Tuesday, June 22, 2021

Rais wa Ufaransa amtunikia Nishani Balozi Radhia


Rais wa Ufaransa amtunikia Nishani Balozi Radhia

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amemtunukia Balozi Mstaafu, Mhe. Radhia N. Msuya wa Tanzania, nishani ya “National Order of Merit”. Balozi Msuya amevikwa nishani hiyo jijini Dar Es Salaam na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Frederick Clavier kwa niaba ya Rais Macron tarehe 17 Juni 2021

 

Balozi Msuya ametunukiwa nishani hiyo kutokana na mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Ufaransa wakati akiwa Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika  katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2006-2010). Ametambuliwa kwa mchango mahsusi aliyoutoa wakati Ufaransa ilipokuwa Rais wa Umoja wa Ulaya.

 

Nishani hiyo ilianzishwa mwaka 1963 kwa nia ya kutambua mchango wa watunukiwa wake katika kuendeleza ushirikiano na Ufaransa hasa katika ustawi wa dunia. Baadhi ya watu mashuhuri waliowahi kutunukiwa nishani hiyo ni Rais François Mitterrand wa Ufaransa; Mfalme Juan Carlos I wa Uhispania na Bw. Njoroge Mungai wa Kenya.

 

Balozi Radhia ni mwanadiplomasia aliyefanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 35.  Ambapo alishika nafasi mbalimbali katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, uliopo New York, Marekani na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.

 

Mwaka 2010 mpaka 2016 Balozi Radhia aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, akisimamia masuala ya SADC, Botswana, Lesotho na Namibia. Mwaka 2017 Balozi Radhia Msuya alipata uhamisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kama Msaidizi wa Katibu Tawala. Nafasi hii aliitumikia hadi alipostaafu utumishi wa umma mwaka 2018. Kwa sasa Balozi Radhia Msuya yuko katika kampuni binafsi ya ushauri inayojishughulisha na masuala ya uwekezaji na diplomasia ya uchumi.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.