Monday, June 21, 2021

MKUTANO WA 17 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA UCHUKUZI, MAWASILIANO NA HALI YA HEWA LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM.

Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa (TCM) umeanza kufanyika leo jijini Dar es Salaam. Mkutano huu utakaofanyika kwa lipindi cha siku tano (5) kuanzia tarehe 21 hadi 25 Juni 2021 unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa programu na miradi, maamuzi na maagizo ya mikutano ya awali katika sekta za miundombinu ya uchukuzi mawasiliano na hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Mkutano huu ambao unafanyika kwa njia ya ana kwa ana na mtandao, na kuhudhuriwa na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kufanya yafuatayo; 

Moja, Kupitisha Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Usalama Barabarani (EAC Road Safety Strategy). Mkakati huu unaombatana na Mpango Kazi wa Usalama Barabarani wa kipindi cha miaka 10 (2021-2030) unalenga kuchukua hatua madhubuti za kuboresha usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti adhari zinazopelekea ulemavu, upotevu wa maisha pamoja na mali kutokana ajari za barabarani. 

Mbili, Kuridhia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Uendeshaji na Usimamizi wa Anga la Juu la Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati hii ya Makubaliano inalenga kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za anga, kuimarisha usalama na mawasiliano ya usafiri wa anga kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na

Tatu, Kuridhia uanzishwaji wa Taasisi ya Mawasiliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutakoambatana na kupitisha Andiko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sambamba na hayo, katika ngazi ya Mawaziri wanatarajiwa kukubali kuibadili Taasisi ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki (East African Communication Organization –EACO) kuwa Taasisi rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo itakuwa na jukumu la simamia sekta ya Mawasiliano ndani ya Jumuiya. 

Kama ilivyo ada ya Mikutano ya Baraza la Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika katika ngazi tatu, Mkutano huu pia utafanyika katika ngazi tatu ambazo ni, Ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 22 Juni, 2021; Makatibu Wakuu, tarehe 23 na 24 Juni, 2021 na Mawaziri, tarehe 25 Juni, 2021.

Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akichangia jambo kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa kutoka nchini Burundi wakifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam. 
Washiriki kutoka nchini Kenya wakifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea.
Sehemu ya Washiriki kutoka nchini Sudani Kusini wakifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Mshiriki kutoka nchini Uganda akiwasilisha mchango wake kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.