Thursday, January 13, 2022

WAZIRI MULAMULA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI WATEULE WA SAUDI ARABIA, KOREA, INDONESIA NA MOROCCO NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mhe. Abdullah bin  Ali Alsheryan. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 
Mara baada ya makabidhiano viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza juu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano. 
Balozi Mulamula akimkaribisha Mhe.Abdullah bin  Ali Alsheryan katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Kim Sun Pyo. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 
Mara baada ya makabidhiano hayo Waziri Mulamula alimhakikishia Mhe.Kim Sun Pyo kuwa serikali ya Tanzania itampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake mapya katika kipindi chake atakachohudumu nchini. Jamhuri ya Korea imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za teknolojia ya mawasiliano, elimu, afya, utalii na ujenzi wa miundobinu.
Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ceasar Waitara na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Halmeinsh Lunyumbu wakifuatilia mazungumzo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Triyogo Jatmiko. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 

Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Triyogo Jatmiko walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na masoko, viwanda, elimu, utalii na kufungua fursa nyingine za kiuchumi kupitia ushirikiano imara wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ufalme wa Morocco, Mhe.Zacharia El Guoumiri. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 

Mazungumzo baina ya Mhe.Balozi Mulamula na Mhe. Balozi Zacharia El Guoumiri yalijikita katika kuimarisha ushirikiano baiba ya Tanzania na Morocco hususani katika sekta za michezo, elimu, maendeleo ya jamii na kuinua ujasiliamali kwa lengo la kukuza viwanda ili kuweza kuwanufaisha wananchi mataifa yao. 

Mazungumzo yakiendelea, kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Azizi akifatilia mazungumzo hayo.

SADC YAKUBALIANA KUENDELEA KUISADIA MSUMBIJI KULINDA AMANI

Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji ulioanza jana tarehe 11 Januari 2022 nchini Malawi umemalizika leo tarehe 12 Januari 2022 ambapo Nchi wanachama wa SADC wamekubaliana kuendelea kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji katika kuhakikisha Amani na usalama vinapatikana.  

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali, wamekubaliana  kuendelea kujitolea kulinda amani na usalama nchini Msumbiji hasa katika Jimbo la Cabo Delgado licha ya nchi nyingi kuendelea kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa uviko 19.

Akifunga Mkutano huo leo, Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera amewashukuru wakuuu wa Nchi na Serikali kwa Ushirikiano na umoja ambao nchi wanachama wa SADC wamekuwa wakionesha katika kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji kupambana na ugaidi.

“Lazima tuungane kwa pamoja na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Msumbiji inakuwa na Amani na Usalama……hivyo basi ni jukumu letu sisi sote katika kuhakikisha wananchi wa Msumbiji wanakuwa na amani kwani bila amani hakuna maendeleo,” amesema Rais Chakwera.

Awali akisoma tamko la pamoja, Katibu Mendaji wa SADC Bw. Elias Magosi amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wameipongeza SADC kwa dhamira yake isiyoyumba ya kusimamia na kutetea amani na usalama, na kwa kutumia rasilimali zake katika kushughulikia na kupambana na ugaidi katika jimbo la Cabo Delgado.

Mkutano huo pia umepongeza hatua ya mshikamano iliyooneshwa kwa ahadi za chakula zilizotolewa na Jamhuri ya Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kupunguza matatizo yanayowakabili wakimbizi  katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera akifunga Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 



Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 




Mkutano ukiendelea


Wakuu wa Nchi na Wawakilishi wa Wakuu wa nchi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 

Wednesday, January 12, 2022

BALOZI MBAROUK ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI, KUKAGUA MALI ZA SERIKALI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa Ubalozi pamoja na kukagua mali za Serikali nchini humo.

Balozi Mbarouk mara baada ya kukagua mali za Serikali, aliushukuru Ubalozi kwa mapokezi mazuri na kusema kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za makusudi kuendeleza kiwanja cha Serikali kwa kujenga jengo la Ubalozi na kitega uchumi. 

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Benedicto Mashiba amemshukuru Mhe. Naibu wa Waziri – Nje kwa kutenga muda wa kutembelea Ofisi ya Ubalozi na kukagua mali za Serikali zilizopo Lilongwe, licha ya kuwa na ratiba ngumu ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akioneshwa kiwanja cha Serikali na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Mhe. Benedicto Mashiba 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akikagua moja kati ya nyumba za Serikali zilizopo Lilongwe, nchini Malawi. Katika ukaguzi huo, Naibu Waziri ameambatana na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Mhe. Benedicto Mashiba



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Nchini Mawali na kupokelewa na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Mhe. Benedicto Mashiba









BALOZI MBAROUK KATIKA MKUTANO WA DHARURA BARAZA LA MAWAZIRI SADC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameshiriki katika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jijini Lilongwe, nchini Malawi.

Mbali na Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali, pia  mkutano huo ulitanguliwa na kikao cha Kamati ya Fedha ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika Jijini Lilongwe, nchini Malawi na kuhudhuriwa na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi wanachama wa SADC. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akishiriki katika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jijini Lilongwe, nchini Malawi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa SADC Jijini Lilongwe, nchini Malawi


Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ukiendelea Jijini Lilongwe nchini Malawi
Mawaziri walioshiriki katika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika picha ya Pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano wao uliofanyika Jijini Lilongwe, nchini Malawi 





BALOZI FATMA ASHIRIKI KIKAO KAMATI YA FEDHA SADC

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab ameshiriki katika kikao cha Kamati ya Fedha ya SADC kilichofanyika Jijini Lilongwe, nchini Malawi. 

Kikao hicho kimetanguliwa na Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji ulioanza tarehe 11 Januari 2021 Lilongwe, Malawi.

Katika Mkutano wa Dharuar wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika kikao cha Kamati ya Fedha ya SADC kilichofanyika Jijini Lilongwe, nchini Malawi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika kikao cha Kamati ya Fedha ya SADC



Tuesday, January 11, 2022

DKT. MPANGO AMWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA DHARURA MALAWI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura Wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji ulioanza leo tarehe 11 Januari 2022 Lilongwe, Malawi.

Awali akifungua Mkutano huo, Rais wa Afrika Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa TROIKA Mhe. Cyril Ramaphosa amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuiunga mkono Jamhuri ya Msumbiji katika Mapambano yake dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yanayoikabili nchi hiyo hasa Katila jimbo la Cabo Delgado.

Aidha, Mhe. Ramaphosa ameongeza kuwa kuna umuhimu kwa SADC kushirikiana katika kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya jumuiya hiyo.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa dharura umeongozwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Edward Komba pamoja na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.

 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango akifuatilia Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji. Mkutano umefanyika Lilongwe Malawi. Kulia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango akiongoza ujumbe wa Tanzania katika ukumbi wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji leo Lilongwe, Malawi

Baadhi ya Ujumbe wa Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali

Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Bishara za Kimataifa wa Zimbabwe Balozi Frederick Shawa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji. Mkutano umefanyika Lilongwe, Malawi.

Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji, Lilongwe, Malawi
Wakuu wa Nchi na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi walioshiriki katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa Mkutano huo leo Lilongwe, Malawi

Friday, January 7, 2022

BALOZI SHIYO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA ETHIOPIA

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Eugene Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho Januari, 5 2022 kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde Ikulu Ethiopia.

Katika mazungumzo yao, Mheshimiwa Rais Zewde alimkaribisha Balozi Shiyo nchini Ethiopia na kumpongeza kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia. Aidha, alisifia mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia uliojengwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Mfalme Haile Selassie, ambao walifanya kazi pamoja kuanzisha Umoja wa Afrika.
Aidha, Rais Zewde aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye suala la matumizi ya maji ya Mto Nile chini ya ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile. 
Vilevile, Mheshimiwa Rais Zewde aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Ethiopia za kuhakikisha changamoto za usalama nchini Ethiopia zinapata ufumbuzi. Pia, amemuahidi Mhe. Balozi Shiyo ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake wakati wote atakapokuwepo nchini Ethiopia. 
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shiyo aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa mapokezi na ukarimu alioupata tangu kuwasili kwake nchini Ethiopia tarehe 26 Novemba, 2021. Aidha, aliwasilisha Salamu za heri kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwenda kwa Mheshimiwa Sahle- Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.
Aidha, Mhe Balozi Shiyo alirejea mafanikio ya ziara ya Mhe. Rais Sahle-Work Zewde aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Januari 2021 ambapo nchi zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati, mifugo na bidhaa za Ngozi, utalii, uhamiaji na ulinzi na usalama. 
Balozi Shiyo ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarsha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye maeneo hayo na maeneo mengineyo yenye manufaa kwa pande zote mbili.  Balozi Shiyo pia ameongelea kuhusu suala la kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Addis Ababa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Addis Ababa.
Balozi Shiyo amemhakikishia Mheshimiwa Rais Zewde kwamba Tanzania itaendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye jithada za kurejesha amani na usalama nchini humo. 
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo akiwasilisha hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo  

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Sahle- Work Zewde na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) Mhe. Innocent Shiyo katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa waliohudhuria hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho  



Tuesday, December 14, 2021

BALOZI MULAMULA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MT. LUCIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ashiriki katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia iliyoandaliwa na Ubalozi wa Sweden hapa nchini. Mbali na Balozi Mulamula, Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo pia alishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika jana jioni jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia. Sherehe hiyo iliandaliwa na  Ubalozi wa Sweden.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiteta jambo na Mbunge wa Urambo (CCM), Margreth Sitta katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Balozi wa Norway Mhe. Elisabeth Jacobsen pamoja na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg pamoja na Balozi wa Norway Mhe. Elisabeth Jacobsen  


Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet akifurahia jambo na Mbunge wa Urambo (CCM), Margreth Sitta pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme 



Badhi ya watoto wakiimba nyimbo maalum ya kumbukizi ya Mtakatifu Lucia 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo pamoja na viongozi wengine akiwemo Mbunge wa Urambo Magreth Sitta wakifuatilia sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia


Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg akiongea na viongozi mbalimbali walioshiriki katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg katika sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia 

Badhi ya watoto wakiimba nyimbo maalum ya kumbukizi ya Mtakatifu Lucia 


Badhi ya viongozi wakishuhudia sherehe za maadhimisho ya Mtakatifu Lucia 


    Maadhimisho ya Seherehe ya Mtakatifu Lucia yakiendelea  



BALOZI SHIYO AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO AU

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Eugene Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika jijini Addis  Ababa tarehe 13 Desemba 2021.

Wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mahamat amempongeza Balozi Shiyo kwa kuteuliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika. Amemkarabisha na kumtakia kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mhe. Mahamat na Balozi Shiyo wamekubaliana kushirikiana katika kusimamia utekelezaji wa masuala ya kipaumbele ya Umoja wa Afrika hususan juhudi za kupambana na UVIKO-19 ikiwemo upatikanaji na utengenezaji wa chanjo za ugonjwa huo barani Afrika pamoja na mikakati ya kunasua uchumi wa Afrika dhidi ya athari za UVIKO-19.

Wamekubaliana kushirikiana katika kutekeleza miradi ya kipaumbele ya Umoja wa Afrika yenye lengo la kuimarisha na kukuza Mtangamano wa Afrika hususan ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi, kuboresha mazingira ya biashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na juhudi za uimarishaji wa hali ya amani, usalama na utulivu barani Afrika.

Vilevile, wamekubaliana kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa mchakato mabadiliko ya kitaasisi ndani ya Umoja wa Afrika ili kuboresha utendaji wa umoja huo.

Aidha, Mhe. Balozi Shiyo alizungumzia kwa undani umuhimu wa kutekeleza maazimio mbalimbali ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya kuwezesha lugha ya  Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kikazi za umoja wa Afrika. Mhe. Mahamat alimhakikishia Mhe. Balozi Shiyo kuwa ataunga  mkono ombi la Tanzania kutaka lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za Kazi za Umoja wa Afrika.

Mhe. Mahamat alitumia fursa hiyo kutoa  salamu za shukurani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwalika kushiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 09 Desemba 2021 na zaidi kwa kukubali kuonana naye tarehe 10 Desemba, 2021 ambapo alipata fursa ya kumwelezea Mhe. Rais kuhusu maeneo  mbalimbali ya kipaombele ndani ya Umoja wa Afrika na Afrika kwa ujumla.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Eugene Shiyo amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Eugene Shiyo akiwa katika picha ya pamoja na  Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.

 Picha ya pamoja