kampuni binafsi, balozi na watu binafsi; na kutoa mafunzo ya lugha saba za kigeni ambazo ni Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza, Kichina, Kikorea na Kireno. Aidha, Chuo kimekamilisha mtaala wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wageni.

63. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Hiari wa Afrika wa Kujitathmini Katika Masuala ya Demokrasia na Utawala Bora (APRM) ulifanya tathmini kuhusu utawala bora nchini na kuandaa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa APRM nchini Tanzania. Taarifa hiyo imeangazia maeneo makuu manne ambayo ni: Demokrasia na Siasa; Usimamizi wa Uchumi; Utendaji wa Mashirika ya Biashara; na Maendeleo ya Jamii. Taarifa imeainisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha 2015 hadi 2019.

64. Mheshimiwa Spika, kikao cha 30 cha Wakuu wa Nchi na Serikali zinazoshiriki Mpango wa APRM, kilichofanyika mwezi Machi 2021 wa njia ya mtandao kilimteua Mheshimiwa Balozi Ombeni Yohana Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Watu Mashuhuri wa APRM, Barani Afrika (The Panel of Eminent Persons). Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa uteuzi huo. Tuna imani kuwa uzoefu wake wa muda mrefu na umahiri katika masuala ya diplomasia, utaendelea kuwa hazina na rasilimali ya kipekee kwa maslahi ya nchi yetu na Bara zima la Afrika. Taarifa ya kina ni kama ilivyobainishwa katika Aya ya 191 hadi 205 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

5.0 SHUKRANI

65. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru Balozi, Mashirika na Taasisi za Kikanda na Kimataifa na Washirika wa Maendeleo kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali yetu.

66. Mheshimiwa Spika, kipekee nazishukuru nchi za Algeria, Australia, Austria, Brazil, Canada, China, Cuba, Denmark, Ethiopia, Finland, Hispania, Hungary, Italia, Iran, Ireland, Indonesia, India, Israel, Jamhuri ya Korea, Japan, Kuwait, Malaysia, Malta, Marekani, Mexico, Misri, Morocco, New Zealand, Nigeria, Norway, Oman, Pakistan, Poland, Qatar, Romania, Saudi Arabia, Singapore, Sri Lanka, Sweden, Sudan, Thailand, Tunisia, Ubelgiji, Uganda, Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Ujerumani, Urusi, Uswisi, Uturuki, Ureno, Umoja wa Falme za Kiarabu, Venezuela na Viet Nam.

67. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani pia kwa ACBF; AfDB; BADEA; DfID; EIB; EU; FAO; GiZ; IAEA; IFAD; ILO; IMF; IOM; JICA; KOICA; MASHAV; PAPU; OPCW; SIDA; UN; UNAIDS; USAID; UNCDF; UNCTAD; UNDP; UNEP; UNESCO; UNFPA; UNHCR; UNICEF; UNIDO; UNODO; UNWOMEN; UPU; WFP; WHO; na WWF. Vilevile, napenda kuwashukuru Abu Dhabi; Association of European Parliamentarians with Africa; Benki ya Dunia; Bill and Melinda Gates Foundation; Global Fund; Investment Climate Facility for Africa; Khalifa Fund; Kuwait Fund; Medecins Sans Frontieres; Red Cross; Trade Mark East Africa; pamoja na Mifuko na Mashirika mbalimbali ya Misaada. Ni dhahiri kuwa ushirikiano wao umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Serikali.

68. Mheshimiwa Spika, kwa moyo mkunjufu, napenda kuwashukuru watendaji na watumishi wa Wizara na Taasisi zake kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Kwa namna ya pekee, namshukuru Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri; Mhe. Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu; Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab, Naibu Katibu Mkuu; Waheshimiwa Mabalozi wa Tanzania; Wakuu wa Idara na Vitengo; Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara; na watumishi wote kwa kufanya kazi kwa umahiri, weledi na ufanisi.

69. Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuwashukuru Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), aliyekuwa Waziri; Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb) na Mhe. William Tate Ole Nasha (Mb) waliokuwa Naibu Mawaziri; Mhe. Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge aliyekuwa Katibu Mkuu na Dkt. Mwinyi Talib Haji aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu kwa mchango wao mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara katika Mwaka wa Fedha 20-20-21.

70. Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa, napenda kumshukuru mume wangu mpendwa Mhandisi Dkt. George Steven Mulamula; watoto wangu pamoja na familia yangu kwa ujumla kwa uvumilivu wao na kuwa karibu nami wakati wote wa kutekeleza majukumu yangu ambayo wakati mwingine yananilazimu kuwa mbali nao kwa muda mrefu.

6.0 MALENGO YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022


71. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 20-21-22, Wizara imeweka kipaumbele katika kutekeleza majukumu yafuatayo:

i. Kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi;

ii. Kuendelea kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa;

iii. Kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Taifa letu ndani na nje ya nchi;

iv. Kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika;

v. Kuendelea kushawishi na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi moja moja, jumuiya za kikanda na kimataifa; na

vi. Kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara.

72. Mheshimiwa Spika, Majukumu mengine ni kama yalivyobainishwa katika Aya ya 214 katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

7.0 MALENGO YA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022

Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)

73. Mheshimiwa Spika, AICC imepanga kupanua huduma za afya kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje la Hospitali ya AICC, ununuzi wa vifaa tiba; kujenga jengo la biashara jijini Arusha; na kukamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa Kituo cha mikutano kitakachoitwa Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC) jijini Arusha.

Chuo cha Diplomasia

74. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Diplomasia kimepanga kuendelea kutoa mafunzo ya mahusiano ya kimataifa; lugha ya Kiswahili kwa wageni; kuendelea kufanya tafiti katika maeneo ya mahusiano ya kimataifa na mbinu za kidiplomasia; kuendelea na ujenzi wa vyumba vya mihadhara kwa lengo la kuongeza udahili na mapato ya Chuo; na kuendelea kutoa ushauri na huduma za kitaalamu kwa Serikali na Taasisi zake.

Mpango wa Hiari wa Afrika wa Kujitathmini Katika Masuala ya Demokrasia na Utawala Bora (APRM)

75. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021-22, APRM inatarajia kuendelea kufanya tathmini za utawala bora za mpango wa APRM ikiwa ni pamoja na kuhuisha mbinu za utafiti kwa kupitia upya hojaji ya APRM; kuandaa taarifa ya mwaka na kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji; na kuimarisha mawasiliano na utoaji taarifa kuhusu Mpango wa APRM.

8.0 MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022

76. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 20-21-22, Wizara inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni mbili, milioni mia tano hamsini, laki nane sabini na tisa elfu ikiwa ni mapato ya Serikali yatakayopatikana kutokana na vyanzo vilivyopo Makao Makuu ya Wizara na Balozi za Tanzania ambavyo ni pango la nyumba za Serikali zilizopo nje ya nchi na kuthibitisha nyaraka.

77. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 20-21-22, Wizara imetengewa bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni mia moja tisini na mbili, milioni mia mbili sitini na tano, laki nne thelathini na nane elfu. Kati ya fedha hizoshilingi bilioni mia moja sabini na nane, milioni mia saba sitini na tano, laki nne thelathini na nane elfu ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida zinazojumuisha shilingi bilioni mia moja sitini na saba, milioni mia tisa thelathini na saba, laki mbili kumi na tisa elfu kwa ajili ya Matumizi Mengineyo; shilingi bilioni kumi, milioni mia nane ishirini na nane, laki mbili kumi na tisa elfu kwa ajili ya Mishahara; na shilingi bilioni kumi na tatu na milioni mia tano ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

78. Mheshimiwa Spika, kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, shilingi bilioni sita na milioni mia tano ni kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi ya ubalozi na kitega uchumi ubalozi wa Tanzania Kinshasa, DRC; shilingi bilioni tano ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya balozi, ubalozi wa Tanzania Muscat, Oman; shilingi bilioni moja ni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia; na shilingi bilioni moja ni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Chuo cha Diplomasia.

9.0 HITIMISHO

79. Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 20-21-22, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi bilioni mia moja tisini na mbili, milioni mia mbili sitini na tano, laki nne thelathini na nane elfu. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni mia moja sabini na nane, milionimia saba sitini na tano, laki nne thelathini na nane elfu ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi bilioni kumi na tatu na milioni mia tano ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

80. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii adhimu kukushukuru tena wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.

81. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.