Mkutano wa 21 wa Baraza la
Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefunguliwa
leo tarehe 06 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.
Mkutano huo umeanza na ngazi
ya Maafisa Waandamizi kwa lengo la kuandaa taarifa zitakazowasilishwa katika
mkutano wa Makatibu Wakuu na Mawaziri. Pia unafanyika ukiwa umewakutanisha nchi
wanachama wote isipokuwa wajumbe wawili (Rwanda na Sudan ya Kusini) ambao wanashiriki
mkutano kwa njia ya mtandao.
Akifungua mkutano Naibu Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na
Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo ameeleza umuhimu wa mkutano wa sekta ya afya
hasa wakati huu ambapo dunia imetangaza kuwepo kwa wimbi la nne la janga la UVIKO-19.
Mhe. Bazivamo amesisitiza nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kushirikiana na kamati ya
uratibu ya UVIKO-19 ya jumuiya hiyo ili kuweza kuhakikisha tahadhari
zinaendelea kutiliwa mkazo sambamba na utolewaji wa chanjo ili kuweza kudhibiti
maambukizi mapya ya ugonjwa huo na kuruhusu kuendelea kwa shughuli za kiuchumi
kwa ustawi wa wananchi.
“Hakuna nchi iliyo salama
dhidi ya janga la UVIKO-19 kwakuwa kama nchi nyingine ndani ya jumuiya haipo
salama ni hatari kwa jumuiya yetu na dunia kwa ujumla” alisema Mhe. Bazivamo
Pia alifafanua, kupitia mkutano
huo nchi wanachama zitapata fursa ya kusikia taarifa zitakazowasilishwa na kila
nchi ili kwa pamoja kuweza kuchangia na kushauri namna bora ya kukabiliana na janga hilo,
kuwasilisha changamoto, na maoni yatakayosaidia kusimamia afya za wananchi kwa
ujumla.
Vilevile masuala mtambuka
yanayozigusa nchi wanachama yatapata nafasi ya kujadiliwa na kupatiwa suluhu ya
pamoja. Masuala hayo ni pamoja na; taratibu za kufuatwa mipakani wakati janga la
UVIKO-19 likiendelea kudhibitiwa, taratibu za upimaji wa UVIKO-19 ndani ya
jumuiya, na kuwezesha usafiri huru wa wafanyakazi, huduma, ajira na bidhaa
unasimamiwa kwa maslahi mapana ya jumuiya.
Mkutano huo unafanyika katika
ngazi tofauti kwa utaratibu ufuatao:- Tarehe 06 - 08 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya
Watalaamu; Tarehe 09 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu; na
tarehe 10 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya Mawaziri.
Ujumbe wa Tanzania katika
mkutano wa ngazi ya watalaamu umeongozwa na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akishirikiana
na Bw. Eliabi Chodota Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za
Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wengine walioshiriki mkutano
huo wanatoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto –
Tanzania Bara, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jami, Wazee, Jinsia, na watoto –
Tanzania Zanzibar; Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, pamoja na taasisi zilizo
chini ya Wizara za Afya.
=============================================================
|
Mwenyekiti wa Mkutano ngazi ya Wataalamu kutoka Jamhuri ya Kenya, Dkt. Kuria Francis akiwakaribisha wajumbe katika Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofunguliwa leo tarehe 6 Desemba 2021 katika Hotel Verde Mjini Zanzibar. |
|
Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Abdul S. Said (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota wakifatilia mkutano. |
|
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano. |
|
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
|
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi |
|
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya |
|
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda. |